Wednesday, June 15, 2016
Rais Magufuli awataka watanzania kuungana na Waislamu walio katika mfungo kuliombea taifa
Ajali !!!Bus la TAHMEED lateketea kwa moto
Leo BASI LA TAHMEED LATEKETEA KWA MOTO MCHANA HUU
Basi la abiria mali ya Kampuni ya Tahmeed, lililokuwa likitokea Jijini Tanga kuelekea Jijini Dar es salaam, likiteketea kwa moto mchana huu katika eneo la Komkonga. Inaelezwa kuwa Ajali hiyo imetokea wakati Basi hilo likiwa limesimama baada ya Abiria mmoja kuomba msaada tutani "WA KENDA KUCHIMBA DAWA" ambapo baadhi ya Abiria wengine nao walishuka na kusikia harufu ya tairi linaloungua. muda mchache tu tairi hilo lilipasuka na moto kuanza kusambaa hadi kwenye tanki la Mafuta.
Hakuna mtu yeyote aliepoteza Maisha kwenye ajali hii na hakuna mali iliyoweza kuokolewa.
Udaku special blog
STIVE NYERERE AWAPA 'BIG UP' HARMONIZE NA IYOBO KWA KUWATULIZA AUNT EZEKIEL NA JACKLINE WOLPER
Mmoja kati ya wasanii wakongwe wa filamu nchini, Steve Nyerere amempongeza msanii wa muziki, Harmonize pamoja na dancer wa Diamond, Mosei Iyobo kwa kuwapa utulivu wasanii wenzake wa filamu Aunt Ezekiel na Jacqueline wolper.
Muigizaji huyo ambaye alikuwa MC katika iftar ya GSM iliyofanyika Kigamboni weekend hii na kuhudhuriwa na mastaa mbalimbali, alisema anawashukuru wasanii hao wa muziki kwa uwamuzi wa kuwahifadhi dada zake hao.
“Mimi nashukuru wasanii wa bongofleva kwa kuwahifadhi dada zetu, Aunt yupo poa, na Wolper naona safi,” alisema Steve Nyerere huku akicheka.
Wolper na Harmonize kwa sasa ni wapenzi na kila mmoja anaonyesha anampenda mwenzake, na Aunt Ezekiel na Mose Iyobo ni wapenzi wa muda mrefu na wanaishi kama familia na mtoto wao mmoja aitwae Cookie.
Chadema Yaondoa Kesi Yake Dhidi ya Polisi
Chadema imeondoa mahakamani kesi dhidi ya polisi ya kupinga amri ya kupiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara, baada ya kubainika mapungufu ya kisheria katika hati yao ya mashtaka.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii ofisini kwake jana, Jaji Mohamed Gwae aliyepangwa kusikiliza shauri hilo alitaja mapungufu ya kisheria yaliyobainika kwenye hati ya mashtaka ya Chadema kuwa ni pamoja na kumjumuisha katika hati ya mashtaka Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Mssanzya, ambaye kisheria alistahili kufunguliwa shtaka katika masjala kuu (main registry).
“Baada ya kushauriana na mawakili wa Chadema kuhusu suala hilo, waliamua kwa hiari yao kuondoa kesi yao kwa ajili ya kuifanyia marekebisho hati yao ya mashtaka,”alisema Jaji Gwae.
Akifafanua, Jaji huyo alisema Chadema wana njia mbili za kurekebisha kasoro hiyo; moja ni kufungua shauri hilo masjala kuu ya mahakama jijini Dar es Salaam ili kuendelea kumshtaki Kamishina Mssanzya.
Njia ya pili kwa mujibu wa Jaji Gwae ni Chadema kuendelea na shauri hilo jijini Mwanza dhidi ya wakuu wa polisi wa wilaya za Maswa, Kahama na Geita bila kumjumlisha Kamishna Mssanzya.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutoka ofisini kwa Jaji, Wakili wa Chadema, John Mallya aliyekuwa na mwenzake Paul Kipeja, alisema shauri hilo halikuanza kusikilizwa jana kutokana na kutokamilika kwa taratibu za kiofisi za kimahakama.
