. Rais John Magufuli ametangaza kupambana na wafanyabiashara wasiozidi 10 waliohodhi biashara ya sukari, akisema ndiyo wameshiriki kuua viwanda na kujitajirisha.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa majengo ya NSSF na PPF jijini Arusha jana, Rais Magufuli alisema atapambana na wafanyabiashara hao bila kujali ni wafuasi wa CCM, Chadema ama CUF hadi mwisho wake.
“Wafanyabiashara hawa walinunua viwanda vya NMC wakafungua mashine na kwenda kuuza Msumbiji na wakisimama utawasikia CCM oyee,” alisema.
Aliongeza, “Utakuta Watanzania tunaendeshwa na wafanyabiashara kati ya watano au kumi tu, ukienda kwenye sukari ni haohao, walioua viwanda ni haohao, nawahakikishia nitalala nao mbele hadi mwisho,” alisema.
Alisema kwa sasa kila Serikali inapojitahidi kufanya mambo ya maendeleo kuna watu wanataka kukwamisha, lakini kamwe hawatashinda.
Alisema biashara ya sukari ni kama dawa ya kulevya, kuna kikundi cha watu ndiyo wanafanya biashara hii, wanakaa wanapanga leo tunatoa kiasi fulani leo hatutoi na wamekuwa wakienda Brazil kuchukua sukari iliyomaliza muda wake na kuileta nchini.
“Wanakwenda kuchukua sukari ambayo imekaribia kumaliza muda wanaileta wanawauzia Watanzania, ndiyo sababu nasema wafanyabiashara wa aina hii nitapambana nao, wawe CCM, wawe Chadema, kwangu mimi ni mkong’oto tu,” alisema.
Mbinu mbadala
Rais alisema kutokana na hali ya biashara ya sukari sasa, ndiyo sababu anashauri wakurugenzi wa mifuko ya hifadhi ya jamii, kufanya biashara ya sukari ambayo ni ya faida kubwa na faida ya haraka.
“Njooni muombe vibali na kwenda kununua sukari na tutawapa ili kuja kuuza kwa Watanzania wakiwamo wanachama wenu.
Alisema sukari inaweza kununuliwa nje kwa bei nzuri na inaweza kuja kuuzwa hapa nchini hadi kwa Sh800 kwa kilo, tena sukari ambayo ni bora.
Kilo 622,000 zakamatwa Moro
Shehena ya sukari tani 622.4 sawa na kilo 622,400 iliyokuwa imehifadhiwa kwenye maghala mkoani Morogoro imekamatwa, huku bei ya bidhaa hiyo katika maduka ya rejareja mkoani humo ikiwa imefikia Sh2,600 hadi 2,800 kwa kilo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen alimwagiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo kuhakiki iwapo sukari hiyo imelipiwa kodi.
Alimwagiza pia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei kuwakamata wahusika na kuwafikishwa mahakamani kwa kuwa kitendo hicho ni moja ya makosa ya uhujumu uchumi.
Dk Kebwe alimtaka Kamanda Matei kuweka ulinzi kwenye maghala ya wafanyabiashara yaliyokutwa na sukari hiyo.
Gulamali ruksa kuuza
Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Dodoma imemfungulia msambazaji wa sukari, Haidary Gulamali kuuza bidhaa hiyo iliyokuwa imekamatwa kwa bei elekezi bila kuweka masharti.
Sukari hiyo tani 154 ilikuwa imehifadhiwa katika ghala lililoko eneo la viwanda la Kizota mkoani hapa ilizuiliwa juzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jodarn Rugimbana alisema Serikali itaendelea na uchunguzi wa suala hilo na ikibainika ana kosa atachukuliwa hatua za kisheria.
Gulamali alisema hakuficha sukari bali amekuwa akiuza kama kawaida katika duka lake lililopo katikati ya mji.
Alisema amekuwa akiiuza kwa Sh2,300 kwa kilo kutokana na gharama za usafirishaji, kodi na ulipaji wa wafanyakazi baada ya kununua sukari hiyo Sh1,750 kwa kila kilo.
Alisemaanaunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kupambana na walanguzi wa sukari nchini, na kutaka nguvu hiyo ielekezwe kwa wauzaji wa rejareja ambao wamekuwa wakilangua bidhaa hiyo.
