Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta) limepinga mpango wa 
Rais John Magufuli wa kukata malipo ya mishahara ya watumishi wa umma 
kutoka Sh40 milioni kwa mwezi hadi Sh15 milioni. 
Akizungumza na 
viongozi wa vyama vya wafanyakazi Kanda ya Ziwa jijini Mwanza jana, Naibu 
Katibu Mkuu wa Tucta, Hezron Kaaya alisema uamuzi huo ni kinyume na 
sheria na utaligharimu Taifa iwapo wahusika wataamua kwenda mahakamani 
kupinga mishahara yao kupunguzwa. 
“Watendaji hawa hawakujipangia 
mishahara wao wenyewe, bali malipo haya yalipangwa na bodi za mashirika 
na taasisi husika ambazo kisheria zimepewa mamlaka hayo. Malipo haya 
hayawezi kupunguzwa kwa kauli za kisiasa bila kuzingatia mahitaji ya 
kisheria,” alisema. 
“Iwapo Serikali itatekeleza lengo hili bila 
kuwapo mjadala mpana na makubaliano ya kisheria kati ya wahusika, basi 
ijiandae kulipa mamilioni ya fedha kama fidia iwapo watakaokatwa 
mishahara yao watakwenda mahakamani.” 
Akiwa mjini Chato wakati 
wa mapumziko ya wiki moja, Rais Magufuli alitangaza kupunguza mishahara 
ya juu kutoka Sh40 milioni hadi Sh15 milioni kwa mwezi, akisema wapo 
watumishi wa umma wanalipwa masilahi manono na kuishi kama wako peponi, 
huku wanaolipwa Sh300,000 wakiishi kama wako jehanamu. 
Kaaya 
aliishauri Serikali kuendelea kuwalipa mishahara hiyo minono wahusika 
hadi mwisho wa mikataba yao, ndipo lengo la kuipunguza litekelezwe ama 
kwa kuwapa wahusika mikataba mipya au kuajiri watu wengine. 
“Serikali
 inaweza kuwa na nia njema kupunguza tofauti kubwa ya mishahara kati ya 
kada ya juu na chini, lakini utekelezaji wake lazima usubiri muda 
mwafaka mikataba ya sasa itakapomalizika,” alisisitiza. 
Katika 
hatua nyingine; Tucta imepinga hatua zinazochukuliwa na baadhi ya 
mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya ya kutangaza kuwasimamisha kazi 
watumishi wa umma ambao hawapo chini ya mamlaka zao kinidhamu. 
Source;mpekuzi 