"Shauri letu bado lipo na tayari limepangiwa Jaji wa kuisikiliza; ni imani yangu kuwa kesho (leo), hatima ya kesi yetu itajulikana,” alisema kwa kifupi wakili Mallya bila kutoa maelezo zaidi.
Juni 10, mwaka huu, Chadema ilifungua kesi mahakamani kupinga amri ya polisi ya kupiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara ya kisiasa, kwa kile kilichodaiwa kuwa ni tishio la kiusalama.
Katika hati ya mashtaka iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, Chadema inaiomba mahakama kutamka kuwa amri hiyo ni batili na utekelezaji wake pia ni batili.
Maombi mengine ni mahakama kutoa zuio la kimahakama kwa polisi kutotoa amri za aina hiyo tena na mahakama kuruhusu vyama vya siasa kuendelea na shughuli za kisiasa, ikiwamo maandamano na mikutano ya hadhara, huku polisi wakiagizwa kulinda usalama kama sheria inavyoagiza.
MPEKUZI
Picha za harusi ya Samuel Eto'o akifunga ndoa na , mpenzi wake wa siku nyingi Georgette Tra Lou huko Italy
RUBY NA ASLAY WAFUNGUKA JUU YA HUSIANO YAO
Msanii wa muziki wa bongo Ruby ambaye ameshirikishwa kwenye wimbo mpya wa kundi la Yamoto Band amefunguka na kusema yeye na Aslay si wapenzi kama ambavyo watu wanasema bali anadai hiyo ilikuwa ni njia kutangaza kazi yao mpya ambayo Rubby ameshiriki.
Kupitia kipindi cha Planet Bongo cha East Africa Radio, Rubby alidai ilibidi watafute kiki kuwa anatoka kimapenzi na Aslay ili waweze kuitangaza kazi hiyo mpya ya Yamoto Band inayoitwa ‘Suu’ ambayo wamefanya pamoja.
“Unajua siku hizi maisha yamebadilika na mashabiki wanapenda sana kiki, hivyo kwa kuwa wanapenda hayo ilibidi tuwape kitu roho inapenda lakini ukweli ni kwamba mimi na Aslay ni marafiki tu si wapenzi kabisa, ilikuwa kiki tu hiyo ili kusaidia kazi hii kufika sehemu kwa haraka” alisema Rubby
Kwa upande wake Aslay alipoulizwa juu ya suala hilo alisema kuwa kitu alichosema Rubby ndiyo uhalisia wenyewe na kukana si wapenzi kama ambavyo awali tetesi zilivyokuwa zikienea kwenye mitandao ambazo zilitengenezwa na wao wenyewe, kwa kuanza kupostiana kwenye mitandao ya kijamii.
eatv.tv
Jenerali Ulimwengu Ataka Kikwete Ashitakiwe.....Adai Kaisababishia Serikali Hasara Kubwa
Mwanahabari nguli nchini Jenerali Ulimwengu amesema Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete anapaswa kushtakiwa mahakamani kwa kuisababishia hasara Serikali kutokana na mabilioni ya shilingi yaliyotumika katika mchakato wa Katiba ambayo haikupatikana.
Akizungumza katika tamasha la nane la Kigoda cha Mwalimu Nyerere katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) jana, Jenerali Ulimwengu alisema fedha nyingi zimepotea wakati wa kuunda Katiba Mpya ambayo haikupatikana.
Mbali ya fedha zilizotumika na Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakati wa kukusanya maoni na nyingine zilizotumika kurekebisha ukumbi wa Bunge uweze kubeba wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, jumla ya Sh24.53 bilioni zilitumika kulipa posho za wajumbe.
Tamasha hilo lililojikita kujadili falsafa za Mwalimu Nyerere katika muktadha wa “Visheni ya Maendeleo ya Watu,” liliwakutanisha wasomi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, wanafunzi na wanasiasa wakiwamo Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba.
Jenerali aliyekuwa anajadili hotuba ya mgeni rasmi, Benjamin Mkapa, alisema fedha nyingi ziligharamia mchakato wa Katiba uliokuwa unaendeshwa na Tume ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba, lakini ulikwama, ndiyo maana hadi leo hakuna Katiba mpya.