Wapinzani wamshukia Magufuli
Akizungumza bungeni jana, Waziri Kivuli wa Viwanda, Biashara na Uwezeshaji, Antony Komu alisema Rais John Magufuli alikurupuka kutoa maagizo ya kukataza uagizaji wa sukari nje bila kujua mahitaji halisi.
“Kama hakukurupuka basi alishauriwa vibaya na watu. Amefanya uamuzi bila kufanya utafiti wa mahitaji ya sukari nchini,” alisema.
Alisema ni vizuri kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuwa na umeme wa uhakika, bei nafuu na kupunguza kodi ili sukari izalishwe kwa wingi na kwa bei nafuu nchini.
Mbunge wa Ubungo, Said Kubenea (Chadema), alisema suala la kutaifisha sukari ya wafanyabiashara na kuigawa bure kunaweza kusababisha benki nchini kufilisika kwa sababu watashindwa kulipa mikopo yao.
Tani 26.5 kuchunguzwa
Kikosi maalumu kinachoshirikisha polisi na TRA, kimeundwa kuchunguza uhalali wa tani 26.5 za sukari zilizokamatwa katika operesheni iliyoendeshwa jijini Mwanza.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema kikosi hicho kitachunguza ilipokuwa ikipelekwa.
Vyombo vya dola vinaendelea na msako dhidi ya wafanyabiashara wanaodaiwa kuficha sukari huku bei ya bidhaa hiyo ikipanda kutoka bei elekezi ya Sh1, 800 hadi kati ya Sh2, 500 hadi Sh4,000 kwa baadhi ya maeneo.
TPC yazungumza
Kampuni ya TPC Limited inayomiliki kiwanda cha sukari cha TPC, ilisema mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Singida bado ina sukari ya kutosha kulisha soko.
Ofisa Mtendaji wa TPC, Jaffar Ally alisema kiwanda chake kitaanza uzalishaji Juni 14, lakini uchunguzi wao unaonyesha wauzaji wa rejareja bado wana akiba ya sukari.
Alisema kiwanda hicho kwa sasa hakina sukari baada ya kuiuza kwa wafanyabiashara kadhaa ambao ni Mohamed Enterprises, Marenga Investment, Setway Ltd, Modern Holding, Alpha Group na Nagji.
Alisema kiwanda hicho huzalisha kati ya tani 450 na 500 kwa siku na kwa mwaka huzalisha kati ya tani 100,000 na 105,000 ambayo hutosheleza mahitaji ya mikoa minne na ile ya jirani.
Imeandikwa na Mussa Juma (Arusha), Hamida Shariff (Morogoro), Ngollo John (Mwanza), Daniel Mjema na Sharon Sauwa (Dodoma).
Tuesday, May 10, 2016
Wanaoficha sukari hawazidi 10
Waziri Mkuu Kumwakilisha Rais Magufuli London.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa anatarajiwa kuondoka nchini leo jioni (Jumanne, Mei 10, 2016) kwenda London, Uingereza kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi unaojadili suala la kupambana na rushwa (Anti-Corruption Summit 2016) utakaofanyika Mei 12, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mchana, Waziri Mkuu amesema anaenda kumwakilisha Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli kwa sababu siku hiyo hiyo, atalazimika kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Museveni.
“Mheshimiwa Dk. Magufuli ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na siku hiyo hiyo, mmoja wa marais wa nchi wanachama anaapishwa. Kwa hiyo amelazimika kwenda kuhudhuria sherehe hizo,” alifafanua Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu mada ya mkutano huo, Waziri Mkuu amesema Tanzania inafanya vema katika mapambano dhidi ya rushwa na kwamba baadhi ya nchi zimeanza kuvutiwa na juhudi ambazo Serikali imekuwa ikichukua.
“Waziri Mkuu wa Uingereza ameandaa mkutano huu na alimwalika Mheshimiwa Rais Magufuli ili ahudhurie akiwa ni miongoni wa wakuu wa nchi 60 watakaohudhuria mkutano huo. Tanzania ni miongini mwa nchi mbili kutoka bara la Afrika ambazo zimealikwa kushiriki. Nchi nyingine ya kutoka Afrika ni Nigeria,” alisema.
