Ripoti ya CAG yaanika majipu lukuki. | KINGAZI BLOG

KARIBU UHABARIKE KIGANJANI MWAKO.

Breaking News
Loading...

Tuesday, April 26, 2016

Ripoti ya CAG yaanika majipu lukuki.


MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ametoa ripoti ya ukaguzi wa hesabu ya mwaka 2014/15 iliyoibua kasoro nyingi kwenye taasisi na mashirika mbalimbali ya serikali huku halmashauri zikibainika kuwa na ‘madudu’ mengi.

Ripoti hiyo inaonesha kati ya halmashauri 164 zilizokaguliwa, 47 pekee ndizo zimepata hati safi, nyingine zilizobakia zina hati zenye mashaka, zisizoridhisha na chafu. Kwa upande wa mashirika ambayo ripoti hiyo imeyagusa, Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) limebainika mauzo ya hisa zake yalikuwa batili, hivyo CAG ameshauri lirudi chini ya usimamizi wa serikali hadi hapo mgogoro wa mgawanyo wa hisa utakapotatuliwa.

Kuhusu Wakala wa Usafiri wa Mwendo wa Haraka Dar es Salaam (DART), ripoti ya CAG imebaini kuwa kwa mwaka wa fedha 2014/15 wakala huyo aliingia mkataba na UDA-RT wa kutoa huduma ya usafiri wa mpito wa kuendesha mabasi 76 kulingana na vigezo vilivyoainishwa kwenye mkataba.

Lakini, Sheria ya Manunuzi ya Umma, mkataba huo ulitoa ongezeko la ununuzi wa mabasi na kufikia 84 ili kulingana na matakwa ya DART. Hata hivyo kwenye ukaguzi wa hesabu zao, CAG alibaini kuwepo na ununuzi wa mabasi 140 ambayo ni sawa na ongezeko la mabasi 56 yasiyo ndani ya mkataba.

Na kwamba pamoja na makosa hayo, pia ilibainika kuwa mabasi hayo yalikuwa na nembo ya UDART badala ya DART, kinyume na vigezo vilivyoainishwa kwenye mkataba na kuiagiza DART kuendesha UDA-RT kwa kuzingatia taratibu zilizoainishwa kwenye mkataba.
Aidha, ripoti hiyo imepigilia msumari kwenye suala la watumishi hewa na kusema tatizo hilo limekuwa sugu na serikali za mitaa zinaongoza kwa kulipa mishahara watumishi waliofariki na waliotoroka huku Sh bilioni 2.7 zikiwa zimetumika mwaka wa fedha 2014/15 kwa malipo hayo.

Jambo lingine ambalo limejitokeza kwenye ripoti ya CAG, ni utoaji wa misamaha ya kodi kwa kiwango cha juu huku ikionesha Sh trilioni 1.6 sawa na asilimia mbili ya pato la ndani la taifa, zilisamehewa katika kipindi kilichoishia Juni 30, 2015.
Madudu halmashauri
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa baada ya ripoti kuwasilishwa bungeni, CAG Mussa Assad alisema wamebaini kasoro nyingi katika taasisi mbalimbali za serikali, huku udhaifu mkubwa ukiwa kwenye serikali za mitaa.
Alisema kwa mwaka unaoishia Juni 30 ,2015, jumla ya hati za ukaguzi 465 zilitolewa kwa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na mashirika ya umma. Ripoti imeonesha kuwa mashirika ya umma na Serikali Kuu yamefanya vizuri kwa kupata hati nyingi safi, huku zile za mashaka zikiwa chache.

Aidha hakuna hati mbaya wala isiyoridhisha. Akifafanua alisema katika ukaguzi huo, halmashauri ndizo zinaongoza kwa kufanya vibaya . Kati ya halmashauri 164 zilizokaguliwa, 47 pekee ndizo zimepata hati safi, nyingine zilizobakia ni zenye mashaka, zisizoridhisha na chafu.

“Mashirika ya umma na Serikali Kuu yamefanya vizuri hakuna wenye hati isiyoridhisha au hati chafu, ila halmashauri bado kuna udhaifu mkubwa kutokana na kutokuwepo na mifumo madhubuti ya kutekeleza mapendekezo ya ukaguzi tunayoyatoa,” alisema Profesa Asaad.

Ripoti hiyo imeweka hadharani udhaifu wa Serikali za Mitaa katika kutekeleza mapendekezo ya CAG kutokana na kubainika kuwa asilimia 63 ya maagizo ya mkaguzi huyo kwa halmashauri nchini hayajatekelezwa.
Misamaha ya kodi
Wakati huo huo, akizungumzia misamaha ya kodi kwa kipindi kilichoishia Juni 30, 2015, Profesa Assad alisema ripoti yao inaonesha kuwa kiasi cha misamaha kilichotolewa ni Sh trilioni 1.6 sawa na asilimia mbili ya pato la ndani la taifa.

Kiwango hicho kwa mujibu wa Profesa Asaad, ni cha juu ikilinganishwa na lengo la serikali la kupunguza misamaha hiyo isizidi asilimia moja ya pato la taifa. Ripoti hiyo pia inabainisha uwepo wa bidhaa zilizohifadhiwa katika maghala kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi ambazo zilipewa misamaha ya kodi ya Sh bilioni 9.1 lakini hakuna ushahidi ulioonesha mauzo hayo kama kweli yalifanywa nje.

Katika misamaha hiyo, pia kuna utata kwenye mafuta yenye dhamana ya kodi ya Sh bilioni tano ambayo yalionekana kwenye mfumo wa forodha wa (TANCIS) kuwa yamesafirishwa nje kupitia nchini lakini hakuna ushahidi wa hilo.

“Sasa ukiangalia hayo na mengine utaona udhaifu mkubwa , tumeshauri serikali iweke mkazo usimamizi wa misamaha ya kodi na itolewe tu kwa mambo yanayostahili na uwepo ufuatiliaji kujua mrejesho wake, ili serikali ikusanye kodi na kujiimarisha kiuchumi”, alisema Profesa Asaad.

Deni la Taifa
Akizungumzia deni la taifa, Profesa Asaad alisema hadi kufikia Juni 30, mwaka 2015, deni la taifa lilikuwa Sh trilioni 33.54. Deni la ndani lilikuwa Sh trilioni 7.99 na deni la nje likiwa Sh trilioni 25.5 hivyo jumla ya deni lote likiongezeka kwa asilimia 27 ikilinganishwa na deni lililoishia Juni 30, mwaka 2014.

CAG ameshauri serikali kuongeza jitihada za ndani za kuhamasisha ukusanyaji wa mapato kujenga wigo mpana wa kulipa madeni na kuwa na mpango wa kupunguza gharama za kuongeza mikopo yenye masharti nafuu.

google+

linkedin

About Author
  • BLOG NAMBA MMOJA KWA MATANGAZO YA AJIRA NA NAFASI ZA KAZI TANZANIA. Soma zaidi

     

    Gallery

    Popular Posts

    About Us