KINGAZI BLOG: 06/01/16

KARIBU UHABARIKE KIGANJANI MWAKO.

Breaking News
Loading...

Wednesday, June 01, 2016

Mzee Majuto akanusha kustaafu kuigiza


Msanii wa filamu za kuchekesha, King Majuto amekanusha taarifa ambazo zilizagaa katika mitandao ya kijamii kwamba amestaafu kuigiza.

Akiongea katika kipindi cha Clouds E cha Clouds TV Jumatano hii, Mzee Majuto amedai sio kweli kwamba amestaafu kuigiza ila kuna baadhi ya filamu ambazo hatafanya tena.

“Watu wameniwekea maneno mdomoni, sijasema nimeacha kuigiza,” alisema Majuto.“Wakati nipo Hija mwaka jana nilikuwa nafikiria niache kabisa kuigiza, lakini baada ya kurudi nikaona nalazimika kuendelea kuigiza ili nipate pesa za kuendesha maisha yangu, kwa sababu bila filamu nitakufa njaa,”

Pia muigizaji huyo amesema hafanyi tena stand up comedy kwa kuwa wakati anafanya kuna matukio ambayo yatakuwa yanaendelea katika ukumbi ambayo dini yake hayaruhusiwi.

Pia Majuto amewataka mashabiki wa filamu zake kuendelea kusubiria kazi zake ambazo atakuwa anaandaa mwenyewe.

WAZIRI WA MAGUFULI ASEMA WATANZANIA 408 WAFUNGWA KWAJILI YA MADAWA YA KULEVYA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Augustine Mahiga

Dodoma:

Watanzania 408 wanatumikia vifungo nje ya nchi na wengine kukabiliwa na adhabu ya kifo baada ya kusafirisha  dawa za kulevya.

Taarifa hiyo imetolewa bungeni leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Augustine Mahiga alipokuwa akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Akizungumzia Watanzania waliokamatwa kwa dawa hizo Mahiga amesema wanakabiliwa na adhabu hizo katika magereza mbalimbali duniani baada ya kukutwa na hatia ya makosa ya kujihusisha na biashara haramu.

Mahinga alitaja idadi yao na nchi ambazo wanashikiliwa kuwa ni Brazil (41), China (266), Iran (68), India (9), Nepal (4), Oman(3), Thailand (14) na Umoja wa Falme za Kiarabu (3).

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano ya June 1




Mbowe: Tupo Tayari Kutimuliwa Wote Bungeni

Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson sasa amesababisha makubwa zaidi; wabunge kutoka vyama vya upinzani wako radhi kutimuliwa wote iwapo kiongozi huyo ataongoza vikao vyote vilivyosalia na wao kuendelea na msimamo wao wa kumsusia. 

Jana, Dk Ackson aliingia kuongoza kipindi cha maswali na majibu na wabunge wote wa vyama vya upinzani wakatoka ndani ya ukumbi na alipomuachia mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kuendelea na shughuli zilizosalia, walirejea ukumbini. 

“Kama Naibu Spika atakuwepo kwenye kile kiti, hatatuona bungeni, hata kama ni leo, ni kesho hata Bunge lote. Tuko tayari kuchukua gharama hiyo,” alisema kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe akiwa nje ya ukumbi wa Bunge baada ya kuongoza wabunge wenzake kutoka ukumbini wakati wa kipindi cha maswali na majibu. 

Kauli hiyo ya Mbowe imekuja siku moja baada ya Dk Ackson kukataa Bunge kujadili sakata la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) waliotimuliwa kwa maelezo kuwa hawafundishwi kwa muda mrefu kutokana na walimu wao kugoma wakidai malimbikizo yao. 

Kitendo cha Dk Ackson kukataa hoja hiyo ijadiliwe, kilisababisha vurugu bungeni kiasi cha kuita askari kuingia kuwatoa wabunge waliokuwa wakipiga kelele na baadaye kuwaamuru waliokataa kukaa waondoke ukumbini. 

Wakiwa nje, walifikia uamuzi wa kususia vikao vyote vitakavyoongozwa na Naibu Spika na wakaanza kutekeleza uamuzi huo jana asubuhi. 

Kauli ya Mbowe pia imekuja siku moja baada ya Kamati ya Maadili, Kinga na Haki za Bunge kuwasimamisha wabunge saba kutoka vyama vya upinzani kuhudhuria vikao vya kuanzia mkutano huu hadi ujao kwa maelezo kuwa walifanya fujo wakati wakipinga hoja ya Serikali ya kusimamisha matangazo ya moja kwa moja ya baadhi ya shughuli za Bunge. 

