Akizungumza na gazeti hili kwa simu, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk Rehema Nchimbi alisema, ibada ya kumuaga rasmi ilifanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) lililopo mkoani humo.
“Tumemuaga na safari ya kwenda Dar es Salaam itaanza muda mfupi kuanzia sasa (jana jioni), tutasafiri usiku mzima tunatarajia kuingia Dar es Salaam kesho (leo) asubuhi tayari kwa mazishi,” alisema Dk Nchimbi.
Kwa mujibu wa taarifa ya ndani ya familia, mwili wa Dumba unatarajiwa kuwasili saa 4:00 asubuhi na taratibu za mazishi zitafanywa nyumbani kwa baba yake, Mzee Dumba eneo la Kigamboni Midizini.
Baada ya chakula itafanyika ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Magogoni lililopo Kigamboni na maziko yatafanyika kwenye makaburi ya Magogoni. Wakati huo huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametuma salamu za rambirambi kwa wanahabari wote kutokana na kifo cha ghafla cha mkuu huyo wa wilaya ambaye pia alikuwa ni Mtangazaji Mwandamizi wa zamani wa Redio Tanzania (RTD), Dar es Salaam.
“Pokeeni salamu zangu za rambirambi za dhati kwa kuondokewa na mwanahabari mahiri Dumba aliyekuwa mfano wa kuigwa. Mbali na utangazaji wake mahiri, alikuwa mzalendo wa kweli aliyetumikia tasnia hii ya Habari na Serikali kwa uadilifu na upendo wa kweli, tutamkumbuka na tutaukosa mchango wake,” alisema Nape.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Elisante ole Gabriel alituma salamu za pole na kuwatakia moyo wa subira na uvumilivu ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu. Baadhi ya wafanyakazi waliowahi kufanya kazi naye walisema, kifo chake ni pigo na pengo lisiloweza kuzibika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Halima Kihemba akizungumzia uhusiano wake na Dumba, alisema yeye alianza kazi RTD mwaka 1971 na kumkuta Dumba akiwa tayari kazini hivyo walifanya naye kazi kwenye Idhaa ya Kiingereza ya External Services wakati Dumba akiwa msaidizi wake.