KINGAZI BLOG: 08/24/16

KARIBU UHABARIKE KIGANJANI MWAKO.

Breaking News
Loading...

Wednesday, August 24, 2016

Jeshi La Polisi Lahusisha Mauaji ya Polisi Wanne na Sakata la Oparesheni UKUTA.........Lapiga Marufuku Mikutano yote ya Ndani ya Vyama vya Siasa

KUFUATIA mauaji ya askari wanne yaliyotokea Kata ya Mbande Temeke kwa watu wanaodhaniwa ni majambazi kuvamia benki ya CRDB na kuwaua askari hao kwa kutumia silaha za moto jeshi la Polisi limetangaza kiama na kuwataka wahusika wote kujisalimisha.

Katika hatua nyingine jeshi la polisi limehusisha tukio hilo na Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA) kufuatia matamko ya baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao wamesikika katika majukwaa ya kisiasa wakihamasisha wafuasi wao wawashambulie askari wa Jeshi la Polisi.

Kauli hiyo imetolewa  na Kamishna Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Nsato Marijan Mssanzya (CP), wakati akizungumza waandishi wa habari Dar es Salaam leo mchana ambapo pia alikiri kuwa mazoezi yanayofanywa na polisi yamelenga kukabiliana na Ukuta.

Akizungumza kwa hisia CP Mssanzya pia amepiga marufuku  mikutano ya ndani yenye viashiria vya uchochezi na hata ikifanyika kwenye majukwaa watamshusha muhusika na kumfikisha kwenye mkono wa sheria.

Amesema Jeshi  hilo limebaini kwamba mikutano hiyo imekuwa ikitumika kuchochea wananchi na kuwahamasisha kuvunja sheria za nchi na kufanya mapambano na jeshi la polisi

"Kwasababu hiyo basi,kwa hali ya kutumia mikutano ya ndani kuchochea watu kuvunja sheria na kupambana na askari, hivyo basi kuanzia sasa jeshi la polisi nchini linapiga marufuku mikutano yote ya ndaniamesema.
 

Aidha CP  Mssanzya  aliwataja askari waliouawa katika tukio hilo wakati wakibadilishana lindo kuwa ni  E.5761 CPL Yahya, F.4660 CPL Hatibu, G 9524 PC Tito na G 9996 PC Gastoni na raia wawili waliojeruhiwa aliowataja kuwa Ali Chiponda na Azizi Yahya wote wakiwa wakazi wa Mbande.

"Katika tukio hilo majambazi ambao idadi yao haikufahamika walifanikiwa kupora silaha mbili aina ya MSG na lisasi 60 na hakuna pesa wala mali ya benki hiyo kuibiwa au kuharibiwa, ni dhahiri kuwa waharifu hao walikuwa na kusudio moja tu la kuwashambiulia askari polisi, "alisema.

Alisema katika hali ya kushangaza baada ya tukio hilo kuna baadhi ya watu waliandika mitandaoni kubeza na kukeji mazoezi ya kawaida ya jeshi la polisi na wengine waliandika ujembe wa kushabikia tukio hilo la kuuawa kwa askari polisi huku wengine wakidiriki kuandika ujumbe unaosema endapo watapigwa na polisi Septemba1 mwaka huu basi viongozi wa jeshi hilo wawaondoe askari wanaoishi uraiani na kuwarudisha kambini.

Aliongeza kuwa jeshi la polisi limejipanga vyema kukabiliana na matukio yote ya uvunjifu wa amani nchini.

Waandishi wa habari wakichukua taarifa hiyo.



Kingunge Awataka Mkapa na Mwinyi Wamshauri JPM Azungumze na Chadema


ALIYEKUWA kada wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru  amewaomba  marais wastaafu, Rais Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa kuzungumza na Rais John Magufuli ili aitishe kikao kati ya Serikali na Chadema kwa ajili ya kusitisha maandamano yaliyopangwa kufanyika Septemba Mosi.

Kingunge  ametoa kauli hii  leo nyumbani kwake jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari  wakati akiongelea  mvutano kati ya Chadema na serikali unaoendelea kwa sasa.