Jana, Mbowe alisema wako tayari kutimuliwa wote kama uamuzi huo utawapendeza viongozi wa Bunge kwa kuwa siasa inaweza kufanywa ndani na nje ya Bunge. 

Mbowe alisema kuwa hali ilishafika hatua nzuri ya kujenga demokrasia nchini na kwamba pamoja na matatizo yaliyokuwepo, hali ilikuwa ikienda vizuri. 

“Lakini tangu kuingia kwa Serikali ya Awamu ya Tano mnaweza kuona Bunge limegeuka kituko. Bunge limegeuka mahali pa kukomoana. Bunge limekuwa mahali pa kutishana,” alisema Mbowe. 

“Naibu Spika anaamua kusitisha mjadala wa maana ili apate muda wa kuwadhibiti na kuwafukuza wabunge bungeni na anaona sifa. 

Tunaacha kujadili hoja ya msingi kama mambo ya Udom. Watoto wadogo wanalala nje haoni ni muhimu, anaona muhimu ni kuwafukuza wabunge wa upinzani.” 

Mbowe, ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema hawezi kukaa, kumsikiliza na kumheshimu Dk Ackson, bali wapinzani wataheshimu anayewaheshimu bila kujali anatoka chama gani na hawatamuheshimu asiyewaheshimu bila kujali cheo chake. 

“Sasa leo (jana) tumekataa kushiriki kipindi cha maswali na majibu kwa sababu yeye (Dk Ackson) anasimamia kipindi hicho na akitoka tutarudi bungeni. 

Akija mwenyekiti, akija Spika mwenyewe tutarudi bungeni. Lakini kama Naibu Spika atakuwepo kwenye kile kiti hatatuona bungeni, hata kama ni leo, ni kesho hata Bunge lote. Tuko tayari kuchukua gharama hiyo,”alisema Mbowe.

Dk Ackson alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia Septemba mwaka 2015 hadi Novemba 2015 alipochukua fomu za kugombea uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya CCM. 

Siku moja kabla ya CCM kuchagua mgombea wake, Dk Ackson alijitoa, hatua iliyoonekana ni kumpisha kada mwenye uzoefu zaidi, Job Ndugai. 

Wakati CCM wakisubiri uchaguzi wa mgombea wao, Rais John Magufuli alimteua Dk Ackson kuwa mbunge na baadaye akachukua fomu za kuwania unaibu spika, akiwa mgombea pekee wa chama hicho. 

Tangu aanze kuongoza Bunge, Dk Ackson amekuwa akikwaruzana na wabunge wa upinzani, ambao walishawahi kuhusisha kuteuliwa kwake na Rais kuwa mbunge ili apate mwanya wa kugombea unaibu spika, na mpango wa Serikali kutaka kulidhibiti Bunge. 

Akizungumzia mkakati wao jana, Mbowe alisema kwa kuwa siasa haifanywi bungeni tu, watakwenda kwa wananchi kuwashitaki viongozi wa Bunge. 

Alisema watafanya hivyo kwa kuwa kitendo cha kuwafungia wabunge wa upinzani kuwatetea wananchi ndani ya Bunge, kinaweza kufanywa pia nje ya chombo hicho. 

“Tutawaamsha wananchi nje ya Bunge kwa kuwa ni fursa hivyo tunakutana na wabunge wote waliotimuliwa na tutaungana wote bila kujali chama cha siasa kwa kuwa tumekubaliana kusimamia ajenda ya nchi na si ya chama chochote,”alisema Mbowe. 

LHRC yataka wabunge warudishwe 

Wakati wabunge saba wakianza kutumikia adhabu ya kufungiwa kuhudhuria vikao, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelitaka Bunge kuwarejesha ili kuendelea na majukumu yao. 

Mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho, Dk Helen Kijo Bisimba alisema hoja ya kuwafukuza wabunge hao kwa sababu ya kudai haki ya kurushwa bunge ‘live’ ni kuwapokonya haki Watanzania waliowachagua kwenda kuwawakilisha bungeni. 

“Wabunge hao wamechaguliwa na wananchi na wanatetea bunge hilo kurushwa ‘live’ kwa maslahi ya wananchi waliowatuma, halafu kiti cha Spika kinaamua kuwafukuza bungeni. 