“Itabidi (Kigoda cha Mwalimu) mumuite mwaka ujao, aje aeleze fedha za wananchi zilizotumika katika mchakato ule zilikuwa na sababu gani,” alisema Jenerali aliyekuwa akishangiliwa na wahudhuriaji.
“Iwapo mawaziri wa zamani wamechukuliwa hatua na kupelekwa mahakamani kwa kusababisha hasara, Mheshimiwa Kikwete anastahili kupelekwa mahakamani kwa kusababisha hasara kwa Serikali na kuzima matumaini ya wananchi na kuachwa wanarandaranda wasijue wafanye nini na baadaye inaweza kutuletea machafuko, kama hatukuweza kutengeneza Katiba ambayo itatuwekea mustakbali wa Watanzania,” alisema.
Jenerali alisema suala la Katiba limekwama na limekwamishwa kwa makusudi kabisa.
Kuhusu Mwalimu Nyerere, Jenerali alisema asingekuwa anazungumzwa kwa sifa nyingi kama sasa, iwapo asingechukua uamuzi wa mwaka 1992 wa kuruhusu mfumo wa vyama vingi, licha ya kwamba waliokuwa wameukubali ni asilimia 20 ya Watanzania.
Kuhusu Rais John Magufuli, Jenerali alisema pamoja na sifa anazopewa sasa za utendaji wake, akitazamwa kwa uwanda mpana, nchi imerudi nyuma kwa miaka 50 kwa masuala ya demokrasia.
Akifafanua namna nchi ilivyorudi nyuma, alisema, “Kwa kufinya uhuru wa kujieleza na hususan kwa kufinya uhuru wa wawakilishi wa wananchi ndani ya Bunge.”
Baadaye, Rais mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo alifafanua kauli ya Jenerali kwa kusema yeye (Mkapa) hakuwa mshauri wa Rais, bali Jaji Warioba alimfuata atoe ushauri na hakuwa kwenye ngazi yoyote ya uamuzi.
“Kwenye chama changu sikuwemo na kwenye Serikali sikuwemo. Siwezi kulizunguzumzia hilo na waandishi wanapenda nitoe maoni,” alisema Mkapa.
Alisema ipo haja ya kujiuliza kwa nini Katiba hiyo ilikwama na hadi sasa hajasikia uchambuzi wa kina kuhusu jambo hilo.
“Kuna haja ya kuwa na mjadala mkubwa lakini siyo kulaumiana tu. Siyo kudai tu. Kuwezesha uhuru wa kuzungumza ni jambo moja na kutumia uhuru huo ni kujadili, kuchambua na kupima na kufanya uamuzi sahihi kitu kingine kabisa,”alisema Mkapa.
Alisisitiza kuwa badala ya kumlaumu mtu mmoja mmoja, mjadala mpana wa kitaifa unahitajika ili kujua kilichosababisha Taifa kukosa Katiba Mpya.
“Hakuna anayeandika ni wapi tulipokwama, tunalaumu na kumjadili mtu, wengine wanasema Katiba imekwamishwa na watu wachache kwa sababu za kimaslahi…tunapaswa kuwa na mjadala wa kina kujua ni wapi tulipokwama,” alisema Mkapa.
Aidha, Jenerali aliwananga viongozi wastaafu akisema amebaini sasa kuwa kwa bahati mbaya wanapata busara baada ya kuacha nafasi za uongozi.
Alisema ili kuwa na busara wakati mtu akiwa madarakani, anatakiwa awasikilize wale anaowaongoza na njia moja ya kufanya hivyo ni kuwapa Katiba ambayo ndiyo mwongozo utakaosimamia mustakabali wao.
Awali, akiwasilisha mada katika tamasha hilo, Mkapa alisema si kana kwamba Mwalimu Nyerere hakupenda kampuni binafsi zije kuwekeza nchini bali alipenda biashara na uwekezaji vifanyike kwa haki, usawa na kuchangia maendeleo ya nchi.
