TATIZO la kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi huwapata wanawake wengi walio katika umri wa kuzaa na wale waliomaliza majukumu yao ya uzazi.
Tatizo linapojitokeza huleta athari nyingi kwa mwanamke kwa kumfanya ashindwe kupangilia mipango yake.
JINSI TATIZO LINAVYOTOKEA
Mwanamke hulalamika kutofahamu vizuri siku zake, hajui anaingia lini, yaani damu inaweza tu kutoka na inachukua muda mrefu hata zaidi ya siku saba ikiwa nyingi au matone matone. Mwanamke hushindwa kupangilia siku za kupata mimba, tatizo huanza taratibu na mwishowe huchukua muda mrefu.
CHANZO CHA TATIZO
Tatizo hili huweza kusababishwa na kuvurugika kwa mfumo wa homoni mwilini, hasa homoni au vichocheo vinavyoendesha na kudhibiti hedhi na uzazi kwa ujumla.
Uwepo wa uvimbe ndani ya kizazi au kwenye vifuko vya mayai pia ni tatizo. Mabadiliko katika tabaka la ndani la kizazi, maambukizi sugu ya kizazi na kuharibika kwa mimba ni mojawapo ya matatizo haya yanayochangia siku za hedhi zitoke bila ya mpangilio.
Matumizi ya baadhi ya madawa na hata dawa za uzazi wa mpango kwa wengine mfano sindano au vipandikizi huweza kuvuruga homoni na kusababisha matatizo haya.
DALILI ZA TATIZO
Mwanamke mwenye tatizo hili hulalamika kutokufahamu mwenendo wa mzunguko wake, hulalamika damu kutoka muda mrefu au siku chache sana chini ya siku tatu, wakati mwingine hapati kabisa.
Anaweza kuwa na maumivu ya tumbo chini ya kitovu, maumivu wakati wa hedhi, maumivu wakati wa kujamiiana na hata damu kutoka mabonge au nyingi na nyepesi. Pia ataelezea ni muda mrefu anatafuta mtoto lakini hapati.
UCHUNGUZI
Tatizo hili humuathiri mwanamke kwa kiasi kikubwa hasa pale damu inapotoka kwa muda mrefu kwa zaidi ya siku saba au asipopata kabisa hedhi katika umri wake kama unamruhusu, pia mwanamke hatakuwa vizuri anapopata maumivu wakati wa hedhi, au anapotafuta mtoto halafu hapati ujauzito.
Uchunguzi hufanyika katika kliniki za madaktari bingwa wa akina mama katika hospitali za mikoa, vipimo mbalimbali vitafanyika kadiri daktari atakavyoona inafaa. Vipimo pia vitazingatia mahitaji ya mwanamke kama yupo tayari kushika ujauzito kwa kipindi hicho. Kwa hiyo katika upimaji atachunguzwa na mfumo wake wa uzazi.
NINI CHA KUFANYA?
Ni vema mwanamke mwenye matatizo haya akazingatia ushauri wa daktari wake ili aweze kupona na kufanikiwa malengo yake ya kupata ujauzito. Baada ya uchunguzi wa kina ndipo utaratibu wa matibabu unaanza.
Mwanamke ambaye ameshafikia ukomo wa kuzaa yaani zaidi ya miaka arobaini na tano na ana matatizo haya basi azingatie sana uchunguzi na tiba.
Pamoja na kwamba tumeona vyanzo mbalimbali vya tatizo hili, lakini pia tusisahau saratani au kansa ya shingo ya kizazi na ya kizazi kwa ujumla vinabidi vichunguzwe kwani dalili zake hazitofautiani sana na matatizo mengine. Wahi hospitali kwa uchunguzi na tiba.