Mzindakaya ataka timu kubuni miradi | KINGAZI BLOG

KARIBU UHABARIKE KIGANJANI MWAKO.

Breaking News
Loading...

Monday, March 21, 2016

Mzindakaya ataka timu kubuni miradi



MWANASIASA mkongwe nchini, Dk Chrisant Mzindakaya, ameushauri uongozi wa mkoa wa Rukwa kuunda timu ya wataalamu kupendekeza miradi ya maendeleo inayofaa kutekelezwa mkoani humo.
Alipendekeza timu hiyo ijumuishe wataalamu kutoka katika taasisi za fedha nchini na wizarani ambao watatafsiri wasifu wa mkoa huo na kuandaa kitabu kitakachoeleza mikakati ya maendeleo ya mkoa.
“Mikakati hiyo ni pamoja ya namna ya kuanzisha au kuendeleza viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vitakavyoongeza thamani ya mazao kwa kuyasindika,” alisema. Alisema kuwa inasikitisha kuona Mkoa wa Rukwa ulio miongoni mwa mikoa inayolima mahindi kwa wingi unaagiza mbegu bora kutoka nje ya nchi au kuletewa za bandia na kusambazwa kwa wananchi.
Alilieleza gazeti hili kuwa, maendeleo ya mkoa huu hayatakuja kwa kutegemea watu wengine walioko nje ya mkoa. Aidha, alishauri wafanyabiashara wa kati na wakubwa mkoani humo wakutane kutambuana ili watoke kwenda kutafuta wawekezaji katika miradi mbalimbali mkoani Rukwa.
Alisisitiza kuwa mageuzi ya maendeleo lazima yafanywe na wazawa wenyewe badala ya kukaa kusubiri watu kutoka nje ya mkoa. “Mkoa umeshafanya makongamano mawili (Julai , 2007 na Novemba 2013) na mahudhurio yalikuwa ya kuridhisha, lakini matokeo yake sio mazuri kwa kuwa hakuna mwekezaji kutoka nje aliyeonesha nia wala kuja kuwekeza mkoani kwetu,” alisema Mzindakaya.
Alisema, jibu la kweli na rahisi ni wawekezaji kuja kutoka mikoa mingine, lakini ni vigumu kama hakuna msukumo wa vipaumbele na fursa za uwekezaji zilizo wazi hasa kwa mkoa huo ambao kijiografia uko pembezoni.
Mzindakaya alisema mkoa huo una zaidi ya viwanda 30 vidogo vya kusindika alizeti katika hatua ya kwanza, hivyo kusababisha wananchi kuendelea kutumia mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.
Alikumbusha kuwa mwaka 1974 mkoa wa Rukwa katika viwango vya mapato na maendeleo ulikuwa wa 18 kati ya mikoa 20 iliyokuwepo nchini, baada ya miaka minne hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliutangaza kuwa miongoni mwa mikoa minne inayozalisha mahindi kwa wingi nchini.
Alieleza kuwa hayo yaliwezekana baada ya viongozi wa Serikali na wabunge kuwashirikisha wananchi kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo ambayo mkoa unajivunia hadi sasa.

google+

linkedin

About Author
  • BLOG NAMBA MMOJA KWA MATANGAZO YA AJIRA NA NAFASI ZA KAZI TANZANIA. Soma zaidi

     

    Gallery

    Popular Posts

    About Us