Waziri Mkuu atafuatana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa na Kikanda, Balozi Dk. Augustine Mahiga, Mkurugenzi wa TAKUKURU, Bw. Valentino Mlowola, wataalamu wa sekta ya rushwa na wanasheria
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU-2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MEI 10, 2016.
Songas yazima mitambo kwa kuidai Tanesco Sh194 bilioni
Dar es Salaam. Kampuni ya kufua umeme kwa njia ya gesi asilia, Songas Limited imezima mitambo yake, baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kushindwa kulipa deni la Dola 90 milioni za Marekani sawa na Sh193.5 bilioni, jambo linalotishia ukosefu wa nishati hiyo muhimu nchini.
Hata hivyo, Tanesco imepinga uamuzi huo na kueleza kuwa ni vitisho kwa wananchi na inakiuka vifungu namba 4.4 , 4.6 na 17 vya mkataba ulioingiwa na Songas.
Mkurugenzi Mkuu wa Songas, Nigel Whittaker alisema jana kuwa wameamua kuchukua hatua ya kuzima mitambo hiyo baada ya kuzidiwa na gharama za uendeshaji kutokana na deni hilo.
“Mtambo huo uliopo Ubungo unazalisha Megawati 189, tumefikia hatua ya kuzima kidogo kidogo kuanzia Aprili 29 mwaka huu kutokana na deni hilo, Tanesco imekuwa ikisuasua katika kulipa,” alisema Whittaker.
Akisisitiza kuwa mradi huo wa Songas, ulioanzishwa tangu mwaka 2004 , ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania na umekuwa ukizalisha umeme kwa kutumia gesi asilia kutoka Songosongo na kuuingiza katika gridi ya taifa.
Whittaker alieleza kuwa kiasi cha umeme wanaozalisha ni takriban asilimia 20 ya nishati inayozalishwa nchini.
“Ilikuwa tuifunge mitambo hii tangu mwaka jana, lakini Serikali ilituomba tuendelee wakati ikisimamia hatua ya kulipwa, tunaendelea lakini hatimaye tumekwama kwa kuwa kuna mahitaji ya msingi ambayo yanategemea fedha ikiwamo matengenezo ya mitambo hiyo,”alisema.
Alisema pia wamejikuta katika hali ngumu kwa kudaiwa na taasisi kadhaa za Serikali ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), na Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC), hivyo wanaendelea kujadiliana na Tanesco na Serikali ili kuangalia jinsi ya kushughulikia jambo hilo kwa kutambua umuhimu wa mradi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba, alisema Songas wamevunja makubaliano ya mkataba hususan kifungu cha 4.4 ambacho kinaitaka Songas kutoa siku 90 ya kuwa na majadiliano.
Aliwatoa wananchi hofu kwa nchi haitaingia gizani kwa kuwa licha ya Songas kutangaza kuzima kabisa mitambo yote Mei 11, tayari walikwisha kuwa wameanza kuizima na haututokea mgawo. “Ingawa ni kweli wanatudai, lakini siwezi kusema kiasi gani nami nitakuwa nimekiuka huo mkataba, kwa hili walilofanya tutachukua hatua hatukubaliani nao,” alisema.
Songas ambao taarifa ya hivi karibuni ya Serikali inaonyesha kuwa wanauzia umeme Tanesco kwa senti za 2.4 za Marekani kwa uniti, wanalipwa capacity charge ya Dola za Marekani 5.2 milioni kwa mwezi ambazo ni sawa na wastani wa Sh11.4 bilioni.
Kulingana na hesabu hizo, kila mwaka kampuni hiyo inalipwa Sh136.9 bilioni tangu 2001 walivyoingia mkataba na Tanesco.
Mahitaji makubwa ya umeme Tanzania mara ya mwisho yalirekodiwa kuwa megawati 898.5.
Watakaotumia barabara ya mabasi yaendayo kasi kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limejipanga kudhibiti madereva wa vyombo vya moto wanaokiuka taratibu na sheria za barabarani hasa kwa kutumia barabara za mabasi yaendayo haraka kinyume cha taratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma, Abel Swai, wakati wa majaribio ya mabasi hayo ambayo yalilenga kutoa elimu kwa abiria jijini Dar es Salaam, amesema madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda wanaongoza kwa kukiuka sheria hizo.
