Umeme warudishia watu zaidi ya bil. 69/- | KINGAZI BLOG

KARIBU UHABARIKE KIGANJANI MWAKO.

Breaking News
Loading...

Sunday, April 03, 2016

Umeme warudishia watu zaidi ya bil. 69/-


KUSHUKA kwa bei ya umeme kwa wateja wa kada mbalimbali wa nishati hiyo na kuondolewa kwa tozo ya huduma ya kila mwezi ya Sh 5,520 kwa kila mteja wa nyumbani, kumerudisha kwa Watanzania zaidi ya Sh bilioni 69, iliyokuwa ikienda katika Shirika la Umeme (Tanesco). Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Felix Ngamlagosi, amesema hayo mwishoni mwa wiki, alipokutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC). Kwa mujibu wa Ngamlagosi, kufutwa tu kwa tozo ya kila mwezi ya huduma kwa wateja wa majumbani ambayo ilikuwa Sh 5,520, ambayo ni mbali na punguzo la bei kwa kada mbalimbali za wateja, kumewarejeshea Watanzania Sh bilioni 69, ambazo hapo awali zilikuwa zikienda Tanesco.
Alipoulizwa iwapo hatua hiyo ya kupunguza bei ya umeme imetokana na shinikizo kutoka serikalini na kama kutayumbisha shirika hilo muhimu kwa uchumi wa nchi. Ngamlagosi alisema, kwanza maombi ya kushusha bei hiyo yametoka Tanesco.
“Sisi tumepokea barua kutoka Tanesco ikituomba suala la kushusha bei ya umeme na sio kwamba walilazimishwa na Serikali na sisi tuliwahoji sana, kama wataweza kujiendesha, baada ya kuridhika na maelezo yao na uchunguzi wetu, ndipo tukakubali,” alisema Ngamlagosi.
Faida ya gesi Akifafanua matokeo ya uchunguzi uliochangia wakubali kushushwa kwa bei hiyo, Ngamlagosi alisema walibaini ukweli kwamba hivi sasa mitambo ya kuzalisha umeme huo unaouzwa na Tanesco, mingi haitumii tena mafuta, bali inatumia gesi asilia inayochimbwa hapa nchini
Umeme wa mafuta ulikuwa ghali kwa kuwa kwanza yananunuliwa kwa fedha za kigeni na hivyo kuporomoka kwa Shilingi, kuliongeza gharama za ununuzi na pia bei yake kimataifa, ina tabia ya kubadilikabadilika, tofauti na gesi inayochimbwa nchini.
Capacity Charge Ngamlagosi alisema mbali na faida ya kutumia umeme unaotokana na gesi, ambao kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), karibu asilimia 70 ya umeme wote kwa sasa ni wa gesi, pia walibaini mitambo yote ya kufua umeme wa dharura imeondolewa.
“Ni kweli Tanesco hivi sasa wanatumia kiasi kidogo cha mafuta na mitambo yote ya dharura haitumiki tena, pia vyanzo vya nishati vimeongezeka na vingi ni vya uhakika na hakuna kampuni ya dharura ya muda mfupi inayolipwa tozo ya uwezo wa mtambo (capacity charge),” alisema Ngamlagosi.
Tozo hiyo ya uwezo wa mtambo, ambayo ilikuwa ikitozwa katika mitambo mingi ya ufuaji umeme wa dharura, iliongeza gharama kwa kuwa hata kama mtambo hauzalishi au umezimwa kabisa, tozo hiyo ilikuwa ikilipwa kwa siku kwa mabilioni ya Shilingi.
Kutokana na faida hizo, ikiwemo kujaa kwa mabwawa ya kufua umeme wa maji, Ngamlagosi alisema punguzo hilo si hasara kwa sababu unafuu wa uzalishaji nishati hiyo nao umeongezeka.
Wafanyabiashara Wakizungumza na gazeti hili jana, wananchi wa kada mbalimbali nchini wakiwemo wasomi na wanasiasa, wamepongeza Serikali kwa kushusha bei ya umeme na kueleza ni mwanzo mzuri wa wananchi kuanza kufaidi kukua kwa uchumi, huku wakitaka wenye viwanda na wafanyabiashara waangalie namna ya kushusha bei za bidhaa na huduma.