Chadema kimeingia kwenye mvutano mkubwa na serikali kutokana na dhamira yake ya kufanya mikutano na maandamano nchi nzima chini ya mwavuli wa Umoja wa Kupinga Udikteta (Ukuta).

Hivi karibuni, Rais John Magufuli alisisitiza kutoruhusu maandamano na mikutano ya kisiasa na kuagiza kuwa, wanaotaka kufanya mikutano wafanye ndani ya mipaka ya majimbo yao na si vinginevyo jambo ambalo Chadema wanapinga.

Hali hiyo imeibua mtikisiko mkubwa nchini huku kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini, wanasiasa, wasomi na wananchi wa kawaida wakitaka kupatikana suluhu kabla ya Septemba Mosi, tarehe iliyopangwa kuanza maandamano na mikutano hiyo.

Kwenye mkutano wake na wanahabari Kingunge anawalaumu viongozi wastaafu wakiwemo marais pamoja na mawaziri wakuu kwa kukaa kimwa wakati huu ambao nchi inatikishwa huku Katiba ya Jamhuri ikisiginwa.

Miongoni mwa viongozi wanaolalamikiwa kutosikika ama kuchukua hatua zozote ili kuilinda Katiba ni pamoja na Marais Wastaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Aman Abeid Karume (Zanzibar).

Viongozi wengine waliotajwa ni Mawaziri Wakuu Wastaafu, Cleopa Msuya; Jaji Mstaafu, Joseph Warioba.

“Mzee Mwinyi yupo kimya, Mkapa kimya, Warioba kimya, Cleopa Msuya kimya, Amani Karume kimya,” amesema Kingunge na kuongeza;

 

“Ukimya huu unatokana na nini? Hawa wote waliwahi kula viapo vya utii kwa Katiba. Mimi nahoji, wazee wenzangu vipi mnakuwa kimya? Nawaambia kuwa mnachofanya si sawa.

 

“Naomba wazee wote tujitokeze kuhesabiwa katika hili la uvunjifu wa Katiba na sheria.”

Kingunge ambaye alihamia Chadema akitokea CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kutokana na kutoridhishwa na namna mchakato wa kumpata mgombea urais kutoka chama hicho amesema, Chadema inatumia haki yake ya kikatiba.

“Naomba Rais Magufuli, akubali kuitisha kikao na Chadema ambacho pia wazee wastaafu watahudhuria, akifanya hivyo hata sisi wazee tutawageukia Chadema na kuwambia wasitishe mpango wao wa maandamano,” amesema.

Amesema kwamba, kibaya zaidi Jeshi la Polisi linaandaa bunduki kwa ajili ya kupambana na raia ambao hawana kitu na kuwa, hali hiyo haipaswi kuvumiliwa.

Mwanasiasa huo amesema, Chadema wameamua kutetea haki yao ya kikatiba na kisheria kwa kufanyaa maandamano kote nchini, na kina wafuasi wengi hivyo si jambo la kubeza.

“Upande wa pili, lipo Jeshi la Polisi na watawala ambao wanaahidi kuwakabili. Kwa bahati mbaya polisi na watawala hawatetei Katiba wala Sheria,” amesema.

Amesema kuwa, Tanzania kwa sasa inakabiliwa na ombwe la uongozi na kwamba, nchi imekosa watawala wenye sifa thabiti ya kuongoza taifa.

“Kwa hakika, tatizo kubwa la sasa la nchi yetu ni ombwe la kiuongozi, kwasababu kama ni watawala tunao kweli kweli, lakini tunachokosa ni watawala wenye maarifa ya kiuongozi.

 

“Inashangaza kuona wazee wastaafu kukaa kimya wakati nchi inakabiliwa na tatizo linaloweza kutuangamiza.

 

“Upande mmoja unanoa mapanga, unaanda bunduki kwa ajili ya kuchinja na kuua na upande wa pili wapo raia tu, tena wasio na silaha zozote.”

Kingunge anasema, wananchi ambao serikali na Jeshi la Polisi wanajiandaa kupambana nao, wanalilia Katiba na sheria zifuatwe.

“Laiti kama Chadema wangekuwa hawatetei Katiba na sheria, kungekuwa na kila sababu ya kuwashughulikia, lakini kwa kuwa wanatetea Katiba na sheria, kuna umuhimu wa kuyapa uzito madai yao,” amesema Kingunge.

