Katika kile kinachoweza kutafsiriwa kuwa
ni mzimu wa "Anne Kilango",simanzi imeendelea kuwagubika wakazi wa
Shinyanga kufuatia rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John
Pombe Magufuli kutengeua uteuzi wa aliyekuwa mkuu wa mkoa huo Anne
Kilango Malecela.
Wakazi hao wa Shinyanga wameeleza kusikitishwa na kitendo hicho na kueleza kukata tamaa kama watapata tena kiongozi mchapakazi kama Kilango kwani walikuwa na imani kubwa na mwana mama huyo machachali.
Wakazi hao wa Shinyanga wameeleza kusikitishwa na kitendo hicho na kueleza kukata tamaa kama watapata tena kiongozi mchapakazi kama Kilango kwani walikuwa na imani kubwa na mwana mama huyo machachali.
Uteuzi wake ulitenguliwa baada ya Machi 20, mwaka huu, kudai kuwa mkoa wa Shinyanga hauna mtumishi hewa wa serikali hata mmoja.
Ikulu ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa katika taarifa za awali kuna watumishi hewa 45, huku kazi ya uhakiki ikiendelea katika wilaya za Ushetu na Shinyanga.
Hata hivyo wakazi wa Shinyanga wakiwemo mama ntilie,waendesha bodaboda,wakulima,waumini wa madhehebu ya dini wameeleza uamuzi uliochukuliwa na rais kuwa ni wa haraka sana kudai kuwa kutokana na ugeni wa Kilango,aliyepaswa kuwajibishwa alikuwa ni katibu tawala wa mkoa kwani ndiyo mtendaji mkuu wa mkoa.
Wakizungumza na waandishi wetu kwa nyakati tofauti ,baadhi ya wakazi wa Shinyanga wameeleza kukataa tama ya kupata mkuu wa mkoa mwajibikaji kama Anne Kilango Malecela aliyeonesha upendo kwa wananchi wa mkoa huo mara tu baada ya kuwasili mkoani humo.
Mama Ntilie Wazungumza
Baadhi ya akina mama lishe/ntilie wanaofanya shughuli zao katika soko kuu la Shinyanga walisema kutokana na kuondolewa kwa Mama Kilango hawaamini tena kuwa watapata mkuu wa mkoa mchapakazi kama Kilango.
"Kwa hali ilivyo katika mkoa wa Shinyanga sasa,anatakiwa kiongozi kama Kilango,kwani ni mwanamke jasiri sana,hapa wamepita wakuu wa mikoa 18 wanaume,huyu mama kwa jinsi ninavyomjua,hakika angekimbiza maendeleo ya mkoa huu kwa kasi ya ajabu",alisema Mwanaisha Abdalah.
“Jamani tusifichane,tumepoteza mpiganaji,huyu mama ni jembe kwani tumekuwa tukimuona hata bungeni jinsi anavyopambana,kwanza alionesha upendo kwa wakazi wa Shinyanga,akaitisha hadi mkutano wa hadhara na kuahidi kuwatembelea wananchi walau mara moja kwa wiki ili kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua”,alieleza Halima Shaban,mmoja wa mama lishe hao.
Wakulima Watoa ya Moyoni
Baadhi ya wakulima kutoka kijiji cha Imesela katika wilaya ya Shinyanga walisema walipata mshtuko kusikia mkuu wa mkoa kaenguliwa nafasi hiyo na kudai kuwa rais hajatenda haki kwani ni mgeni mkoani humo waliopaswa kuwajibishwa ni maafisa utumishi na makatibu tawala.
Boda boda wanena
Waendesha bodaboda nao walisema kuwa kilichofanyika ni kuponzwa kwa Kilango na watendaji wa serikali wanaomsaidia katika ofisi.
“Tunamuomba mheshimiwa rais atuonee huruma wanashinyanga kwa kuturidishia kipenzi chetu Kilango,tulikuwa na imani naye ya kutukomboa wananchi,mi nafikiri Pengine mama yetu alikuwa amechanganyikiwa kutokana mme wake Mzee John Malecela kuwa ni mgonjwa hivyo akaamini kila taarifa aliyopewa na katibu tawala wake”,alisema Juma Hatibu.
Hali halisi katika ofisi za mkoa
Uchunguzi tulioufanya umebaini kuwa wafanyakazi wa mkoa wa Shinyanga hawana furaha kutokana na mkuu wao kuondolewa kwa mkuu wao
Baadhi ya wafanya kazi wa ofisi hiyo waliokataa kutajwa majina yao walisema Kilango alionesha upendo kwao baada ya kuwasili mkoani na kuamini kuwa ndiye kiongozi pekee mwenye uwezo wa kumaliza matatizo ya wananchi na hata wafanyakazi kitendo kilichowafanya watoe machozi baada ya kupata taarifa za kuenguliwa kwa mkuu wao.
Akiwasalimia waumini wenzake juzi, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, mjini Shinyanga, baada ya kupewa fursa ya kusema neno, Kilango alisema anamshukuru Mungu kwa kila jambo kwa yote yaliyomtokea.
“Ndugu waumini wenzangu, hili ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu, hata mtu unapojifungua mtoto akafariki dunia, unamshukuru Mungu kwani hayo ni mapenzi ya Mungu.
"Ukiona mzazi wako kafariki dunia pia, unamshuruku Mungu. Tunao wajibu wa kumshukuru Mungu kwa kila jambo,” alisema kwa maneno mafupi na kisha kuketi, huku akiacha simanzi miongoni mwa waumini wenzake, wakiwamo viongozi wa kanisa.
Baadhiya waumini wa kanisa hilo waliozungumza na waandishi wetu walisema uamuzi uliofanywa na mheshimiwa rais yanaumiza kwani wakazi wa Shinyanga walitegemea Kilango kuwa kiongozi wa mfano wakiamini uchapakazi wake utausaidia mkoa kupiga hatua.
"Tunamuomba mheshimiwa rais abadilishe mawazo na kuturudishia mkuu wetu wa mkoa Anne Kilango,tuna imani kubwa na Mama huyu,hatuoni kosa lake,hana kosa aliyepaswa kuondolewa ni katibu tawala kwani ndiyo mtendaji mkuu",walisema waumini hao.