“Bodaboda wanaongoza kwa kukiuka sheria na taratibu za barabarani, wanasahau kwamba barabara za mabasi ya mwendo kasi hazitakiwi kutumiwa na vyombo ambavyo havihusiki,” amesema.
Amesema kuwa, magari ya watu binafsi, bodaboda na vyombo vingine havitaruhusiwa kutumnia barabara za DART na dereva atakaekamatwa akitumia barabara hizo atatozwa faini za papo hapo ambayo ni sh. 30000 au kupelekwa mahakamani.
“Jeshi la polisi tumejiandaa kuhakikisha kwamba kila kundi linalotumia barabara linafuata kanuni na sheria za barabarani ili kuondoa usumbufu,” amesema Swai.
Said Mrisho, Mkazi wa Kinondoni ambaye ni dereva wa bodaboda amekiri kuwa kuna baadhi ya madereva wanatumia barabara za DART kwa makusudi na kwamba jeshi la polisi lisiwafumbie macho bali liwachukulie hatua zinazostahili ili kutokomeza ukiukwaji huo.
“Wapo baadhi ya madereva hutumia barabara hizo kwa makusudi, wanajua fika kama ni kosa kisheria lakini wanaendelea kulifanya, mimi ninaomba sheria ichukue mkondo wake dhidi yao,” amesema.
Mrisho amesema usafiri wa mabasi ya mwendo kasi utakapo anza bodaboda zitanufaika kutokana na kwamba zipo sehemu ambazo mabasi hayo hayafiki, na kwamba hali hiyo kwa upande mwingine itaathiri wananchi.
Mwingine mbaroni kwa kuficha sukari
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
Dar es Salaam. Polisi wanamshikilia mfanyabiashara Bushir Haroun kwa tuhuma za kuficha kilo 4,000 za sukari katika ghorofa lake Hananasaf, Kinondon Dar es Salaam.
Mfanyabiashara huyo ambaye leo asubuhi baada ya kuvamiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, anadaiwa kuwa na uhusiano na mfanyabiashara mmoja mkubwa wa sukari ambaye ameficha tani nyingi za bidhaa hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaambia wanahabari kuwa wafanyabiashara ambao wanaficha sukari wanalazimisha viongozi watumie vifungu vya sheria ambavyo hawapendi kuvitumia.
“Huyu mfanyabiashara mkubwa ana tani nyingi za sukari na anatumia ndugu zake kuisambaza nusunusu ili tuzikute katika nyumba za watu kama hivi mnavyoona. Mimi nina uwezo wa kukuhamisha katika mkoa wangu ninapoona unahatarisha maisha ya wakazi Dar es Salaam,” ameonya Makonda.
Haroun, ambaye anashikiliwa na polisi, amekiri kuwa sukari hiyo ni mali yake ambayo aliihifadhi kwa ajili ya kutoa msaada kwa watu wasiojiweza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Christopher Fuime amesema mifuko ya sukari hiyo ilikuwa imechanganywa na gypsum.
Album ya Navy Kenzo ina collabo za kimataifa za kutisha.
Navy Kenzo hawataki mchezo. Album yao ijayo, Above in A Minute ina collabo kibao za kimataifa.
“Tuna collabo na Alikiba, tuna collabo na Patoranking, tuna collabo na R2Bees kutokana Ghana, tuna collabo na Jesse Jagz kutoka Nigeria,” Nahreel ameiambia Bongo5.
Ameongeza pia kuwa ziara yao itaendelea hadi Nigeria na Ulaya.
BUNGENI:Mussa Azzan Zungu Achaguliwa Kuwa Tena Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
KUTOKA BUNGENI: Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azzan Zungu amechaguliwa leo kuwa tena Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akitoa neno la shukrani Zungu amesema nafasi hiyo sio rahisi lakini ataitumikia kwa uadilifu tena bila kupendelea upande wowote.Napia ametoa shukrani kwa wabunge waliomchagua kuwa tena kwenye nafasi hiyo.
Waziri Mkuu: Serikali Itaagiza Tani 70,000 Za Sukari
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaagiza kutoka nje ya nchi tani 70,000 za sukari ambapo kati ya hizo, tani 11,957 zimeshawasili nchini na zitaanza kusambazwa kesho (Jumatano).