Mwanasiasa huyo amesema kuwa, mvutano wa sasa sio wa Chadema na serikali isipokuwa ni suala la wananchi wote wa wenye mapenzi mema na taifa lao.

 

“Hili ni suala la kila mtu anayependa utawala wa Katiba, Sheria na Utawala Bora,” amesema.

MAAJABUUU!! !!WANAUME WAZAA MAPACHA WATATU KWA KUPANDIKIZA


WANAUME wawili wanaoishi kama mume na mke (mashoga) nchini Afrika Kusini wanasemekana kuwa watu wa kwanza katika ukanda huo na huenda duniani kwa kuwa wazazi wa mapacha watatu, wawili wakiwa wanafanana, kwa kupitia mtu mwingine aliyebeba mimba.
Wazazi hao ambao walikuwa majirani na mwanamichezo za zamani mlemavu, Oscar Pistorius, walikutana na mtu waliyempatia mbegu zao wakati wa mashitaka ya mauaji yaliyokuwa yanamkabili.
Christo na Theo Menelaou wamewachukua watoto wao nyumbani kwao mjini Pretoria baada ya kukaa hospitali kwa wiki tatu za matatizo. Kutokana na kuzaliwa kabla ya wakati wao, Julai 2, mapacha hao walijikuta maisha yao yakining’inia kati ya uhai na kifo.

 

Joshua alikuwa mtoto wa kwanza kuzaliwa kwa njia ya upasuaji na ndiye alikuwa mzito kuliko wote akiwa na uzito wa kilo 1.8; Zoe alifuatia akiwa na kilo 1.3 na Kate aliyekuwa na kilo 1.3 pia.
Watoto hao waliwekwa kwenye mashine za kuwasaidia kupumua hadi walipokuwa na nguvu za kutosha na kuweza kuondoka katika hospitali ya Sunninghill ya Johannesburg.
Waliondoka siku tofauti kwenda nyumbani, ambapo Joshua alikuwa wa kwanza kuruhusiwa siku ya Julai 22, akafuata Zoe aliyeruhusiwa siku kumi baadaye na Kate ambaye aliruhusiwa Agosti 4.
Christo Menelaou aliliambia shirika la utangazaji la Sky News: “Ukiwa shoga, siku zote unafikiri kwamba haiwezekani ukawa mzazi hata kama una upendo kiasi gani.
“Ni vigumu kupewa mtoto wa kuasili na kila mara tuliambiwa kwamba ni wazazi wa kawaida tu ndiyo huruhusiwa. Pia hatukuweza kufikiri kwamba tungempata mtu ambaye angekubali kubeba mbegu za mashoga.
Hata hivyo, mama mmoja mwenye watoto watatu, waliyekutana naye wakati wa mashitaka ya Pistorious, alikubali kutubebea mbegu zetu.”
Sheria za Afrika Kusini kuhusu upandikizaji wa mbegu kwa watu wengine, iliwataka wanaume wote wawili hao, mtu mwenye kubeba mbegu zao na mumewe wasaini mkataba mbele ya jaji kusisitiza kwamba walikubaliana kwa hiari katika jambo hilo na kwamba pasingekuwepo na kupeana fedha au kubeba gharama zozote.
Wawili hao walikwenda kwenye benki ya mayai na kuchagua mayai ambapo yai moja lilirutubishika na mbegu ya Christo na kuwekwa katika tumbo la mbeba mimba na baadaye aliwekewa yai lililokuwa na mbegu ya Theo.
Baada ya wiki kumi za mimba hiyo, uchunguzi ulionyesha kwamba moja ya mayai hayo yaliyorutubishika lilikuwa limejitenga na mbeba mimba alikuwa ana mapacha watatu, wawili wakiwa ni wenye kufanana.
Wakati ambapo madaktari wengi waliwashauri wanaume hao kwamba mbeba mimba huyo akatishe uhai wa mapacha wawili ili kutoa fursa ya mtoto wa tatu kuendelea bila matatizo, hatimaye walimpata mtaalam wa masuala ya watoto ambaye alisema angewasaidia jinsi ya kuhakikisha watoto hao wanazaliwa salama.Dk Heidra Dahms, ambaye ni mtaalam wa masuala ya watoto katika Hospitali ya Sunninghill na aliyesimamia kuzaliwa kwa watoto hao, aliliambia shirika la Sky News : “Ni jambo adimu sana. Sijawahi kusikia kitu kama hicho hata siku moja.”Watoto walikuwa ni wadogo mno, mapafu yao yalihitaji msaada wa ziada ili kupumua na Theo alilazimikakulala kando ya kitanda hadi walipopata nguvu.Hata hivyo, wazazi hao wanakabiliwa na changamoto ya kumfanyia upasuaji Zoe kutokana na kasorokwenye moyo, upasuaji ambao unahitajika kufanyika katika kipindi cha miezi sita.
Pamoja na yote hayo, wawili hao wanasherehekea kuitwa ‘baba’, jambo ambalo hawakutegemea kamwe lingewezekana.
Hivi sasa wanaendelea kuwatunza watoto wao hao watatu nyumbani kwao kwa msaada wa mayaya wawili usiku na mchana ambapo kila mtoto amefungwa kidude kinachotoa sauti iwapo watashindwa kupumua.
Theo alisema: “Tunalazimika kuwasugua taratibu kwenye migongo yao au kutekenya vidole vyao ili kuwakumbusha kupumua.
“Tunajisikie tumebarikiwa sana,” alisema kwa furaha.

