Charles ambaye ni Diwani wa Chadema Kata ya Vijibweni Manispaa ya Temeke, alimshinda mpinzani wake kwa kupata kura 84 dhidi ya kura 67 alizopata mgombea wa CCM, Yenga Omary.
Uchaguzi huo ulifanyika baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuamuru uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, kufanyika jana kama ilivyopangwa.
Uchaguzi huo ulifanyika katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, na kwa mara ya kwanza tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa uanze nchini mwaka 1992, Jiji la Dar es Salaam litakuwa chini ya Upinzani.
Uchaguzi huo ulianza saa 4:37 asubuhi baada ya akidi ya wapiga kura kutimia ambapo wajumbe waliokwisha kufika hadi muda huo walikuwa 158 kati ya wajumbe 163 waliopaswa kushiriki kupiga kura.
Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando ndiye alifungua kwa kuwataka wajumbe kuwa watulivu katika muda wote wa uchaguzi huo ili kufanikisha kazi hiyo ambayo ilikwama kwa muda mrefu.
Baada ya ufunguzi huo aliwakaribisha wajumbe mmoja mmoja kujinadi kwa wapiga kura, akianza mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yenga Omary aliyeahidi kuwatumikia wananchi wote bila kujali itikadi za vyama.
Mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyeungwa mkono na Ukawa, Charles aliyetaja vipaumbele vyake viwili vya kuanza navyo kazi endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo, akiahidi kutafuta utatuzi wa tatizo la uhaba wa madawati katika shule nyingi za msingi na kutatua kero ya foleni jijini Dar es Salaam.
Awali uliandaliwa utaratibu wa kupiga kura kwa kutumia namba zilizogawiwa kwa wapiga kura wote, lakini Chadema ilipinga matumizi ya namba na kutaka kutumia majina kwa kwenda kupiga kura, utaratibu uliokubalika.
Ilipotimu saa 5:20 wajumbe walianza kupiga kura kwa utaratibu wa kuita majina kwa kuanzia na Manispaa ya Ilala, ikafuatia Manispaa ya Kinondoni kisha kumalizia na Manispaa ya Temeke.
Baada ya kumalizika kwa upigaji kura, kazi ya kuhesabu kura lilianza na mgombea wa CCM alienda kusimamia kura zake mwenyewe huku wa Chadema akisimamiwa na Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sarah Yohana alisimama na kuanza kutangaza matokeo hayo kwa kueleza kuwa waliopiga kura ni 158 na kura halali zilikuwa 151 na kura saba ziliharibika.
“Idadi ya waliopiga kura ni 158, kura zilizoharibika ni kura saba, kura halali 151. Mgombea Yenga Omary amepata kura 67 na mgombea Isaya Charles amepata kura 84,” alisema Yohana.
Meya huyo mpya wa Jiji la Dar es Salaam, Charles aliwashukuru wajumbe wote kwa kumwamini na kumpa nafasi hiyo huku akiahidi kufanya kazi na makundi yote.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi huo, Diwani wa Kata ya Mwananyamala, Songoro Mnyonge alisema demokrasia imefuata mkondo wake na sasa kilichobaki ni kufanya kazi.
Aliyekuwa mgombea wa Urais kupitia Chadema aliyeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa alisema anashukuru kwa demokrasia kuheshimiwa na kumtaka Meya huyo mpya wa jiji kufanya kazi kwa bidii. Uchaguzi huo ulihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa na mawaziri ambao pia walikuwa ni wapiga kura katika uchaguzi huo.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria na kupiga kura ni Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk Augustine Mahiga na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.
Upande wa wanasiasa wa upinzani ni Mwenyekiti wa Chadema, na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji na wengineo.