Dodoma. Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeitaka Serikali kuteua bodi za Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Wanyamapori, ambazo zimemaliza muda.
Mbali na kuteua bodi hizo, wameiomba Serikali kutoa fedha zinazotengwa kwa ajili ya wizara kwa wakati, kuiwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Bodi ya Tanapa ilimaliza muda wake mwaka 2014. Tangu wakati huo, Serikali haikuteua bodi nyingine kusimamia utendaji wa mamlaka hiyo.
Akiwasilisha hotuba kwa niaba ya mwenyekiti wa kamati, Atashasta Nditiye, Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi alisema Wizara ya Maliasili na Utalii ina mchango muhimu kwa uchumi wa Taifa, endapo itasimamiwa kikamilifu.
Alisema baadhi ya mashirika na taasisi za umma yamekaa muda mrefu bila kuwa na bodi, hali inayoathiri utekelezaji wa majukumu ya mashirika hayo.
Kapufi alisema kamati inaitaka Serikali kuteua bodi za taasisi hizo, ziweze kufanya kazi kama ilivyopangwa.
Akizungumzia fedha za maendeleo kwa wizara hiyo, mpaka kufikia Machi, mwaka huu, alisema zilizopokewa ni Sh1 bilioni za nje, kati ya Sh7.7 bilioni zilizotengwa kwa ajili hiyo. Alisema fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zilijumuisha Sh5.7 bilioni, fedha za nje na Sh2 bilioni za ndani. Hata hivyo, Serikali haikutoa kiasi chochote kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
“Katika miradi 10 ya maendeleo, hakuna hata mradi mmoja uliotekelezwa kwa ufanisi. Utoaji huu wa fedha za maendeleo ni hatari kwa maendeleo ya sekta hii muhimu,” alisema kaimu mwenyekiti huyo.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Bukombe (CCM), Dotto Buteko ameapa ‘kufa’ na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Magembe kama hatapata majibu kuhusu unyanyasaji unaofanywa na askari wa wanyamapori katika Hifadhi ya Kigosi Moyowosi.
Akichangia hotuba ya wizara hiyo bungeni jana, Buteko alisema asilimia 40 ya ardhi ya Wilaya ya Bukombe ni hifadhi na hakuna uhusiano mzuri na wananchi wa maeneo ya jirani.
Alisema Kijiji cha Iloselo katika Kitongoji cha Mpalala, maofisa hao wamechoma moto myumba 40, wakati kijiji hicho kinatambuliwa na Serikali.
“Watu walipigwa na kuharibiwa mazao yao. Halafu watu wanaendelea kujitapa mtatufanya nini? Nakwambia mheshimiwa waziri, jambo hili lisipopata majibu leo nakufa na wewe,” alisema.
Alisema ni lazima wananchi wa Bukombe wafutwe machozi kwa udhalilishaji waliopata kutoka kwa maofisa hao.
Buteko alisema jumla ya ng’ombe 215 na punda wanne walipigwa risasi na askari ya wanyamapori, na alitaka apewe majibu kwa kitendo hicho. Alisema ng’ombe 603 wametaifishwa na kwamba kwenye kundi hilo la wamiliki watano, watatu walikubali kutoa fedha na wakadanganywa kuwa watapewa ng’ombe wao mahakamani, lakini hawakupewa hadi leo.
Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya alisema hotuba ya waziri wa Maliasili imeonyesha kuwa kuna mapori ya akiba 28 na mapori tengefu 42, lakini ukweli ni kwamba yapo katika vitabu na si halisia.
“Kaliua vijiji 21 vilivyosajiliwa vipo katika mapori ya akiba. Waziri akija hapa kuhitimisha, atueleze nini wanafanya kwa watu hawa ambao wanaishi maisha ya hofu,” alisema.
Mbunge Kasulu Mjini (CCM), Daniel Nsanzugwanko alitaka sheria ya misitu kupitiwa upya kwa sababu imepitwa na wakati.
“Mapori ya akiba yangepitiwa ili mipaka ihuishwe kuepuka migogoro ya kati ya wafugaji na wakulima,” alisema.