Magufuli apongezwa sana kwa uteuzi wa Ma-RC | KINGAZI BLOG

KARIBU UHABARIKE KIGANJANI MWAKO.

Breaking News
Loading...

Tuesday, March 15, 2016

Magufuli apongezwa sana kwa uteuzi wa Ma-RC

 


UTEUZI wa wakuu wa mikoa uliofanywa na Rais John Magufuli juzi, umeonekana kuwaridhisha wengi kutokana na watu wa kada tofauti kupongeza wakisema umezingatia weledi, elimu, rika na historia ya uchapakazi ya wahusika.
Miongoni mwa waliozungumzia uteuzi huo wakisema unaendana na kasi ya utendaji wa Rais Magufuli, wamo wasomi, wanasiasa na watu wa kawaida. Lakini pia, baadhi ya wakuu wa mikoa ambao wameachwa kwenye uteuzi, hususani aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, wamekosoa wanaodhani uteuzi una kasoro wakisema kutokuwamo baadhi ya watu, hakumaanishi kuwa uteuzi una upungufu bali uko sahihi na unaendana na kasi ya Rais Magufuli.
Hata hivyo, upande wa wanaharakati wa masuala ya jinsia, wameonekana kutoridhishwa kwa kile kinachodaiwa ni kuwapo idadi ndogo ya wanawake. Kandoro: Uteuzi ni sahihi Wakati huo huo, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro amepongeza uteuzi na kusema hana kinyongo kwa kutopewa nafasi katika uteuzi huo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Kandoro alisema kutopewa nafasi kwenye uteuzi huo hakumaanishi kuwa uteuzi una upungufu bali uko sahihi na wenye kuendana na kasi ya Rais Magufuli. Hata hivyo, Kandoro ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa waliopita, alionesha kutoridhishwa na baadhi ya kauli za watu wanaozungumzia uteuzi huo akisema hauna tija katika utendaji wa kiserikali.
“Watu wasiwe na mtazamo hasi kwani nafasi yoyote ya kuteuliwa mwisho wake kuna ukomo hivyo tutambue kuwa anayeteua ipo siku anatengua uteuzi huo, nimepokea vizuri na ikumbukwe kuwa uteuzi ni uteuzi tu,” alisisitiza. Kandoro aliwapongeza wakuu wa mikoa wapya na zamani waliobaki, akisema hana kinyongo na kutokuwamo kwenye safu kwa kuwa muda alioitumikia serikali ni mwingi hivyo anastahili kupumzika na kuwaachia wengine.
“Nimeitumikia serikali hii kwa muda usiopungua miaka 40; Sasa waliotaka niendelee wanataka nitumikie hadi naingia kaburini? Hivyo kwa sasa inafaa mimi kupumzika ili niendelee na shughuli zingine,” alisema Kandoro. Kwa upande wa baadhi ya wananchi waliozungumzia uteuzi huo, walikuwa na maoni tofauti ambapo baadhi walimpongeza Rais kwa kuwateua waliokuwa watumishi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wakisema watasaidia kuimarisha ulinzi wa nchi.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, Dk Benson Bana, alisema uteuzi huo wa Dk Magufuli umezingatia vigezo vyote ambavyo Serikali ya awamu ya tano imejiwekea. “Wapo walioteuliwa ambao ni wazoefu wa muda mrefu na muda mfupi chanya kwa maana ya kwamba wote wamefanya vizuri katika utendaji wao,” alisema.
Alitoa mfano wa Paul Makonda, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kusema, amekuwa mbunifu na kuonesha uwezo katika kusimamia na kufuatilia masuala ya maendeleo ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake. Dk Bana alisema kupangwa kwa wanajeshi waliokuwa na vyeo vizito kwenye mikoa ya pembezoni mwa nchi kama vile Kagera, Kigoma, Geita na Katavi ni uamuzi mzuri.
“Maeneo ya pembezoni yamekuwa yakikabiliwa na matukio mengi ya uhalifu, ikiwemo ujambazi, kwa sifa za Ma RC hawa kazi yao itakuwa rahisi,” alisema. Kuhusu elimu, alisema kati ya wakuu hao wa mikoa hakuna kiongozi yeyote ambaye ni mbumbumbu. Alipongeza kile alichoeleza kuwa, rais amezingatia mchanganyiko maalumu wenye weledi.
“Lakini pia nachukua fursa hii kumpongeza Rais kwa kuwatambua mawaziri na wabunge ambao hawakuchaguliwa na wananchi kwa sababu za kisiasa lakini utendaji wao ni mzuri,” alisema na kumtolea mfano Aggrey Mwanri, aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora. Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACTMaendeleo), alipongeza uteuzi wa vijana katika safu hiyo ya wakuu wa mikoa huku akiwahimiza kuchapa kazi wasikiangushe kizazi cha vijana wa sasa.
Aliwapongeza Anthony Mataka (Mkuu wa Mkoa wa Simiyu), Halima Dendego (Mtwara), Jordan Rugimbana (Dodoma) na Amos Makalla wa Mbeya kwa uteuzi huo. “Ni dhahiri sasa wajibu wa uongozi sasa ni wetu, ni wa kizazi chetu, msituangushe, maana mkituangusha ninyi na kizazi kimeanguka. Mola awatangulie,” alisema Zitto. Walioteuliwa waahidi Kwa upande wake, Rugimbana aliyepangiwa Mkoa wa Dodoma, alimshukuru Rais Magufuli akisema amepokea uteuzi kwa mikono miwili.
“Mimi ni kamanda na kamanda hachagui vita popote anapigana, nawaahidi wakazi wa Dodoma na viongozi wenzangu wa mkoa huu ushirikiano katika kusimamia na kufuatilia maendeleo ya wananchi,” alisema. Naye Anne Kilango aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. Anna Kilango alimshukuru Dk Magufuli na chama chake kwa kumpatia fursa hiyo. Alisema amejipanga kusimamia na kufuatilia sekta madini, kilimo na ufugaji katika mkoa huo.
Aliahidi kuwa atahakikisha kuwa migogoro ya wakulima na wafugaji hainyemelei wakazi wa Shinyanga. Wanaharakati jinsia Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA), Edda Sanga, alipotakiwa na mwandishi kutoa maoni juu ya uteuzi huo, alisema mitandao inayojishughulisha na masuala ya wanawake, imepanga kutoa tamko lao rasmi kuhusu uteuzi huo.
Juzi Dk Magufuli alifanya uteuzi wa wakuu wa mikoa ambao umewatema wakuu wa mikoa 12 na kuwateua wapya 13. Miongoni mwa walioteuliwa, wamo mawaziri wanne wa zamani walioangushwa kwenye uchaguzi uliopita. Aidha, amewapandisha wakuu wa wilaya watano, akiwemo Makonda anayeongoza Mkoa wa Dar es Salaam.
Amewabakiza wakuu wa mikoa saba katika vituo vyao vya kazi; watano wamehamishwa vituo vya kazi na mmoja amepangiwa mkoa mpya wa Songwe. Kwenye safu hiyo ya wakuu wa mikoa wanaoapishwa leo Ikulu, Dar es Salaam, wamo wanajeshi wapya wanne.

google+

linkedin

About Author
  • BLOG NAMBA MMOJA KWA MATANGAZO YA AJIRA NA NAFASI ZA KAZI TANZANIA. Soma zaidi

     

    Gallery

    Popular Posts

    About Us