Nassibu Abdul a k a Diamond Platnumz
Miaka kumi tu nyuma, ulipokuwa ukimzungumzia mwanamuziki mwenye jina kubwa kwa sasa, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ hakukuwa na mtu aliyekuwa akimfahamu, labda washkaji zake wa kitaa ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa wakimwambia ‘Mwana wewe pigana tu kuna siku utatusua”.
Ndiyo, alipambana, alipopiga ngoma kama Kamwambie, Mbagala na nyingine nyingi zilimfanya kuwa juu na kumpa tuzo kadhaa. Leo hii, unapomzungumzia Diamond, haumzungumzii yule kijana aliyeiba hereni za mama yake akauze ili akarekodi singo yake, bali utakuwa unamzungumzia msela f’lani mwenye taito kubwa hapa Bongo.
Baada ya kukimbiza sana, mwisho wa siku mwana akajikuta akiwa staa mkubwa, si Bongo tu, mpaka nje ya nchi hii. Kwa sasa, amekuwa ni busta kwa mastaa wengine, yaani staa kutoka ndani na nje ya Afrika anamshukuru Diamond kwa kumfanya kujulikana zaidi. Wapo wengi lakini wachache wafuatao wanaweza kukubali kuwa, Diamond amewabusti kimtindo.
Diamond na AY
AY
Ukizungumzia wasanii wa kwanza-kwanza kutusua nje ya mipaka ya Bongo, huyu msela yupo. Alipiga ngoma nyingi na wasanii wa Uganda, Kenya ila pia alipiga ngoma na msanii kutoka Jamaica, Sean Kingstone.
Baada ya kuvuma sana na kuweka video zake Youtube, hakuwa na watazamaji wengi. Kwa mfano ngoma yake ya Touch Me aliyofanya na Sean Kingstone ambaye ana mashabiki wengi duniani ilipata watazamaji 110,703 duniani kote. Ukiachana na hiyo, ngoma yake ya kimataifa ambayo
aliwahi kufanya na Saut Sol ya I Don’t Wanna Be Alone ilipata watazamaji 26,097.
Achana na video hizo, baada ya kukaa kwa kipindi kirefu ndipo akaamua kufanya hit song na Diamond iitwayo Zigo remix. Cha kushangaza zaidi, ndani ya wiki ya kwanza tu ikawa na watazamaji milioni moja, kwa siku 67 ikawa milioni 5.
Mwenyewe ameshangazwa, hakuamini kilichotokea lakini kwa jicho la tatu ni lazima tugundue kwamba ni nguvu ya Diamond Platnumz ndiyo iliyomfanya kufikisha watazamaji wengi namna hiyo.
Diamond na AKA
AKA
Unapomzungumzia msanii mkubwa Afrika, basi huyu Msauzi, AKA jina lake halitakosa. Ana jina kubwa na amefanya ngoma nyingi ila katika video zake zote, video ambayo imetazamwa na watu wengi ni ile ya Make Me Sing ambayo amepiga na Diamond Platnumz ambayo mpaka sasa ina watazamaji milioni 2,924, 412
Amepaishwa, ameweka rekodi ya kuwa Msauzi wa kwanza video yake kutazamwa na watazamaji wengi ndani ya wiki ya kwanza tu ambayo ilifikisha watu milioni moja. Nyuma ya hayo, kuna jina la Diamond ambalo limemfanya kupata watazamaji wengi kwani ngoma yake yenye watazamaji wengi mbali na hiyo ni Baddest aliyowashirikisha Burna, Chana na Yanga ina watazamaji milioni 1,097,812.
Juzikati alifunguka kwamba amefurahi sana kwani ngoma yake imemtambulisha mpaka nchini Rwanda ambapo yeye anaamini hayo ni mafanikio makubwa, ila kupitia mgongo wa Diamond ameweza kufanya vizuri Afrika Mashariki na ngoma zake kupigwa mara kwa mara.
Diamond na Akothee
AKOTHEE
Ni mwanamuziki mkongwe, kutoka katika familia ya kitajiri nchini Kenya. Inawezekana haukuwa ukimfahamu ila baada ya kufanya Ngoma ya My Sweet Love na Diamond, ukamfahamu.
Ni mwanamuziki aliyepaishwa zaidi na Diamond, amepiga ngoma nyingi lakini hata video zake hazikuwa zikiangaliwa na watu wengi mitandaoni. Akaona kwa kusafisha nyota bora apige Ngoma ya Give It To Me na mwanamuziki kutoka Nigeria, Mr Flavour ndipo ngoma hiyo ikatazamwa na watu 267,573 tu.
Unajua alifanya nini baada ya hapo? Akaamua kutoa ngoma na Diamond iitwayo My Sweet Love ambapo kwa kupitia jina la Diamond mpaka sasa imetazamwa mara 1,494,675, mara tano zaidi ya ngoma aliyopiga na Flavour.
Mbali na kuwang’arisha zaidi wakongwe hao, pia Diamond hakuwa mbali katika kuwatangaza wanamuziki chipukizi akiwemo Hermonize ambaye mpaka sasa video yake ya Bado imetazamwa mara 2,897,477 huku ngoma ya wakongwe, Saut Sol waliyomshirikisha Ali Kiba ya Unconditionally Bae ikiwa imetazamwa mara 1,168,202 tu