KINGAZI BLOG: 07/15/16

KARIBU UHABARIKE KIGANJANI MWAKO.

Breaking News
Loading...

Friday, July 15, 2016

Pingamizi la Tundu Lissu Kutaka Afutiwe Kesi ya Uchochezi Lagonga Mwamba


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) ya kufutiwa mashitaka ya uchochezi yanayomkabili na wenzake watatu.

Hakimu Mkazi Mkuu, Emillius Mchauru alitoa uamuzi huo jana baada ya kukubali pingamizi lililowasilishwa na upande wa Jamhuri waliodai mashitaka hayo yasifutwe kwa kuwa hati ya mashitaka haina makosa.

Mbali ya Lissu, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni mwandishi wa gazeti la Mawio, Jabir Idrissa, Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob. Hata hivyo, uamuzi huo ulitolewa jana bila Lissu kufika mahakamani hapo kwa kuwa anaumwa.

Akiieleza mahakama, Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alidai Lissu ameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa anaumwa, lakini wadhamini wake akiwemo Ibrahim Ahmed wamefika mahakamani na kueleza kuwa Lissu anaumwa malaria. Aidha, ilielezwa kuwa mshtakiwa Idrissa anaumwa na yupo Zanzibar kwa ajili ya matibabu.

Katika maombi yao, washitakiwa kupitia kwa Wakili Kibatala waliiomba mahakama ifute mashitaka hayo kwa kuwa hati ya mashitaka imekosewa kwa kutokueleza makosa hayo wametenda wapi na pia mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza masuala yanayohusu Zanzibar.

Akisoma uamuzi, Hakimu Simba alisema baada ya mahakama kupitia hoja za pande zote mbili katika kesi hiyo imejiridhisha kuwa hati ya mashitaka haina makosa.

Aidha, alisema mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa makosa yaliyofanyika yanahusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivi karibuni, mahakama ilifuta mashitaka mawili ya uchochezi kati ya matano yanayowakabili washitakiwa hao, baada ya upande wa jamhuri kuyaondoa katika hati kwa kuwa hayana kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Katika mashitaka yao inadaiwa Januari 12 hadi 14, 2016, Dar es Salaam washitakiwa walichapisha taarifa ya uchochezi yenye kichwa cha habari ‘ Machafuko yaja Zanzibar’.

Pia inadaiwa Januari 14, 2016 Dar es Salaam walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar. Inaendelea kudaiwa siku hiyo hiyo, Lissu na wenzake bila ya kuwa na mamlaka yoyote yale waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar ili wasikubali kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

PICHA 5 ZA NDOA YA ZITTO KABWE ILIYOFANYIKA ZANZIBAR

Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe jana aliuacha rasmi ukapera baada ya kufunga ndoa na mpenzi wake aliyemvisha pete ya uchumba miezi miwili iliyopita, ndoa na tafrija zote zilifanyika Zanzibar.


MAGAZETI YA LEO IJUMAA JULAI 15 KWENYE HEADLINES ZA KITAIFA KIMATAIFA MICHEZO N.K





RAIS MAGUFULI AANZA SAFARI YA KUHAMIA DODOMA

RAIS John Magufuli ameonesha nia ya kuhamia Dodoma kwa kuanza kushughulikia masuala muhimu, ikiwamo ya kuzindua awamu ya kwanza ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma na kuhamishia maadhimisho ya Siku ya Mashujaa mkoani Dodoma.
Akizungumza juzi wakati wa mkutano wa kitaifa wa amani ulioandaliwa na Jumuiya ya Ahamadiyya, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema katika kuonesha dhamira ya kuhamia Dodoma ambao ulitangazwa kuwa Makao Makuu ya Tanzania miaka ya 1970, Rais alielekeza fedha zilizobaki kwenye bajeti iliyopita zitumike kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege ambao pia ujenzi wake utazinduliwa na Rais mwenyewe Julai 22, mwaka huu.Aidha, Rugimbana alisema Rais Magufuli pia ameagiza maadhimisho ya Siku ya Mashujaa mwaka huu yahamie Dodoma ambapo kwa miaka mingi sasa yamekuwa ikifanyika kwenye Viwanja vya Mashujaa, Mnazi Mmoja Dar es Salaam.“Ndio natoka kwenye kikao cha kuzungumzia maadhimisho hayo kufanyika Dodoma hilo linadhihirisha wazi dhamira ya Rais kuhamia Dodoma,” alisema Rugimbana na kuongeza kuwa Rais Magufuli atashiriki Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) utakaoanza Julai 23, mwaka huu.
Akizungumzia suala la amani, mkuu huyo wa mkoa alisema serikali itawachukulia hatua kali viongozi wa taasisi mbalimbali ambao wamekuwa na tabia za kutumia nafasi zao kuhubiri uchochezi na hivyo kutishia amani na utulivu wa nchi.
Alisema viongozi ambao wamekuwa na tabia za kutumia taasisi zao kama sehemu ya kuhubiri masuala ya uovu, ikiwemo kushawishi vitendo vya uvunjifu wa amani, serikali haitawafumbia macho.Aliwataka viongozi wa dini nchini kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Katiba za taasisi zao na siyo kufanya mambo kwa maslahi yao binafsi na tamaa. Alisema pia serikali inaunga mkono jitihada za taasisi za dini katika kuhubiri amani na utulivu wa nchi ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi mbalimbali.“Kama serikali, tunaunga makono jitihada zenu mbalimbali ikiwemo kupinga vitendo vya maovu pamoja na ufisadi ambao umekuwa ukilitafuna taifa letu,” alisema.
Naye Mwakilishi wa Jumuiya hiyo ya Ahmadiyya, Abdulrahman Ahmed akitoa mada kuhusu amani, alisema Waislamu wanatakiwa kuzingatia miiko ambayo imewekwa na dini hiyo katika kusaidia kudumisha amani na utulivu.
Wakati huo huo, mapema wiki hii Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema serikali inakarabati na kuongeza ukubwa wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma ili upokee ndege kubwa za mizigo, abiria na viongozi wa kitaifa na kimataifa, ikiwa ni maandalizi ya kuufanya mkoa kuwa makao makuu ya nchi kivitendo.
Ujenzi huo unatarajia kugharimu kiasi cha Sh bilioni 11.5 ambazo ni fedha za ndani na utakamilika kwa muda mfupi ili kutoa fursa kwa mashirika ya ndege kuanza huduma mkoani Dodoma, ikiwemo ndege kubwa zitakazonunuliwa na serikali mwaka huu.
Profesa Mbarawa akizungumza baada ya kukagua uwanja huo alisema uamuzi huo unafikiwa kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano kutaka kuufanya Dodoma makao makuu ya nchi kivitendo, jambo linalotarajiwa kuongezeka shughuli mbalimbali zikiwemo za kiutawala, uchumi, biashara na diplomasia sambamba idadi ya wageni.
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Upanuzi wa uwanja huo kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mbila Mdemu alisema mpaka sasa mita 900 zimekamilika kwa kuweka tabaka la kwanza lami katika eneo la kuruka na kutua ndege na kazi ya kuchimba na kusawazisha eneo la kurefusha njia imekamilika.
Alisema wanatarajia kukamilisha kazi hiyo kwa muda mfupi. Upanuzi wa uwanja huo unahusisha njia ya kuruka na kutua kwa ndege yenye urefu wa Km 2.5 na mita 500 za taa za kuongozea ndege na usalama wa kuruka kwa ndege.

 

Gallery

Popular Posts

About Us