NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni amesema askari wa usalama barabarani watakaobainika kupokea rushwa watashughulikiwa kwa kuwa wataweka mitego kwa ajili ya kuwakamata.
Alisema wananchi wamekuwa wakilalamikia askari hao kuwa wanapenda rushwa na ndio chanzo cha ajali barabarani na kwamba wanachafua taswira ya jeshi hilo.
Akizungumza na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam jana jijini humo, Masauni alisema mtego watakaouweka ndilo kaburi lao na kwamba watafungwa kwa sababu ya tamaa ya Sh 10,000, hivyo wajihadhari.
Alisema Taifa linakabiliwa na changamoto ya ajali za barabarani na kwamba wana wajibu wa kuwalinda raia wa nchi hii, badala ya kushiriki kuwaangamiza kwa tamaa ya fedha. Alisisitiza kuwa hawataweza kufikia uchumi wa kati endapo nguvu kazi zitaendelea kupotea kutokana na ajali za barabarani.
“Kuondoa ajali inawezekana na watu watakaoleta sababu za ajabu ajabu hiki sio kipindi chake ni lazima tuzitekeleze kama tulivyopanga kwenye mkakati wetu kwamba ndani ya miezi sita tuwe tumepunguza ajali kwa asilimia 10,”alisema akisisitiza askari kubadilika, kwani ndio wasimamizi wakubwa wa usalama barabarani.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili askari hao, alisema kuwa wapo baadhi ya askari ambao wanafanya kazi katika mazingira hatarishi na magumu kama vile kupigwa risasi, kugongwa na magari na kwamba jitihada zao zinatakiwa zitambulike kwa kupandishwa vyeo na mishahara kwa kazi nzuri wanazofanya.
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga alisema mkutano huo ni sehemu ya kutoa elimu kwa askari watakaosimamia mkakati huo kuhakikisha ajali zinapungua.
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Abdulrahman Kaniki alisema ajali za barabarani ni miongoni mwa changamoto zinazolikabili Taifa.
Alisema ni wakati wa askari kuongeza chachu, ari na mbinu katika kutekeleza majukumu yao kwa wananchi na kwamba wapo imara kutekeleza maagizo halali kutoka kwa viongozi wao.