Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea na Celtic Chris Sutton amepigilia msumari wa moto kwa Arsenal kwa kusema kwamba kamwe wasitarajie ubingwa kama timu hiyo itaendelea kuwa chini ya Arsene Wenger.
Katika dirisha hili la usajili Arsenal wamemsajili Granit Xhaka tu, huku wenzao Manchester City, Manchester United na Chelsea wakiwa wamefanya usajili wa maana kuimarisha vikosi vyao kwaajili ya msimu mpya.
Sutton ambaye alibeba kombe la Ligi ya England akiwa na Blackburn Rovers, amemlaumu Arsene Wenger kwa kutoonesha nia ya dhati ya kufanya usajili wa kusiaidia timu na kusisitiza Mfaransa huyo anahitaji kuachia ngazi kwa manufaa ya timu.
“Nina mashaka makubwa na Arsenal katika msimu huu tena. Hawajaonesha nia yoyote mpaka sasa,”Sutton aliiambia BBC Five Live.
“Nadhani bodi na Wenger wanawaangusha sana mashabiki wao. Mimi sijui ni wapi Arsenal wanaelekea, kama ningekuwa ni shabiki wa Arsenal, basi ningehuzunika sana.
“Wamesema hatawatumia fedha nyingi, bodi inafurahia tu jambo hili, au uongo? Kila mwaka, wao kazi yao ni kushiriki Ligi ya Mabingwa na kupata fedha.
“Wenger sio kocha mwenye malengo na Arsenal tena, alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda taji msimu uliopita, lakini alishindwa. Hawataki kutumia pesa, na kama wewe ni shabiki wa Arsenal, jitathmini vizuri, maana kila mwaka itakuwa ni mwendo wa ‘top four’ tu.
Halafu unaona timu kama Manchester United, Manchester City wanaonesha nia ya ubingwa msimu huu, hili linazidi kuleta ugumu zaidi kwa Arsenal, nasema hivi….mpaka Wenger aondoke ndipo Arsenal watatwaa ubingwa.”