"Endapo ningepewa nafasi ya kuwashauri wapiga kura, ningewaambia kwenda kushiriki vikao vya Bunge wenyewe kwa sababu wabunge wao wameondolewa bungeni, hata mimi mbunge wangu wa Kawe ameondolewa,”alisema.

Taarifa toka Ikulu kuhusu uteuzi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO

TAARIFA KWA UMMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli, amemteua Dkt. Alex L. Kyaruzi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Kufuatia uteuzi huo, Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Profesa Sospeter M. Muhongo (Mb.), amewateua wafuatao kuwa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO kuanzia tarehe 31/5/2016 hadi tarehe 30/5/2019;
1.   Dkt. Samwel Nyantahe
2.   Dkt. Lugano Wilson
3.   Bw. David Elias Alal
4.   Mhandisi Stephen Peter Mabada
5.   Mhandisi Leonard R. Masanja

Aidha, Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Profesa Sospeter Muhongo (Mb) amekamilisha uteuzi wa Wajumbe wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kuanzia tarehe 30/5/2016 hadi 29/5/2019 wajumbe  hao ni :

    Bw. Abdalah H. Musa
    Dkt. Coretha Komba
    Bw. Felix M. Maagi
    Dkt. Lightness Mnzava
    Bw. John B. Seka

Uzinduzi wa Bodi hizo utafanyika Makao Makuu ya Mashiriki hayo Siku ya Alhamisi tarehe 2 Juni, 2016, saa 4:00 asubuhi kwa Bodi ya STAMICO na saa 8:00 mchana kwa Bodi ya TANESCO.

Imetolewa na;

KATIBU MKUU

31 MEI, 2016

RAIS MAGUFULI ASEMA SERIKALI ITAKOMESHA WATUMISHI NA WANAFUNZI HEWA



Rais John Magufuli.

RAIS John Magufuli (pichani) amesema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kumaliza makosa yote yaliyojitokeza huko nyuma ikiwemo tatizo la watumishi na wanafunzi hewa lililoibuka hivi karibuni.Amewataka Watanzania kuacha kuingiza siasa kwenye makosa yanapojitokeza, hasa yale yanayogusa sehemu nyeti kama elimu, kwani yakiachwa kuna uwezekano wa kutengeneza taifa la watu wa ajabu.Alisema tangu aingie madarakani amekumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo matatizo ya rushwa, ukwepaji kodi, watumishi hewa na sasa amekumbana na tatizo la wanafunzi hewa.“Nchi yetu ina changamoto na mambo mengi sana hata mimi nimekumbana na changamoto naziona mwenyewe, nikigeuka hivi watumishi hewa ambao hadi sasa wamefikia 10,500, nikigeuka hivi kuna wanafunzi hewa,” alisisitiza.Alisema ni Tanzania pekee ambayo mtu anaweza kupata daraja la nne kidato cha nne katika elimu ya sekondari, halafu akapata fursa ya kujiunga na chuo kikuu na kupatiwa mkopo wa serikali, wakati mhitimu aliyefaulu kidato cha sita akikosa fursa hiyo.

Alisema endapo kulifanyika makosa lazima yarekebishwe, kwani inafahamika fika mtu akimaliza kidato cha nne akifeli ataanzia ngazi ya Astashahada, Stashahada ndio apate nafasi ya kujiunga chuo kikuu.“Sasa hapa kwetu ni tofauti ukifeli kidato cha nne unajiunga chuo kikuu,” alihoji na kuwataka watu waache siasa kwenye makosa kwani mambo kama hayo yakiachwa kuna hatari ya nchi kutengeneza taifa la ajabu.

Hivi karibuni, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako aliivunja Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kuwasimamisha kazi viongozi wanne waandamizi kwa tuhuma za kudahili wanafunzi wasio na sifa.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya TCU, Awadh Mawenya naye alisimamishwa kazi kwa kosa la kushindwa kuwachukulia hatua watumishi waliodahili wanafunzi hao wasio na sifa.

Profesa Ndalichako alichukua hatua hizo baada ya TCU kudahili wanafunzi 489 waliopata daraja la 4.32 katika mitihani yao ya kidato cha nne lakini walijiunga na chuo kikuu na kupatiwa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 784.

Wahadhiri UDOM Wataja Kiini cha Mgomo Kilichosababisha Wanafunzi 7802 Warudishwe Nyumbani



JUMUIYA ya Wanataaluma ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA) imesema kilichotokea si walimu kugoma kufundisha programu ya Stashahada Maalumu ya Elimu, Sayansi, Hisabati na Tehama, bali tatizo ni kutoelewana na Menejimenti ya chuo kutokana na mazingira mabovu ya uendeshaji wa programu hiyo chuoni hapo.