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Mei 10, 2016) wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Akitoa ufafanuzi wa sukari ambayo imekwishawasili nchini, Waziri Mkuu alisema tani 2,000 zitapelekwa mikoa ya Kaskazini, tani 3,000 (mikoa ya Kanda ya Ziwa), tani 2,000 (mikoa ya Kusini), tani 2,000 (Nyanda za Juu Kusini) na tani 2,000 (mikoa ya Kanda ya Kati).
“Tani nyingine 24,000 za sukari zitawasili Ijumaa hii na hadi zitoke bandarini itakuwa kama Jumapili kwa hiyo zinaweza kusambazwa kuanzia Jumatatu. Tani nyingine 20,000 zitawasili baadaye, ama mwishoni mwa mwezi huu au mapema mwezi Juni,” alisema Waziri Mkuu.
Amesema anawataka Watanzania wasihofu kuhusu uhaba wa sukari uliojitokeza hivi karibuni kwani umesababishwa na watu wachache.
“Mheshimiwa Rais ameagiza watu waliohodhi bidhaa hii wakamatwe na sukari isambazwe. Lakini pia tunaagiza kwa muda mfupi kwa sababu viwanda vyetu vinatarajia kuanza uzalishaji ifikapo Julai,” alisema.
Amewataka wasambazaji wa sukari waziuze kwa wafanyabishara wadogo ili wao wawawuzie wananchi kwa bei elekezi ya sh. 1,800.
Pia amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia zoezi la ukaguzi ili kubaini zaidi wale waliohodhi bidhaa hiyo.
Akifafanua kuhusu mkakati wa Serikali kuongeza uzalishaji wa sukari nchini, Waziri Mkuu amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha tatizo la uhaba wa sukari nchini linakwisha ifikapo 2019.
“Wananchi wasiogope, Serikali imechukua hatua kwa udhibiti mzuri ili tusije kuporomosha soko letu la ndani,” alisema.
“Tunao mkakati wa kuboresha viwanda vya ndani, wenye viwanda wenyewe au kwa ubia na wawekezaji kutoka nje, wanaweza kufungua mashamba kwenye maeneo matatu tuliyotenga kwa ajili hiyo,” alisema.
“Serikali imetenga maeneo matatu yanayofaa kwa kilimo cha miwa huko Bagamoyo, Ngerengere na Kigoma. Huko wanaweza kulima na kujenga viwanda vya sukari na uzalishaji ukawa unapanda mwaka kwa mwaka hadi tutakapoweza kuimaliza hii gap iliyopo,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S . L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MEI 10, 2016.
HILI NDILO BALAA JIPYA LA MAKALIO YA KICHINA
Tabia ya baadhi ya wasichana hasa wa mjini kuwa na tamaa ya kuwa na makalio makubwa na hivyo kulazimika kutumia dawa mbalimbali, imekuwa ikishamiri kila siku licha ya serikali kuHIpiga marufuku uingizwaji wa dawa hizo
Gazeti hili matoleo yaliyopita liliwahi kuandika jinsi mastaa wengi Bongo wanavyotumia dawa hizo lakini uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, kasi ya matumizi ya dawa hizo yamekuwa yakishamiri huku waathirika wengi wakijiuguza kwa siri baada ya kupata madhara.
Katika tukio jipya la hivi karibuni, mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Hamisa ambaye alidai ni mke wa mtu alisema kuwa, alishawishiwa na rafiki yake kutumia dawa hizo ili naye awe na ‘zigo’ lakini ameanza kuona zinamletea matatizo.
“Nimekuwa nikisikia kuwa dawa hizi zina madhara lakini kuna rafiki yangu mmoja ambaye aliwahi kutumia na yuko poa ndiye aliyenipeleka kwenye duka moja lililopo Kijitonyama na kununua. Awali sikuona tatizo lakini kadiri siku zinavyokwenda nahisi maumivu f’lani, najuta kuzitumia dawa hizi kwa kweli,” alisema mwanamke huyo.
OFM mtaani
Baada ya kupata malalamiko hayo, waandishi wetu walifanya uchunguzi na kubaini kuwa dawa hizo zinauzwa kwa siri sana tangu serikali icharuke na kutoa tamko la kuwashughulikia wale wanaoziuza.
