CHADEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Vincent
Mashinji amesema kuwa Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi
ndiyo msingi imara pekee unaoweza kuweka mifumo na taasisi kwa ajili ya
maendeleo ya kweli yatakayogusa maslahi ya Watanzania wote badala ya
nchi kuongozwa na kauli za viongozi.
Kutokana na umuhimu huo wa kuzingatia maoni ya wananchi yanayobeba
matakwa yao katika mchakato wa Katiba Mpya, amesema kuwa CHADEMA
hakitashiriki Kura ya Maoni ya Katiba Mpya Inayopendekezwa ambayo
ilipitishwa na Bunge Maalum la Katiba baada ya kubadili na kuondoa
mapendekezo yaliyotolewa na wananchi kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba
Mpya.
Badala yake, CHADEMA kitaendelea kuweka agenda ya kupigania Katiba Mpya
na bora katika vipaumbele vyake, kwa sababu itatibu vidonda na kumaliza
makovu yaliyoko katika jamii kutokana na matatizo mbalimbali kama vile
ukosefu wa haki, migogoro ya ardhi, wananchi kukosa huduma za msingi za
kijamii zikiwemo elimu, maji na afya.
Dkt. Mashinji ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipoukaribisha
ujumbe wa Chama cha Centre Party cha Norway uliofika ofisini kwake
jijini Dar es Salaam kutia saini makubaliano ya ushirikiano kati ya
vyama hivyo kwenye Mradi wa Elimu ya Demokrasia awamu ya pili
unaofanyika Wilaya ya Mtwara Vijijini.
Dkt. Mashinji pia amekishukuru chama hicho kwa kusaidia kutoa elimu ya
uraia kwa Watanzania hususani maeneo ya vijijini katika mradi ambao
unahusisha vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi ndani ya Bunge, huku
akisisitiza kuwa CHADEMA kiko tayari kwa ushirikiano unaozingatia
maslahi na matakwa ya wananchi hasa katika kukuza uelewa wa kudai haki,
demokrasia na uongozi bora ndani ya nchi.
“Suala la Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi kama
ilivyowasilishwa kwenye rasimu ya pili na Tume ya Mabadiliko ya Katiba
Mpya ni agenda muhimu kwa Watanzania wapenda nchi yao na sisi ni
kipaumbele kwa mwaka huu na kuendelea hadi hapo nchi yetu itakapopata
Katiba Mpya ya Wananchi.
“Jana na leo tumewasikia baadhi ya viongozi wa serikali wakisema kuwa
wanajiandaa kuitisha kura ya maoni…hatutashiriki kura ya maoni ya Katiba
Mpya Inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba. Tunajua Watanzania
wengi wanataka Katiba Mpya iliyotokana na maoni yao, si ile
iliyochakachuliwa bungeni.
“Katiba Mpya iliweka masuala kuhusu haki za wananchi, kuimarisha misingi
na kuweka mifumo ya demokrasia na uongozi bora, walau kwa kuanzia.
Hatuwezi kusema sasa tutatumia mikakati gani kuwahamasisha Watanzania
kuidai Katiba Mpya…tutajua namna ya kuvuka tukishafika mtoni,” amesema
Katibu Mkuu Dkt. Mashinji.
Aidha, Katibu Mkuu Dkt. Mashinji amesisitiza kuwa suala la nchi kuwa na
misingi na mifumo imara ya demokrasia na uongozi bora ni muhimu kwa
Tanzania, katika wakati ambapo nchi inaelekea kwenye uchumi mkubwa wa
nishati ya gesi na mafuta, akisema vinginevyo ni hatari iwapo taifa
lenye utajiri mkubwa wa rasilimali, litaendelea kuwa na wananchi
waliokata tamaa kutokana na mfumo mbovu uliopo.
Akisisitiza umuhimu wananchi kuwa Katiba inayotokana na wananchi, Dkt.
Mashinji alitolea mfano wa nchi ya Norway ambayo miaka mingi nyuma
ilikuwa sawa na Tanzania, lakini ilifanikiwa kuondokana kuwa taifa
maskini kutokana na uwepo wa uongozi bora, mifumo na taasisi imara za
kidemokrasia ambazo ziliweza kusimamia ustawi wa taifa hilo kutokana na
uchumi wa gesi na mafuta na sasa ni kati ya mataifa yaliyoendelea barani
Ulaya na duniani kwa ujumla.
Kwa upande wake ujumbe huo uliokuwa ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Centre
Party, Knut Olsen, umesema kuwa chama hicho kinashukuru kwa mradi huo
kuingia katika hatua ya pili kuanzia mwaka 2016-2019 huku hatua ya
kwanza ikiwa na mafanikio makubwa katika jamii ya wananchi wa maeneo ya
pembezoni.
“Kama unavyojua, mradi huu kupitia TCD unahusisha vyama vyote vyenye
uwakilishi ndani ya bunge, na lengo letu ni kuwajengea uwezo viongozi wa
vyama hasa wanawake na vijana katika ngazi ya jamii kwenye vitongoji,
vijiji, kata na bunge ili waweze kushiriki mchakato wa maamuzi.
Tunatarajia kuendelea kupata ushirikiano katika hatua ya pili,” amesema
Inger Bigum, ambaye ni Meneja wa Mradi hapa nchini.
Wengine waliokuwa katika ujumbe huo wa Centre Party ni pamoja ni Katibu
Mkuu wa Vijana Sara Hamre, Katibu Mkuu wa Wanawake, Eline Stokstad-Oslan
na Katibu Mkuu wa Wazee, Kristin Madsen.
Mradi huo wa Elimu ya Demokrasia katika Wilaya ya Mtwara Vijijini
unaohusisha vyama vyenye uwakilishi bungeni kupitia Kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD) chini ya ufadhili wa chama hicho, katika awamu ya kwanza
ulihusisha kata za Msangamkuu, Nanyamba, Ziwani na Mbembaleo na katika
sasa awamu ya pili utakuwa katika kata za Mkunwa, Tangazo, Mayanga na
Madimbwa.
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA