Mkazi wa Gongo la Mboto, Omary Hamis (25) amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa miaka tisa ambaye ni mlemavu wa kusikia na kuongea.
Hakimu Mkazi, Flora Haule wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi wa mashahidi tisa ukiwamo wa daktari na fomu namba tatu ya polisi (PF3), iliyotolewa mahakamani hapo kama kielelezo dhidi ya mshtakiwa huyo.
“Mahakama imekukuta na hatia hivyo inakuhukumu kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na kosa la kumlawiti mvulana wa miaka tisa ambaye ni mlemavu wa kusikia na kuzungumza, ili iwe fundisho kwa jamii,” alisema hakimu Haule.
Katika ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, ilidaiwa kuwa mtoto huyo siku ya tukio alifika kwenye banda la kuonyeshea video ambalo linamilikiwa na Hamisi saa za jioni, kwa ajili ya kuangalia video, lakini Hamis alimfukuza kutokana na kutokuwa na pesa ya kiingilio.
Baada ya kumfukuza mtoto huyo aliondoka, lakini baadaye alirudi bila ya Hamis kuwa na taarifa akakaa ndani ya banda na kisha kupitiwa na usingizi uliosababisha abaki kwenye banda hilo peke yake hadi usiku.
Hamis alitumia mwanya huo kumlawiti mtoto huyo kwenye jumba bovu lililopo jirani na ofisi yake hiyo.
Mashahidi waliieleza mahakama kuwa walisikia sauti ya mtu ambayo ilikuwa haisikiki vizuri akiomba msaada, ndipo waliposogea na kumkuta Hamis akitekeleza kitendi hicho huku akijua kuwa ni kosa kisheria.
Mashahidi walidai hata walipomkaribia, Hamis aliendelea kutekeleza kitendo hicho hadi walipolazimika kumpiga mateke. Hamis alikiri kuwa siku hiyo watoto walifika kwenye banda lake hilo.
Wakili wa Serikali, Ester Kyara aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa wote wanaotumia mabanda ya kuonyesha video kufanya ukatili kwa watoto.
Katika utetezi wake, Hamisi alisema ana familia inayomtegemea hivyo apunguziwe adhabu, maombi ambayo yalitupiliwa mbali na mahakama hiyo na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Hamisi anadaiwa kutenda kosa hilo Agost 26, 2014 eneo la Gongo la Mboto.