Katika uchunguzi huo, yamegundulika maduka kibao mitaa ya Kariakoo, Kinondoni na Mwenge jijini Dar ambapo wauzaji huziuza dawa hizo ‘kimagutu’ kana kwamba wanauza madawa ya kulevya au bangi.
Mwandishi wetu alifika kwenye duka moja lililopo Msimbazi baada ya kulengeshwa kuwa dawa hizo zinauzwa hapo, muuzaji alipoulizwa uwepo wa dawa hizo, kwanza alikataa lakini baadaye alikubali huku akionekana ni mwenye wasiwasi.
Afisa Habari wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania, Gaudensia Simwanza.
Dukani kwa Maimartha
Ilidaiwa kuwa, asilimia kubwa ya mastaa wanaotumia dawa hizo wanazinunua kwenye duka la Mtangazaji wa Azam TV, Maimartha Jesse na ili kujiridhisha OFM walitinga kwake na kumkuta dada ambaye jina lake halikufahamika ambaye alisema dawa hizo hawana dukani hapo ila mwandishi akitaka anaweza kutafutiwa.
Baada ya mwandishi kujifanya anazihitaji kwa udi na uvumba, mdada huyo alimpigia simu mtu ambaye haikujulikana ni nani na ndani ya muda mfupi akawa amezileta dawa hizo ambazo zipo kwenye mfumo wa losheni.
Alipopigiwa simu Maimartha na kabanwa juu ya kudaiwa kuwaharibu wanawake wenzake kwa kuwauzia dawa hizo, aliruka kimanga na kusema:
“Mimi sitaki kuzungumzia kuwa nauza au siuzi kwa sababu naiheshimu sana serikali na nafuata maelekezo wanayotoa, lakini ninavyojua dawa hizo zinauzwa kwa siri sana na wanaotaka kuuziwa ni wengi.”
Aidha, wasanii wengi hawa wa kike wamekuwa wakidaiwa kutumia dawa hizo huku mastaa wa kizazi cha sasa kama vile Gift Stanford Gigy, Glasnost Kalinga ‘Gilla’, Asha Salumu ‘Kidoa’, Janet Jackson ‘Jayjay’ na wengine wakidaiwa kuwa maumbile waliyonayo siyo ‘orijino’.
Ijumaa lilipata fursa ya kuzungumza na wadada hao ambao sasa ni habari ya mjini kutokana na maumbo yao ambapo kila mmoja alifunguka kivyake:
Gigy: Kusema ukweli sijawahi kutumia dawa hizo, nazisikia tu. Umbo langu ni orijino na wala hayo masponji zivai, hata nikivua sasa.
Kidoa: Shepu yangu ni ya kuzaliwa nayo, najua dawa za Kichina ni shida hivyo siwezi kuthubutu kuzitumia.
Gilla: Mh! Wapo wanaoniambia natumia dawa hizo, kiukweli nimezaliwa hivyo na hivi sasa nimepungua hapo mwanzo si ndo mgenishangaa.
TFDA wanasemaje?
Baada ya OFM kufanya uchunguzi wake, waandishi wetu walizungumza na Afisa Habari wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania, Gaudensia Simwanza ambaye alisema wanapambana kuhakikisha dawa hizo haziingii nchini na atakayekamatwa cha moto atakiona.
“Lakini kwa kuongeza tu ni kwamba kuhusu watumiaji wanaopata madhara kwa matumizi ya dawa hizo wengi unakuta hatuna taarifa nao kwa sababu huwa hawaji kwetu moja kwa moja, wanakwenda mahospitali na sehemu nyingine kupata tiba, ila tunapopata taarifa kama hizi tunafuatilia na kuzitendea kazi,” alisema Simwanza.
Aidha, dokta mmoja anayefanya kazi katika wizara ya afya ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa, sasa hivi wako makini kuhakikisha uuzwaji holela wa dawa zenye madhara kwa watumiaji unakoma.
“Unajua hiki siyo kipindi cha mchezo, TFDA wanafanya kazi yao lakini wizara ya afya nayo inapambana, kikubwa ni tahadhari kwa watumiaji wa dawa hizo, wajue kwamba kuna madhara makubwa ambayo yanaweza kuhatarisha maisha yao hivyo waache,” alisema dokta huyo.
SOURCE GLOBAL PUBLISHERS