Sumaye,Lowassa,na Gwajima wachambuliwa Dodoma | KINGAZI BLOG

KARIBU UHABARIKE KIGANJANI MWAKO.

Breaking News
Loading...

Sunday, July 24, 2016

Sumaye,Lowassa,na Gwajima wachambuliwa Dodoma


VIGOGO mashuhuri wa Chadema waliowahi kuwa mawaziri wakuu; Edward Lowassa na Frederick Sumaye, jana waligeuka gumzo ndani ya Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kumchagua Rais John Magufuli, kuwa Mwenyekiti wa tano wa chama hicho.

Gumzo hilo, lilianzishwa na Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba, alimpomtaka Askofu wa Kanisa la Ufufuko na Uzima, Josephat Gwajima, asimpotoshe Magufuli ili yasije yakampata ya Sumaye, ambaye sasa anachezea mchangani Kibaha.

Sumaye mchangani

“Hata akina Sumaye hawakuunda vyama vyao. Bado wanahangaika; na sasa Sumaye anacheza mchangani Kibaha,” alisema Makamba.

Sumaye ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu na NEC ya CCM, kwa sasa anawania uongozi wa Kanda ya Pwani katika Chadema. Kabla ya kusema kuwa Sumaye anahangaika na siasa za mchangani, Makamba alimtaka Gwajima kuacha uongo na kusingizia viongozi wa CCM.

“Wewe siyo wa kwanza kukataa kazi hii. Hata watangulizi wako Kikwete na Benjamin Mkapa nao walifanya hivyo hivyo,“ alisema Makamba ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Makamba alisema hata manabii na mitume wengi, kama Haruni, Mussa, Yona au Yunus na Yeremia walifanya vivyo hivyo, walipopewa utume au unabii na Mungu, kwani waliogopa kufanya kazi hizo lakini, alisema mara zote Mungu aliwaagiza kuwa wasiogope kuwa manabii na mitume, kwani atatia maneno kwenye vinywa vyao.

Aidha, Makamba alitaka viongozi wa dini mfano Askofu Gwajima, waache kumfitini Kikwete eti kwamba alikuwa hataki kumpa uenyekiti Magufuli.

“Mzigo wa chama ulikuwa umebebwa na Mkwere Kikwete ambaye sasa anaondoka; na kwa kuwa kuna msemo kuwa ‘mzigo mzito mpe Mnyamwezi au Msukuma, nawaomba wajumbe wote sasa mzigo wa chama tumpe Msukuma Magufuli,” alisema na kauli yake hiyo ilishangiliwa na wajumbe.

Lowassa na ufisadi

Akielezea aina ya kiongozi anayetoka CCM na anayeingia, Makamba alisema kuwa anayetoka, Kikwete ni mpiganaji wa ufisadi, kwa kuwa alifikia hatua ya kumtosa rafiki yake Edward Lowassa, kuwa hafai kuwa Rais kwa kuwa anatuhumiwa kwa ufisadi.

Alisema kada wa chama hicho anayeingia baada ya Kikwete, Dk Magufuli yeye ndiye muasisi wa Mahakama ya Mafisadi, ambayo tayari imeshaanzishwa kwa Sheria ya Bunge. Kwa mujibu wa Makamba, Kikwete ni kiongozi aliyepiga vita umasikini na anapoondoka, anayeingia Dk Magufuli msimamo wake ni asiyefanya kazi na asile.

Kumchinja Kobe

Naye mmoja wa vigogo wa Chadema aliyerejea CCM, Fred Mpendazoe, alikuja na dhana ya namna ya kumchinja kobe, akifananisha na utaratibu uliotumika, kukata jina la Lowassa katika majina 38 ya wagombea urais.

Mpendazoe alisema Kikwete alifanya ‘timing’ sana kushughulikia ufisadi ndani ya chama hicho, kwa kuwa kati ya makada hao 38 waliokuwa wakiwania urais, baadhi akiwemo Lowassa walikuwa na tuhuma za ufisadi na kukatwa kwa majina yao, kulifanyika kwa wakati sahihi.

Gia angani

Mpendazoe alisema anashangaa kusikia Magufuli anabana demokrasia na kuhoji kati ya chama kilichotangaza nafasi ya urais na kuruhusu wagombea 38 kugombea, huku mchujo ukifanyika hadharani na kilichompata mgombea kwenye chopa (helikopta), ni kipi chenye demokrasia?

Akifafanua zaidi, Mpendazoe alisema Chadema ilimpata mgombea wake angani ndani ya helikopta, na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe alipokwenda katika vikao, akasema chama hicho kimebadilisha gia angani.

CCM B

Naye Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alihoji yeye kuitwa CCM B, baada ya Rais Magufuli kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole na kusema inakuwaje yeye aliyetoka katika chama hicho mwaka 1995, apewe jina hilo.

Alisema kama kupewa cheo na Magufuli, ndio sababu ya kuitwa CCM B, basi hata Mbunge wa Vunjo, James Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, ni CCM B kwa kuwa aliteuliwa kuwa Mbunge na Rais Jakaya Kikwete.

Mrema alisema kama kuitwa kwake CCM B ni kutokana na kutoka ndani ya CCM; basi Lowassa na Sumaye ni CCM A, kwa kuwa wao wametoka mwaka jana wakati yeye ametoka tangu 1995.

Haeleweki

Naye Magufuli alisema alimshangaa Rais mstaafu Benjamini Mkapa, kwa kumteua mtu mmoja kuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 mfululizo, wakati waliofanyakazi na Waziri Mkuu huyo, akiwamo yeye waliona kuwa ni mtu asiyeeleweka. Waziri Mkuu wa Mkapa, alikuwa Frederick Sumaye.

credit-habari leo

google+

linkedin

About Author
  • BLOG NAMBA MMOJA KWA MATANGAZO YA AJIRA NA NAFASI ZA KAZI TANZANIA. Soma zaidi

     

    Gallery

    Popular Posts

    About Us