Ni historia leo kwa Zanzibar | KINGAZI BLOG

KARIBU UHABARIKE KIGANJANI MWAKO.

Breaking News
Loading...

Sunday, March 20, 2016

Ni historia leo kwa Zanzibar



UCHAGUZI wa marudio Zanzibar unafanyika leo, huku Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC),
Jecha Salum Jecha, akiwahakikishia Wazanzibari kufanya kila linalowezekana, ili kuuendesha uchaguzi kwa usalama na amani na kuhakikisha unakuwa huru na wa haki. Wagombea urais watakaoshiriki katika uchaguzi huo ni Dk Ali Mohamed Shein wa CCM, Seif Sharif Hamad wa CUF, Juma Ali Khatib wa TADEA, Khamis Iddi Lilla wa ACT Wazalendo, Hamad Rashid Mohamed kutoka ADC na Said Soud Said wa AFP.
Wengine ni Ali Khatib Ali wa CCK, Mohamed Masoud Rashid wa CHAUMMA, Abdalla Kombo Khamis wa DP, Kassim Bakari Ali wa JAHAZI ASILIA, Tabu Mussa Juma wa Demokrasia Makini, Seif Ali Iddi wa NRA, Issa Mohamed Zonga wa SAU na Hafidh Hassan Suleiman wa TLP.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 kutokana na kasoro zilizojitokeza kama zilivyotangazwa na Jecha, huku CUF ikitangaza kususa uchaguzi huo. Wakati uchaguzi huo unafutwa, CCM ilishashinda viti vya uwakilishi kwenye majimbo 27 na CUF pia ilishinda majimbo 27 na wawakilishi walioshinda walikabidhiwa hati ya ushindi, lakini kutokana na kasoro ambazo Tume ilibaini uchaguzi huo ukafutwa.
ZEC yatoa utaratibu Tamko la ZEC kuhusu uchaguzi wa leo linaeleza kuwa wananchi watamchagua Rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani. Jumla ya wapiga kura visiwani Zanzibar ni 503,193. Pia wananchi wa Jimbo la Kijitoupele katika orodha hiyo watamchagua mbunge baada ya uchaguzi wa Oktoba kutofanyika kutokana na kuchelewa kuwasili kwa vifaa vya kupigia kura katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Taarifa iliyotolewa jana na Jecha ilisema vituo vyote vya kupigia vitafunguliwa saa 1.00 asubuhi na kufungwa saa 10.00 jioni. Alisema Tume yake imekamilisha taratibu zote muhimu zitakazowezesha wapiga kura kupiga kura bila ya usumbufu. “Hivi ninavyozungumza, vifaa vyote muhimu vinavyohusika na kazi ya kupigisha kura tayari vimesambazwa katika vituo vyote vya kupigia kura Unguja na Pemba,” alisema Jecha.
Alisema uchaguzi wa leo umefuata sheria na aliwataka wananchi wote kuzingatia ipasavyo maelekezo ambayo yametolewa na yatakayotolewa na maofisa wa Tume, watakaokuwepo vituo vya kupigia kura. Alisema maelezo hayo yanalenga kudumisha utulivu wakati wote wa kupiga kura, kuhesabu na kujumlisha kura katika vituo. Alitoa mwito kwa wapiga kura, wagonjwa na ambao hawawezi kupiga kura wenyewe, waruhusiwe kwa mujibu wa sheria kwenda vituoni na watu wanaowaamini, ili kuwasaidia kupiga kura.
Alifafanua kuwa mtu ataruhusiwa kumsaidia mtu mwingine kupiga kura baada ya mpiga kura kumridhisha msimamizi wa kituo kuwa kweli hawezi kupiga kura na anahitaji msaada wa mtu mwingine. Mwenyekiti huyo wa ZEC ambaye amekuwa haonekani hadharani tangu atangaze kufuta matokeo ya uchaguzi wa Oktoba mwaka jana, alitahadharisha kuwa ni kosa kubwa kwa mwananchi kutaka kupiga kura kabla ya kituo kufunguliwa au baada ya kufungwa, au mtu anayetaka kupiga kura wakati hana haki ya kufanya hivyo.
Aliwahakikishia wananchi kuwa Tume inafanya kila linalowezekana ili kuuendesha uchaguzi wa leo kwa salama na amani na pia itahakikisha kuwa uchaguzi huo unakuwa huru na wa haki. Naye Ofisa Mdhamini wa ZEC, Pemba Ali Mohamed Dadi alipozungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Tume Chake Chake Pemba, amesema maandalizi yamekamilika kwa kazi za usambazaji wa vifaa.
Dadi alifafanua kwamba vituo 463 vitatumika kwa ajili ya wapigakura ambapo katika kituo cha Mkoani vipo vituo 117, Chake Chake vituo 122 wakati katika kituo cha Micheweni 91 na Wete vipo vituo 133. “Maandalizi ya uchaguzi wa marudio katika kituo cha Pemba yamekamilika na kwa upande wa Tume ya Uchaguzi Pemba tumeweka vituo 463 ambavyo vitatumika kwa wapiga kura kutekeleza demokrasia ya kuchaguwa viongozi wa vyama vya siasa,” alisema.
Waangalizi wa kimataifa Jecha alisema ukiondoa waangalizi wa ndani ambao tayari wametuma maombi yao ZEC pia utaangaliwa na waangalizi wa kimataifa kutoka Umoja wa Afrika (AU), waangalizi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Tume za Uchaguzi za Nchi za Kusini mwa Afrika (ECF-SADC), Commoro na ubalozi wa Zambia ambao tayari wamewasili visiwani hapa.
Kauli ya CUF na CCM Chama cha Wananchi (CUF) kimetangaza uchaguzi wa marudio unaofanyika leo ni haramu na hawawezi kushiriki wala kutambua matokeo ya uchaguzi huo. Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Ahmed Mazrui alisema hata kama aliyekuwa mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad atashinda kamwe hawawezi kutambua matokeo hayo kwa sababu wananchi wa Zanzibar tayari walishaamua kupitia sanduku la kura.
Mazrui alisema msimamo wa chama chake ni kuendelea kudai haki yao na kuendeleza msimamo wao wa kutokushiriki uchaguzi wa marejeo kwa kuwa wanaamini kuwa uchaguzi uliopita ulikamilika.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai amenukuliwa na vyombo vya habari akielezea kuwa chama hicho kitaenda kushiriki uchaguzi wa leo kikiwa na matumaini ya kushinda kutokana na maandalizi waliyofanya. Vuai alinukuliwa akisema pamoja na vyama vingine kujitoa kwenye uchaguzi huo, lakini anaamini kuwa vyama vilivyobaki vitatoa upinzani mkubwa kwa chama chake.

google+

linkedin

About Author
  • BLOG NAMBA MMOJA KWA MATANGAZO YA AJIRA NA NAFASI ZA KAZI TANZANIA. Soma zaidi

     

    Gallery

    Popular Posts

    About Us