.
Hotuba ya Godbless
sakata la mkataba wa Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi jana lilitikisa Bunge wakati msemaji wa kambi ya upinzani, Godbless Lema alipogoma kusoma hotuba ya maoni mbadala ya Wizara ya Mambo ya Ndani kutokana na kutakiwa kuondoa vipengele kadhaa, likiwamo suala hilo.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alikatisha shughuli za chombo hicho jana asubuhi akieleza kuwa kwenye meza za wabunge kulikuwa hotuba ya Kamati ya Bunge pamoja na ya upinzani, lakini ya upinzani ijadiliwe kwanza na Kamati ya Kanuni za Bunge kama inakidhi maudhui ya Bunge.
Baadaye jioni alieleza kuwa baada ya Kamati ya Kanuni za Bunge kupitia hotuba hiyo, imebaini kasoro kadhaa na kupendekeza baadhi ya aya ziondolewe na ndipo alipomruhusu Lema kusoma hotuba hiyo ya maoni mbadala bila ya kujumuisha vipengele hivyo.
“Mheshimiwa mwenyekiti, kwa mwongozo wako huo, maana yake ni kwamba hotuba yangu yote nitakuwa nimeiondoa,” alisema Lema baada ya kusomewa maagizo ya kuondoa aya ambazo Zungu na kamati yake waliona zinakiuka kanuni.
“Basi mimi nishukuru tu kwa mke wangu kufika bungeni na tuendelee na shughuli nyingine.”
Lugumi Enteprises na Jeshi la Polisi walisaini mkataba wa Sh37 bilioni wa kufunga mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole kwenye vituo 108, lakini ilimudu kufunga kwenye vituo 14 tu, wakati ilishapewa asilimia 99 ya fedha hizo kinyume cha mkataba.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga anahusishwa kwenye sakata hilo kwa kuwa anadaiwa kuwa ni mbia kwenye kampuni ya Infosys iliyotakiwa kufunga vifaa hivyo.
Tayari Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) imeunda kamati ndogo kufuatilia suala hilo na kutoa taarifa baada ya wabunge kuhoji sakata hilo na kutaka mkataba huo uwasilishwe PAC.
Akiwa nje ya ukumbi wa Bunge jana, Lema alisema ni lazima waziri Kitwanga ajiuzulu ili uchunguzi wa kamati ndogo ya PAC ufanyike kwa ufanisi.
“Kampuni yake ndiyo iliyofunga vifaa vya LugumI kwenye vituo vya polisi na mimi nina nyaraka ambazo nimepewa na haohao Jeshi la Polisi, nyingi za kutosha. Sasa leo kamati inazunguka kwenye vituo vyote vya polisi wakati IGP alishasema vifaa vyote vilifungwa,” alisema na kuongeza:
“Kwa vile IGP alishasema vifaa vyote vilishafungwa, hiyo kamati inakwenda kumuhoji nani?”
Baada ya kurejea saa 10:00 jioni jana, Zungu alisoma maelekezo yaliyopendekezwa na Kamati ya Kanuni za Bunge kuwa yaondolewe kwenye hotuba hiyo ya upinzani kwa kuwa yanakiuka Kanuni za Bunge.
Zungu alisema baada ya kupitia hati zilizowasilishwa jana, alibaini kuwa taarifa ya upinzani imezungumzia mambo ambayo kwa maoni yake yanakiuka Kanuni za Bunge hivyo aliagiza Kamati ya Kanuni za Bunge ikutane ili kupitia na kujadili maudhui ya hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani bungeni na kumpa mapendekezo.
Zungu alisema kamati hiyo imebaini hotuba hiyo ilikiuka baadhi ya Kanuni za Bunge, hivyo imependekeza maeneo yote ambayo yamekiuka kanuni yarekebishwe.
Alisema maagizo hayo ni kuondoa kipengele kinachozungumzia mauaji ya viongozi wa kisiasa na maeneo yote yaliyoendana na kipengele hicho kuanzia ukurasa wa saba hadi wa tisa.
“Kwa eneo linalozungumzia mkataba tata wa Lugumi na Jeshi la Polisi, kamati inapendekeza maneno yote yanayoanzia ukurasa wa 10, aya ya nne hadi ukurasa wa 14 aya ya kwanza, yaondolewe,” alisema Zungu.
Alisema eneo jingine la kuondoa ni maneno yanayomhusu Rais John Magufuli katika sakata la uuzwaji wa nyumba za Serikali ambalo lilikuwa ukurasa wa 15, aya ya kwanza hadi ya tatu, badala yake kuweka neno “Serikali”.
Nyumba hizo ziliuzwa na Serikali ya Awamu ya Tatu wakati Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi.
Zungu alisema kipengele kinachohusu rushwa na Bunge kutumika kulinda wahalifu, kiondolewe kuanzia ukurasa wa 15 hadi 17 kwani kinakiuka masharti ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
Pia, alisema kamati ilipendekeza kuondolewa kwa maneno yote yaliyoko kuanzia ukurasa wa 19 hadi 20 kwenye eneo linalohusu tabia ya Rais Magufuli na usalama wa nchi kwa kuwa yanakiuka kanuni.
