Magufuli atoa neno Chato. | KINGAZI BLOG

KARIBU UHABARIKE KIGANJANI MWAKO.

Breaking News
Loading...

Monday, April 04, 2016

Magufuli atoa neno Chato.

RAIS John Magufuli amesali Ibada ya Jumapili kijijini kwao wilayani Chato kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais, na kusisitiza Watanzania wote kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani na kuwataka kupendana, kushirikiana na kutobaguana.


Dk Magufuli ambaye yuko mapumzikoni nyumbani kwake Lubambangwe katika kijijini cha Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita, aliungana na waumini wenzake wa Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato, kusali ibada ya Jumapili ya Pili ya Pasaka. Pamoja na mambo mengine, aliwausia Watanzania wote kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani.

“Niwaombe Watanzania wote tuendelee kushirikiana na kushikamana, kwa umoja wetu na siku zote tumtangulize Mungu mbele. Wakati tunaadhimisha wiki moja baada ya kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, Yesu Kristo alikufa kwa sababu ya dhambi zetu, sisi wote tujitahidi kufuata matendo ya Yesu Kristo ya kusameheana, kupendana, kushirikiana na tusibaguane,” alibainisha Rais Magufuli.

Pamoja na Rais Magufuli na mkewe Mama Janeth, ibada hiyo ilihudhuriwa na Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga na mkewe Mama Ida Odinga, ambao ni familia rafiki ya Rais Magufuli waliowasili Chato juzi jioni kwa mapumziko wakitokea Nairobi, Kenya.

Katika salamu zake kwa waumini wa Parokia ya Chato, Odinga aliwashukuru Watanzania kwa uhusiano mzuri walionao na Wakenya, huku akitoa mfano wa jinsi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyojitoa kupigania uhuru wa mataifa mengi ya Afrika ikiwemo Kenya.
Odinga alitoa mfano wake mwenyewe kuwa Mwalimu Nyerere alimpatia pasi ya kusafiria ya Tanzania aliyoitumia kwa miaka mitatu akienda kusoma nje ya nchi baada ya utawala wa Kikoloni wa Kenya kukataa kumpa pasi hiyo.

Kuhusu urafiki wake na Rais Magufuli, Odinga alisema, “urafiki huo ulianza tangu Rais Magufuli alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na yeye kuwa Waziri mwenye dhamana ya ujenzi wa Kenya, ambapo mara kadhaa walibadilishana uzoefu na kushirikiana katika mipango ya miradi ya ujenzi wa barabara, na kwa umuhimu huo ametoa mwito kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendeleza ushirikiano na mshikamano uliojengwa na waasisi wake wakiongozwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.”

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amlitoa mchango wa Sh milioni 10 kwa Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato mkoani Geita kwa ajili ya kuchangia upanuzi wa kanisa hilo. Fedha hizo zilikabidhiwa na Kaimu Mnikulu Ngusa Samike katika misa ya pili ya ibada ya Jumapili ya Pili ya Pasaka iliyofanyika kanisani hapo jana.

Kabla ya misa hiyo ya pili, Rais Magufuli na mkewe Mama Janeth wakiwa pamoja na Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga na mkewe Mama Ida, walisali misa ya kwanza, na Rais Magufuli aliahidi kuchangia Sh milioni 10 kwa ajili ya upanuzi wa kanisa hilo ambao unaendelea.
Katika misa hiyo, Paroko wa Parokia ya Chato, Padri Henry Mulinganisa alieleza kuwa kanisa hilo linatarajia kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake baadaye mwaka huu, na kwamba maadhimisho hayo yanakwenda sambamba na upanuzi wa kanisa ambao unachangiwa na waumini wenyewe.

Padri Mulinganisa alimshukuru Rais Magufuli kwa mchango huo, na amemuahidi kuwa utatumika vizuri ili uendeleze upanuzi wa kanisa hilo pamoja na michango ya waumini wengine.

google+

linkedin

About Author
  • BLOG NAMBA MMOJA KWA MATANGAZO YA AJIRA NA NAFASI ZA KAZI TANZANIA. Soma zaidi

     

    Gallery

    Popular Posts

    About Us