MWANASIASA mkongwe nchini, Dk Chrisant Mzindakaya, ameushauri uongozi
wa mkoa wa Rukwa kuunda timu ya wataalamu kupendekeza miradi ya
maendeleo inayofaa kutekelezwa mkoani humo.
Alipendekeza timu hiyo ijumuishe wataalamu kutoka katika taasisi za
fedha nchini na wizarani ambao watatafsiri wasifu wa mkoa huo na kuandaa
kitabu kitakachoeleza mikakati ya maendeleo ya mkoa.
“Mikakati hiyo ni pamoja ya namna ya kuanzisha au kuendeleza viwanda
vidogo, vya kati na vikubwa vitakavyoongeza thamani ya mazao kwa
kuyasindika,” alisema. Alisema kuwa inasikitisha kuona Mkoa wa Rukwa
ulio miongoni mwa mikoa inayolima mahindi kwa wingi unaagiza mbegu bora
kutoka nje ya nchi au kuletewa za bandia na kusambazwa kwa wananchi.
Alilieleza gazeti hili kuwa, maendeleo ya mkoa huu hayatakuja kwa
kutegemea watu wengine walioko nje ya mkoa. Aidha, alishauri
wafanyabiashara wa kati na wakubwa mkoani humo wakutane kutambuana ili
watoke kwenda kutafuta wawekezaji katika miradi mbalimbali mkoani Rukwa.
Alisisitiza kuwa mageuzi ya maendeleo lazima yafanywe na wazawa
wenyewe badala ya kukaa kusubiri watu kutoka nje ya mkoa. “Mkoa
umeshafanya makongamano mawili (Julai , 2007 na Novemba 2013) na
mahudhurio yalikuwa ya kuridhisha, lakini matokeo yake sio mazuri kwa
kuwa hakuna mwekezaji kutoka nje aliyeonesha nia wala kuja kuwekeza
mkoani kwetu,” alisema Mzindakaya.
Alisema, jibu la kweli na rahisi ni wawekezaji kuja kutoka mikoa
mingine, lakini ni vigumu kama hakuna msukumo wa vipaumbele na fursa za
uwekezaji zilizo wazi hasa kwa mkoa huo ambao kijiografia uko pembezoni.
Mzindakaya alisema mkoa huo una zaidi ya viwanda 30 vidogo vya
kusindika alizeti katika hatua ya kwanza, hivyo kusababisha wananchi
kuendelea kutumia mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.
Alikumbusha kuwa mwaka 1974 mkoa wa Rukwa katika viwango vya mapato
na maendeleo ulikuwa wa 18 kati ya mikoa 20 iliyokuwepo nchini, baada ya
miaka minne hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliutangaza
kuwa miongoni mwa mikoa minne inayozalisha mahindi kwa wingi nchini.
Alieleza kuwa hayo yaliwezekana baada ya viongozi wa Serikali na
wabunge kuwashirikisha wananchi kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo
ambayo mkoa unajivunia hadi sasa.