Aidha, imelaani kitendo cha wanafunzi 7,802 wa Programu Maalumu ya Ualimu wa Msingi na Sekondari, waliorudishwa nyumbani bila kupewa muda wa kutosha kujiandaa kwa kuzingatia umri wao na mazingira waliyokuwa wanaishi, hali inayofanya wazagae mitaani huku wakiwa hawana pa kwenda.

Hayo yako kwenye tamko lililotolewa jana na Katibu wa jumuiya hiyo, Lameck Thomas, ambalo lilieleza kuwa lawama zimekuwa zikitupwa kwa walimu kutokana na taarifa hizo kutolewa na upande mmoja, ambao ni Menejimenti ya chuo kwenda serikalini bila kuwepo na taarifa yoyote kutoka kwa walimu kupitia jumuiya yao.

Thomas alisema si kweli kama walimu waligoma kufundisha lakini tatizo kubwa ni kutoelewana kati ya walimu na Menejimenti ya chuo kutokana na mazingira mabovu ya uendeshaji wa programu hiyo chuoni hapo.

"Hatuzungumzii fedha zaidi tunazungumzia suala la kuboresha elimu ili taifa lipate walimu wa baadaye katika kufundisha Sayansi, Hisabati na Tehama, vifaa vya kufundishia navyo ni changamoto kubwa,” alisema.

Katibu huyo alisema kama Jumuiya ya Wanataaluma wanapata hisia kwamba Wizara ya Elimu, imeamua kwa makusudi kushirikiana na uongozi wa chuo kupotosha uhalisia wa jambo hilo kwani hakuna hata wakati moja ambao wamefanya mawasiliano na walimu wenyewe kupata ukweli kutoka upande wao.

“Alichosema waziri bungeni juzi ni taarifa ya upande mmoja ambayo haitatupeleka kwenye utatuzi wa kudumu wa suala hili kutokana na ukweli kwamba walimu nao wana mengi ya kuzungumza,” alisema katibu huyo.

Alisema serikali imejenga desturi ya kuonana na menejimenti za vyuo pindi yanapotokea matatizo bila kupata taarifa kutoka vyanzo vingine hali ambayo imekuwa inasababisha vyanzo sahihi vya matatizo kutojulikana kwa uwazi.

Alisema changamoto za ufundishaji kutokana na uhaba na walimu kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo. Akitoa mfano alisema kwa sasa Chuo cha Sayansi Asilia na Hesabu, kina upungufu wa walimu 128 waliokuwa wanahitajika kufundisha programu hiyo kwa ufanisi; na kwa muhula uliopita walimu 72 tu ndio walibeba mzigo wa upungufu huo na muhula huu hali ilikuwa inaelekea kuwa mbaya zaidi.

“Wingi wa wanafunzi na uhaba huu wa walimu ulisababisha upangaji wa ratiba na kufundisha kutokana na ukweli kwamba kozi ziligawanywa katika mikondo mingi ambayo walimu walilazimishwa kuifundisha huku wakiwa na majukumu ya kufundisha kozi za shahada na majukumu mengine,” alifafanua.

Alisema chuo kimekuwa na desturi ya kupokea wanafunzi wengi bila kuzingatia idadi ya walimu waliopo na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia na hiyo si mara ya kwanza kwa chuo kufanya hivyo, kwani mwaka 2008 walileta wanafunzi wengi ambao matokeo yake walimu kufundisha masomo mengi kuliko uwezo wao wa kazi.

Alisema taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma ilipotoshwa, kwani haijaeleza ukweli wa madai uliowasilishwa na chuo husika. 

Alisema katika Chuo cha Sayansi Asilia na Hesabu taarifa inasema yaliyowasilishwa ni madai ya Sh milioni 367.8 na kupungua mpaka Sh milioni 90 wakati uhalisia ni kwamba madai hayo hata yangebanwa namna gani yasingepungua mpaka chini ya Sh milioni 223.7.

Alisema mfano mwingine ni Chuo cha Elimu Masafa na Sayansi za Kompyuta ambao taarifa inasema waliwasilisha madai yanayozidi Sh milioni 100 wakati taarifa ya chuo inasema ni madai ya Sh milioni 53.7 tu.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Edson Baradyana alisikitishwa na yaliyotokea na kuitaka serikali kufanya jitihada za makusudi ili kumaliza mgogoro huo na hilo litawezekana kama walimu, wanafunzi na Menejimenti kukaa pamoja.