Walisema kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakipata maumivu kutokana na umeme kuwa ghali, jambo lililofanya wengi kutomudu gharama zake wakiwemo wa mijini na vijijini.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alipongeza Tanesco, Ewura na Serikali kwa punguzo hilo kwani Watanzania wanaanza kufaidi uzalishaji wa umeme kwa gesi asilia inayopatikana nchini na siyo mafuta yaliyokuwa ya gharama kubwa.
Alisema nia ni kumpunguzia mlaji gharama za maisha, kama ilivyo lengo la Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa gharama nafuu. “Kutokana na kupungua gharama hii ya umeme hakika na wazalishaji viwandani watakuwa wamepunguziwa gharama, hivyo ni wakati wa kufikiria kupunguza gharama za bidhaa zao ili kuendelea kumpatia mwananchi wa kawaida unafuu wa maisha,”alisisitiza.
Dk Banna alisema ni dhahiri kuwa uchumi wa nchi ulikuwa ukikua katika vitabu tu huku wananchi wakishindwa kuona manufaa yake lakini sasa wananchi wameanza kufaidi ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuwa na umeme wa uhakika na nafuu. Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alisema suala la kupungua bei ya umeme ni zuri na linadhihirisha kuwa nchi imepata Rais anayejali wananchi wake.
Alisema mara nyingi katika suala hilo, watu waliishi gizani huku kukiwa na mikataba mingi ya bandia, lakini hakukuwa na mtu aliyejali ila sasa wananchi wameanza kuona haki ya kutumia rasilimali zake na kunufaika nazo.
Alisema wananchi wengi wa vipato vya kati mara nyingi walilazimika kulala giza hususan mijini kwani ilikuwa ukinunua umeme wa Sh 10,000 unapata wa Sh 2,000 lakini sasa wananchi watafurahi na kuacha kuishi gizani kutokana na gharama hizo nafuu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo alisema kushuka kwa bei ya umeme ni jambo zuri kwa maendeleo ya nchi, kwani nafuu ya nishati inasaidia katika kupunguza gharama za maisha. Alisema nafuu hiyo itasaidia wananchi wa vijijini nao kumudu gaharama kwani bei kubwa iliyokuwepo, ilifanya wananchi wa vijijini kushindwa kumudu gharama hizo.
Ahadi ya Muhongo Itakumbukwa mara tu baada ya kuapishwa Desemba mwaka jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alitoa ahadi kuwa kazi yake ya kwanza itakuwa kuhakikisha nchi inapata umeme usiokatika mara kwa mara na kushusha bei yake.
Waziri huyo aliagiza Tanesco, Ewura na TPDC, kumpelekea mapendekezo ya kushuka kwa bei ya umeme akihoji kama gharama za shirika hilo zilitokana na kutumia mitambo ya mafuta, kwa sasa hata hayo mafuta yenyewe yameshuka bei katika soko la dunia.
Profesa Muhongo alisema hata kama Shilingi ilikuwa ikipoteza thamani dhidi ya Dola ya Marekani, lakini pipa la mafuta katika soko la dunia lililokuwa Dola za Marekani 200, lilishuka hadi dola 100 na Januari mwaka huu, lilikuwa kama dola 35 kwa pipa moja, hivyo Tanesco nayo walipaswa wajue gharama za uzalishaji umeme wa mafuta zimepungua.
Alisema moja ya ahadi za Rais John Magufuli ni kufufua viwanda, lakini haiwezekani kuwa na viwanda vingi, kama gharama za umeme zitakuwa juu kwa kuwa vitashindwa kujiendesha.
Profesa Muhongo alitumia nafasi hiyo kutoa tahadhari kwa yeyote atakayeona hataweza kutimiza majukumu yake ipasavyo, ajue kuwa ataondolewa katika nafasi yake, kwani suala la umeme ni la kufa au kupona. Imeandikwa na Ikunda Erick na Theopista Nsanzugwanko.

google+

linkedin

About Author
  • BLOG NAMBA MMOJA KWA MATANGAZO YA AJIRA NA NAFASI ZA KAZI TANZANIA. Soma zaidi

     

    Gallery

    Popular Posts

    About Us