“Baada ya kupitia maoni na ushauri wa kamati, naomba kutoa mapendekezo yafuatayo. Kwa kuzingatia masharti ya Kanuni ya 64(1) ambayo imekataza kuzungumzia jambo lolote ambalo linasubiri uamuzi wa Mahakama, kutotumia jina la Rais kwa dhihaka, kutozungumzia mwenendo wa Rais, kutosema vibaya au kutoa lugha ya matusi kwa mbunge yoyote.
“Baada ya kutafakari na kuzingatia maamuzi mbalimbali ya Spika na kuzingatia masharti ya Kanuni ya 64, namwelekeza msemaji wa kambi ya upinzani bungeni, aondoe maneno yote hapo juu,” alisema Zungu na kumwita Lema ili asome maoni mbadala, lakini akakataa.
Kutokana na msimamo huo wa Lema, Zungu aliruhusu majadala uendeleee na wabunge wakaendelea kuchangia hotuba hiyo.
Wakati akichangia, Lema alianza tena kuzungumzia suala la Lugumi, akimhusisha Waziri Kitwanga na kampuni ya Infosys, jambo ambalo Zungu alilizuia tena akisema tayari mambo hayo yameshapigwa marufuku.
Lema alikubali na kuahidi kuyaepuka masuala hayo huku akionya siasa zisifanyike bungeni kwa kuzuia mambo muhimu kuzungumzwa kwa kuwa hakuisaidii serikali yoyote.
Lema alimwambia Kitwanga ajibu hotuba yake na kwamba anayetafutwa si Lugumi, bali waziri mwenyewe ambaye alidai ana urafiki na Rais Magufuli, kauli ambayo ilimfanya Zungu amkatishe tena kwa kuwa ameshakatazwa kutumia jina hilo bungeni.
Zungu alimkatisha tena Lema na kumtaka ajikite katika mjadala bila kugusa watu, jambo lililomfanya ajiulize atazungumzia nini zaidi, huku akishangiliwa na wabunge wa kambi ya upinzani.
Kutokana na hali hiyo, Lema alisema ameanza kumkumbuka Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwa kuwa alisemwa sana, lakini hakuwahi kuliingilia Bunge hata siku moja.
Jaribio la kuzungumzia sakata la Lugumi pia lilifanywa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba lakini naye alizuiwa na mwenyekiti.
Nje ya ukumbi, Mbunge wa Bunda (Chadema), Ester Bulaya alisema si vizuri kwa hotuba ya maoni mbadala kutosomwa kwa sababu ya kumlinda mtu mmoja.
“Kama kweli Mheshimiwa Rais hana hana upendeleo, angemwambia Waziri Kitwanga resign (jiuzulu) ili isitie doa hizo jitihada ambazo yeye anasema anazifanya kwa masilahi ya Watanzania,” alisema Bulaya, mmoja wa wabunge wanaochangia hoja bila ya woga tangu alipokuwa CCM.
“Leo hii waziri anapewa tenda kwenye wizara anayoiongoza, halafu tutegemee kuna haki itatendeka? Yaani kumlinda mtu mmoja eti ndiyo kunafanya kambi rasmi ya upinzani, ishindwe kutoa maoni mbadala?
Bajeti ya Mambo ya Ndani
Awali, akisoma hotuba ya makadirio na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Waziri Kitwanga aliomba Sh864 bilioni kwa shughuli za wizara hiyo kwa mwaka 2016/17, lakini hakuzungumzia sakata la Lugumi na Jeshi la Polisi.
Alipohojiwa na waandishi wa habari nje ya ukumbi kuhusu sababu za kutolijumuisha, alisema kuwa hakulizungumzia kwa sababu ni suala ya kiutendaji na liko sawa.
Pamoja na Kitwanga kutozungumzia suala hilo, Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ililigusia.
Mwenyekiti wake, Balozi Adadi Rajabu alisema matarajio ya wengi ni kusikia kamati yake inazungumzia mitambo ya kuchukulia alama za vidole iliyoagizwa na Jeshi la Polisi.
“Naomba kulijulisha Bunge hili kuwa kamati inatambua uzito na umuhimu wa suala hili. Hata hivyo, kwa kuwa suala hilo ni hoja iliyoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Bunge limeipa jukumu Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika wizara za Serikali yaliyoainishwa katika taarifa ya CAG, hivyo basi ni vyema PAC ikaachwa iendelee kushughulikia hoja ya CAG,” alisema Balozi Rajabu.
Awali, kabla ya agizo hilo la kuondoa maneno hayo kwenye hotuba ya Lema, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa aliomba mwongozo akieleza kuwa kambi ya upinzani huandaa hotuba kama kambi hivyo haiwezekani wakapangiwa nani wa kwenda kwenye kamati na kama kuna udhaifu basi Serikali ijibu.
Akijibu hilo, Zungu alisema ndiyo maana amemtaka msemaji wa kambi hiyo pamoja na kiongozi wa kambi ya upinzani kukutana na Kamati ya Kanuni za Bunge kujadili suala hilo.
Zungu aliagiza tena Kamati ya Kanuni za Bunge na wajumbe wote wakutane na Lema ambaye ndiye msemaji wa kambi hiyo kwa Wizara ya Mambo ya Ndani na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe ambaye awali hakuwapo na kuwakilishwa na Mchungaji Msigwa.