DIAMOND PLATINUMS NA ALI KIBA USO KWA USO,SASA WASHINDANISWA TUZO HII 2016


Diamond Platnumz na Alikiba watachuana mwaka huu kuwania kipengele cha Best Male Eastern Africa kwenye tuzo za All Africa Music [Awards] 2016 za nchini Nigeria.
Waandaji wa tuzo hizo wametoa orodha ya kwanza ya wasanii wanaowania mwaka huu.

Diamond na Kiba wana upinzani pia kutoka kwa Bebe Cool, Eddy Kenzo, Jose Chameleone na Navio wa Uganda. Hata hivyo hakuna msanii wa Tanzania aliyetajwa kwenye kipengele hicho upande wa wanawake.

Tuzo hizo zitatolewa mwezi November jijini Lagos, Nigeria.

Hatutamvumilia atakaye vuruga amani - Majaliwa

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha inalinda amani ya nchi kwa gharama zozote na kamwe haitoruhusu mwanasiasa yeyote kusababisha vurugu zitakazochochea uvunjifu wa amani.

“Hatuzuii kuwa na vyama vya siasa ila haturuhusu vurugu kupitia vyama vya siasa na hakuna jambo lisilokuwa na mipaka. Mambo ya kuhamasishana kufanya vurugu hatutayaruhusu, tunataka watu wafanye kazi,” alisisitiza.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Agosti 23, 2016) wakati akizungumza na viongozi wa dini pamoja na wazee wa mkoa wa Rukwa mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

Alisema Serikali inataka Watanzania wawe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi zao za kuwaingizia kipato na kuwaletea tija, hivyo suala la kudumisha amani ni muhimu kwani vurugu zikitokea hawatakuwa na mahali pa kukimbilia na hakuna shughuli ya maendeleo itakayofanyika.

“Suala la uhamasishaji wananchi juu ya utunzaji wa amani ni la lazima hivyo viongozi wa dini na wazee kwa pamoja tushirikiane katika kukemea vitendo vya uchochezi kwasababu vurugu zikitokea Watanzania hatuna mahali pa kukimbilia,” alisema.

Aidha, Waziri Mkuu aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa pamoja na viongozi wake kwa sababu kazi ya uongozi ni ngumu na inachangamoto nyingi.Pia aliwaagiza viongozi wa dini wa mkoa wa Rukwa kuharakisha uundwaji wa Kamati ya Amani ya mkoa huo.

Awali, Sheikh wa mkoa wa Rukwa, Sheikh Rashid Akilimali amesema madhehebu ya dini hayawezi kuvuruga amani ya nchi ila anahofu na viongozi wa vyama vya siasa kutokana na vitendo vyao vya kuhamasisha vurugu.

