Waziri wa nchi ofisi ya Rais (utawala bora) Bi.Angela Kairuki
SAKATA la mishahara hewa iliyokuwa ikiigharimu Serikali zaidi ya Sh
bilioni 1.8 kila mwaka, limechukua sura mpya baada ya mishahara hiyo
kubainika kuwepo karibu katika kila kona ya nchi.
Mbali na kusababisha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne
Kilango kusimamishwa kazi kabla hata ya kumaliza mwezi tangu aanze
kutumikia cheo hicho, sasa watumishi walionufaika na mishahara hiyo
wameanza kushikwa na kufikishwa mahakamani.
Jana, Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Imani Abdul,
maarufu kwa jina la Nyamangaro (44), alipandishwa kizimbani katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, akikabiliwa na makosa ya wizi wa
mishahara ya watumishi hewa inayofikia Sh milioni 29.4.
Mishahara ya 2013
Wakili wa Serikali, Michael Ng’hoboko alidai mbele ya Hakimu wa
mahakama hiyo, Joyce Minde, kuwa kati ya Aprili 29, 2013 na Machi 27,
2014, mshitakiwa aliiba Sh milioni 29.4 huku akijua wazi kuwa kitendo
hicho ni kinyume na sheria.
Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa mshitakiwa alikuwa akijipatia
mishahara hiyo ambayo wahusika walishastaafu kazi muda mrefu kupitia
akaunti yake namba 50802503513, iliyoko Benki ya NMB, tawi la mjini
Singida.
Hata hivyo, mshitakiwa alikana kutenda makosa hayo na kesi yake
imeahirishwa hadi Aprili 27 mwaka huu itakapotajwa tena. Mshitakiwa
alitakiwa kutoa Sh milioni 14.7 taslimu ya dhamana mahakamani au awe na
mali isiyohamishika yenye thamani inayolingana na kiasi hicho cha fedha.
Taarifa zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni zinaonesha kwamba
mshitakiwa hakufanikiwa kupata fedha hizo na kurudishwa rumande.
Idadi yao
Uhakiki uliofanywa na serikali kuhusu tatizo la wafanyakazi hewa
nchini, mpaka sasa umebaini wafanyakazi hewa 1,680 waliokuwa wakilipwa
mabilioni hayo ya fedha. Uhakiki unaendelea na wafanyakazi hewa zaidi
wanaendelea kugunduliwa.
Kutokana na changamoto hiyo, Machi 15 mwaka huu wakati Rais John
Magufuli akiwaapisha wakuu wa mikoa, alitoa siku 15 kwa viongozi hao
kuhakikisha wanajumuisha wafanyakazi wote na kuwaondoa watumishi hewa.
Alipokwenda Chato mkoani Geita, Rais Magufuli alitolea mfano wa
mfanyakazi mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambaye alikuwa
akilipwa mishahara ya watu 17 na kueleza kuwa mfanyakazi huyo
atafikishwa mahakamani.
Rais Magufuli pia alisema Serikali yake imejiandaa kuboresha maslahi
ya wafanyakazi kwa kupunguza kodi kutoka asilimia 11 ya sasa hadi
asilimia 10 au 9 kuanzia bajeti ijayo.
Saturday, April 16, 2016
Wanufaika mishahara hewa waanza kubanwa
Published Under
KITAIFA
About Author
BLOG NAMBA MMOJA KWA MATANGAZO YA AJIRA NA NAFASI ZA KAZI TANZANIA. Soma zaidi