Baradyana alisema wanafunzi hawakutendewa haki kwani ilitolewa notisi ya ghafla ya kuondoka chuoni huku wengine wakiwa hawana nauli na hawakujua pa kwenda hali inayofanya waendelee kuzurura mitaani.

Alisema wanaamini kama Menejimenti ya chuo ingeonesha ushirikiano wa karibu kwa walimu wanaofundisha programu hiyo na kushirikiana, hayo yasingetokea au yasingekuwa makubwa kiasi hicho.

“Lazima kuangaliwa na kutatuliwa kwa changamoto nyingine zilizoibuliwa na wanataaluma na wanafunzi katika uendeshaji wa programu hiyo badala ya kujikita kwenye suala la malipo tu, serikali iwe na utaratibu wa kuwasiliana na walimu na wanafunzi mara kunapotokea matatizo vyuoni ili kupata taarifa toshelezi kutoka pande zote,” alisema Mwenyekiti wa Udomasa.

Aidha, wakati wa kurejeshwa nyumbani kwa wanafunzi hao wa Udom kukibebwa kisiasa na vyama vya upinzani, taarifa ya serikali imeeleza kuwa wahadhiri waliogoma, walitaka kulipwa posho ya zaidi ya Sh milioni 900.

Akitoa taarifa ya pili bungeni juzi usiku, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako  alisema wanafunzi hao si sehemu ya kazi zilizoko katika mikataba ya ajira ya wahadhiri hao, ila ni sehemu ya kazi ya ziada.

Kwa kuwa kazi hiyo ni ya ziada, Profesa Ndalichako alisema walikubaliana walipwe posho ya kazi ya nyongeza ambayo uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ulikuwa tayari kutoa zaidi ya Sh milioni 200.

Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, wahadhiri hao walisisitiza kuwa wanataka posho hiyo iwe zaidi ya Sh milioni 900, jambo lililokataliwa na Mkaguzi wa Ndani wa Mahesabu wa Udom aliyesema kuwa kiwango hicho ni kikubwa kuliko uhalisia wa kazi yenyewe.

Kutokana na kutokubaliana kati ya wahadhiri hao na uongozi wa Udom, wahadhiri hao ndio wakaitisha mgomo wa kufundisha wanafunzi hao huku wakiendelea na kazi za kufundisha walio katika programu za shahada ya kwanza na kuendelea.

Profesa Ndalichako alisema kwa uamuzi huo wa wahadhiri, serikali isingeweza kuwachukulia hatua kwa kuwa wamegomea kazi ya ziada na si kazi waliyoajiriwa na kuingia mkataba na chuo.

Kwa hali hiyo, Profesa Ndalichako alisema serikali ililazimika kuingilia kati ambapo Mei 10, mwaka huu Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya alikwenda chuoni hapo kutafuta suluhu.

Mbali na Naibu Waziri, alisema hata makatibu wakuu wa wizara hiyo nao walikwenda kuzungumza na wahadhiri hao bila mafanikio, huku wanafunzi hao wakikaa chuoni bila kuingia darasani kwa wiki ya tatu.

Profesa Ndalichako alisema mbali na madai ya wahadhiri hao, pia wakati wa kutafuta suluhu ya jambo hilo, walitazama suala la tija kwa wanafunzi hao wa diploma maalumu ambao ni zaidi ya 7,800 na pia kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza ambao pia wanapaswa kufundishwa na wahadhiri hao.

Kutokana na kukosa masomo kwa wiki tatu mfululizo na kuwepo kwa uwezekano wa kukosekana tija katika ufundishaji, Profesa Ndalichako alisema ndio uamuzi wa kuwarudisha nyumbani wanafunzi hao ukafanyika ili serikali iangalie upya utaratibu wenye tija zaidi wa kuwaendeleza wanafunzi hao.

Aidha, Profesa Ndalichako alisema wakati wanafunzi hao wakitakiwa kurudi nyumbani, walizingatia hali yao ya kipato, kwa kuwa tayari walikuwa wameshapewa fedha za kujikimu za siku 60 tangu Aprili 21, mwaka huu. 

Profesa Ndalichako aliwataka wanafunzi hao kuvuta subira wakati serikali inatafuta namna bora ya kuwapatia elimu hiyo kwa kuzingatia tija kwao.

 

Gallery

Popular Posts

About Us