Kufuatia hali hiyo Sheikh Akilimali aliwaomba wanasiasa nchini kutovuruga amani kwani machafuko yakitokea watashindwa kufanya ibada mbalimbali ikiwemo kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Sheikh Akilimali alisema kwa sasa wananchi wako huru kwenda kufanya ibada misikiti na makanisani kutokana na uwepo wa amani, hivyo aliwasisitiza wanasiasa kutothubutu kuichezea amani.

“Tafadhalini wanasiasa msituharibie amani ya nchi yetu. Amani haichezewi tunaona kwa wenzetu wanavyohangaika, wanaishi kwa tabu sisi hatujazoea kukimbia. Sisi Watanzania ni moja na tunaishi kwenye nyumba moja hivyo hatuna budi kushirikiana kuilinda amani yetu,” alisema.

Kwa upande Katibu wa Wazee mkoani Rukwa, Kanali Mstaafu, John Mzurikwao alimuomba kiongozi huyo kuwasaidia kutatua kero mbalimbali zinazoukabili mkoa huo zikiwemo za malipo ya pembejeo kwa mawakala wa kilimo pamoja na mgogoro wa ardhi katika shamba ya Efatha.

Waziri Mkuu alisema suala la malipo kwa mawakala wa pembejeo za kilimo linafanyiwa kazi na watalipwa baada ya Serikali kukamisha zoezi la uhakiki wa madeni hayo ili kujiridhisha kama kweli wakulima wapatiwa pembejeo na kwa kiwango gani.

UDOM kuongeza wataalam wa shahada ya mafuta na gesi

Chuo Kikuu cha UDOM kimeandaa mtaala wa elimu kwa ajili ya shahada ya uzalimili katika sekta ya mafuta na gesi ili kutoa watalaam wengi zaidi wa masuala ya athari za kimazingira zinazoweza kusababishwa na uchimbaji wa rasimali hiyo.

Kaimu Makamu mkuu wa chuo hicho Dkt. Peter Msofe amesema hayo mjini Dodoma katika uifunguzi wa mkutano wa wadau wa elimu kutoka nchi za Uganda na Tanzania wanaoandaa mtaala wa unaolenga kuzinufaisha nchi mbalimbali za Afrika.

Dkt. Msofe amesema kuwa mtaala huo umekuja wakati muafaka wakati Tanzania imegundua gesi nyingi hivyo kuna uhitaji wa watalaam ambao wataweza kujua faida na athari za rasimali hiyo kimazingira na kiafya nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitivo cha Sayansi Asilia na Hisabati Said Ali Vuai, amesema kuwa mtaala huo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa masomo 2017/2018.

Airlander 10: Ndege ndefu zaidi duniani yapata ajali

 Ndege ndefu zaidi duniani - Airlander 10 - imeharibika baada ya kuanguka ikitua kwenye safari yake ya pili ya kufanyiwa majaribio.

Ndege hiyo ya urefu wa 302ft (92m) - ambayo kwa kiasi fulani ni ndege na pia kwa kiasi fulani puto - iliharibika ikiwa katika uwanja wa Cardington, Bedfordshire nchini Uingereza.

Ndege hiyo ya thamani ya £25m imeharibika eneo wanamoketi marubani baada ya kuangika kwa 'pua' mwendo wa saa tano saa za Uingereza.

Ndege ndefu zaidi hatimaye yapaa Uingereza

Msemaji wa HAV, kampuni iliyounda ndege hiyo, amesema marubani na wahudumu wengine wote wako salama.

Kampuni hiyo imekanusha madai kwamba waya uliokuwa umening'inia kutoka kwenye ndege hiyo ulikwama kwenye kigingi cha nyaya za simu na kusababisha ajali hiyo.
Ndege hiyo ilifanya safari yake ya kwanza 17 Agosti.

 Kampuni ya HAV inapanga kuunda ndege 10 aina ya Airlander kufikia mwaka 2021.

 Airlander 10 kwa takwimu
44,100 lbs (20,000kg): Uzani wa ndege hiyo

20,000ft (6,100m): Umbali ambao inaweza kupaa juu angani

80 knots (148km/h): Kasi yake ya juu zaidi

Siku 5: Muda ambao inaweza kukaa angani

22,050 lbs (10,000kg): Uzani ambao inaweza kubeba



 

Gallery

Popular Posts

About Us