Kuhusu sukari, Mkapa ambaye alijitetea kwa kuanzisha sera ya ubinafsishaji, alisema wakati anaingia madarakani, viwanda vya sukari vikiwamo Kilombero na Mtibwa vilikuwa havizalishi kabisa au kuzalisha kidogo, hivyo kulikuwa na tatizo la sukari.
Alisema baada ya ubinafsishaji, sukari ilianza kuzalishwa kwa wingi lakini akahoji ni nini hakikufanyika hadi nchi ikafikia mahali ilipo sasa.
Ugawaji mikoa
Akichangia mjadala huo, mhadhiri mwandamizi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Martha Qorro alisema Serikali imeendelea kuongeza idadi ya mikoa, jambo ambalo linazidi kuwagawa wananchi.
Pamoja na kuathiri umoja wa kitaifa, mhadhiri huyo alikuwa na maoni kuwa, fedha nyingi kwa sasa zinatumika kuendesha mikoa inayoongezwa badala ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
Hata hivyo, Mkapa alisema wakati wa uongozi wake aliongeza mkoa mmoja tu wa Manyara, ambao aliumega kutoka Arusha baada ya kuona uhitaji na kufanya vikao.
Rais huyo mstaafu alisema suala la kuzingatia wakati wa ugawaji wa mikoa ni kutowagawa wananchi kwa misingi ya ukabila na udini.
Mstaafu huyo aliyeiongoza nchi kipindi cha mwaka 1995-2005, alisema suala la kuangalia ni mahitaji ya watu ndiyo maana alikaa na viongozi wa maeneo yote hayo na hatimaye kufanikiwa kuigawa Arusha.
Alisema Watanzania wengi wamekuwa na desturi ya kutumia muda mwingi katika kuilaumu Serikali badala ya kufanya kazi kwa maendeleo ya nchi.
“Watanzania tunatakiwa tufanye kazi kwa bidii ili tuifikishe nchi yetu kwenye maendeleo na si kutumia muda mwingi katika kuilaumu Serikali,” alisema Mkapa.
Maalim Seif Azungumza mazito kwa Wamarekani Kuhusu Sakata Zima la Zanzibar
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad amesema vitendo vya unyanyasaji wapinzani vinavyoendelea nchini ni maradhi yanayokikumba chama tawala.
Maalim Seif aliyasema hayo alipokuwa akihutubia mkutano uliondaliwa na Kituo cha Elimu cha Kimkakati cha Kimataifa cha Marekani (CSIS) juzi, uliofanyika Washington DC nchini Marekani.
Akizungumzia kukandamizwa kwa wapinzani nchini, Maalim Seif alitoa mfano wa yeye kuhojiwa na polisi 11 kwa saa tatu na kijana aliyehukumiwa kifungo cha miaka mitatu au kulipa faini ya Sh7 milioni kwa kumkosoa Rais John Magufuli kwenye ukurasa wa facebook.
Kadhalika alitoa mfano wa viongozi wa Chadema kuhojiwa polisi na baadhi kuwekwa rumande kwa saa kadhaa huku kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo naye akihojiwa kwa kufanya mkutano.
“Tunashuhudia mmomonyoko wa hali ya juu wa demokrasia sasa hivi… na hali hii itazidi miezi michache ijayo,”alisema.
Alisema wapinzani wanakandamizwa zaidi upande wa Zanzibar, na kusema kuwa CUF inataka ufafanuzi wa Muungano na wala si kuufuta.
Kiongozi huyo wa CUF alimlaumu Rais John Magufuli na kusema licha ya kuwa nchi za nje zinamuona anafanya vyema katika kupambana na rushwa, lakini Wazanzibari hawana furaha na uongozi wake.
“Kuna mitazamo tofauti hasa kwa walio nje ya Tanzania kwamba anapambana na rushwa, lakini kama kiongozi wa nchi, ameshindwa kufanya majukumu yake kuhusu Zanzibar,” alisema
Alisema mara zote Rais Magufuli anapoulizwa kuhusu suala la Zanzibar, husema hawezi kuchukua hatua.
“Wazanzibari wanachokitaka ni kuona Rais Magufuli anawajibika kama kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Maalim Seif ambaye katika mkutano huo, aliambatana na mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa Ladhu na katibu wake, Issa Kheri Hussein.
