Kondakta wa daladala, Hamim Seif (42) mkazi wa Mwananyamala 
Ujiji, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu 
akikabiliwa na shtaka la kutishia kumuua Rais John Magufuli kwa maneno. 
Seif
 alipandishwa kizimbani mahakamani hapo jana mchana na kusomewa shtaka 
hilo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kenneth Sekwao. 
Mshtakiwa
 huyo alikana shtaka hilo na Hakimu Mkazi, Hellen Liwa alisema kuwa 
dhamana ya mshtakiwa huyo iko wazi na alitakiwa kuwa na wadhamini 
wawili, kutoka taasisi ya Serikali inayotambulika, ambaye atasaini hati 
ya dhamana ya Sh2 milioni. 
Licha ya dhamana yake hiyo kuwa wazi,
 mshtakiwa huyo alishindwa kukamilisha masharti hayo kwani baada ya 
kusomewa mashtaka alipoulizwa kama alikuwa na wadhamini alishindwa 
kuwapata. 
Akimsomea shtaka linalomkabili, Wakili Sekwao alisema 
kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Machi 10 mwaka huu katika baa ya 
Soweto, Makumbusho wilayani Kinondoni kinyume cha kifungu cha 89 (2) (a)
 na kifungu cha 35 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu. 
Wakili Sekwao
 alisema akiwa katika baa hiyo, mshtakiwa alitishia kumuua Rais wa 
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli kwa maneno kwa njia ya
 kujitoa mhanga. 
“Kwa haya mambo anayoyafanya Rais Magufuli, 
mimi nimo tayari kujilipua kwa kujitoa mhanga ili kumuangamiza,” alisema
 Wakili Sekwao akimnukuu mshtakiwa huyo. 