Pamoja na mambo mengine, Maalim Seif alisema chama chake kipo tayari kufanya uchaguzi mwingine, endapo utasimamiwa na taasisi za kimataifa zisizofungamana na upande wowote.
Alisema wakati wakisubiri hilo, wafuasi wa chama hicho wanaendelea kufanya mgomo baridi usio na nia ya vurugu ili kuonyesha kuwa mambo hayawezi kwenda kama kawaida.
Akijibu swali la mmoja wa waliohudhuria mkutano huo kuhusu kutuhumiwa kuuvunja Muungano endapo atakuwa Rais wa Zanzibar, Maalim alisema chama tawala kimekuwa kikivibatiza vyama vya upinzani majina ya uongo ili kuvibomoa.
“Kuna wakati walikiita CUF kuwa ni chama cha Kiislamu, lakini hilo si kweli, tumenyang’anywa ushindi zaidi ya mara tano na wala hatujaleta fujo,”alisema.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast, Maalim alielezea jinsi uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana ulivyofutwa na kusema kuwa CUF imekuwa ikinyang’anywa ushindi tangu mfumo wa uchaguzi wa vyama vingi uanze mwaka 1995.
“Tumefanya chaguzi tano, 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015 katika chaguzi zote hizi, watu wa Zanzibar waliichagua CUF kuongoza Serikali. Lakini CUF imenyimwa kushika madaraka,” alisema Maalim na kuongeza:
“Kuna harufu ya hatari, kwa miaka yote hiyo tumejitahidi kuwatuliza wafuasi wetu, tumeangalia namna ya kuzungumza na wenzetu ili waheshimu maamuzi ya watu, lakini hawasikii.”
Alisema uchaguzi wa mwaka jana ulifanyika kwa uhuru na haki na matokeo yalionyesha kuwa CUF kimeshinda, lakini polisi waliizingira Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na baadaye Mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salim Jecha akayafuta matokeo hayo.
Alisema hata Umoja wa Ulaya (EU) walitoa ripoti yao wiki mbili zilizopita, iliyoonyesha kuwa ZEC haikuwa na mamlaka ya kufuta matokeo hayo.
“Nilijaribu kuwasiliana na Dk Ali Mohamed Shein , lakini hakutaka kupokea simu yangu, lakini baadaye nilimuandikia barua nikitaka mazungumzo naye, alikubali kwa masharti kuwa wawepo watu wengine.”alisema na kuongeza:“Tukakubaliana tufanye mazungumzo, lakini wawepo viongozi wakubwa, wakati tukiendelea na mazungumzo, Jecha alitangaza kuwa uchaguzi utarudiwa Machi 20.”
Maalim Seif alitaja athari za kufutwa kwa uchaguzi huo kuwa ni pamoja na kuvunja maridhiano ya kisiasa ya Zanzibar na Maamuzi ya Wazanzibari wengi walioamua nchi yao iongozwe kwa Mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Alitaja athari nyingine kuwa ni kuwarudisha nyuma watu wa visiwa vya Unguja na Pemba, kuibuka kwa siasa za chuki, migogoro na kubaguana.
“Hayo ni pamoja na kudhoofika kwa sekta za uchumi, biashara, ukosefu wa ajira na maendeleo kwa jumla, na siyo kwa Zanzibar pekee bali kwa Jamhuri yote ya Muungano wa Tanzania, hasa iwapo Mataifa yataitenga na kulinyima Taifa misaada, hali ambayo haiwezi kuepukika”. alisema
Akieleza msimamo wa waandaaji wa mkutano huo, uliojumuisha marais mbalimbali wastaafu wa Marekani na Ulaya, Mkurugenzi Mkuu wa NDI, Peter Craig aliwataka viongozi wa kisiasa wa nchi nyingine za Afrika kuiga mwenendo wa Maalim Seif.
“Tunaomba watu wengine wenye migogoro ya aina hii waige mfano huu wa Seif Sharif Hamad na sisi tutakuwa pamoja nao mpaka haki itendeke na ipatikane na tukianzia na Zanzibar,” alisema