Kuanzia sasa wateule wengi wa Rais John Magufuli serikalini watakuwa vijana kwa kuwa amegundua wengi hawapendi rushwa, amesema.
Aidha, Rais Magufuli amesema anafahamu kwamba vijana hawapendwi lakini amegundua ndio wachapakazi ambao watasaidia kulipeleka taifa katika maendeleo anayoyatamani.
Rais Magufuli alisema hayo jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa makandarasi wa mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Dodoma, jijini.
“Nimegundua vijana wengi hawapendi rushwa, hivyo nitaongeza vijana kila nikiteua kwa kuwa niliowaweka naona matunda ya kazi zao," alisema na kuongeza kuwa: “Najua watu wanawachukia sana ila nitawaongeza.
“Palipo na vijana nimeona mambo yanaenda na kuna mabadiliko. Wazee ndio tumelifikisha taifa hili hapa. Hakuna asiyejua kuwa Tanzania ilichakaa kila mahala.”
Tangu aingie Ikulu Novemba 5, mwaka jana, Rais Magufuli amejipambanua kama mwenye kupiga vita wizi, rushwa, ufisadi, ukwepaji kodi, uzembe na ukosefu wa maadili wa watumishi wa umma.
Aidha, Rais Magufuli alisema idadi ya watumishi hewa imefikia 10,292 huku vijana wengi wenye ujuzi wanamaliza vyuo vikuu na kukosa ajira. Alisema kama si tatizo la uwapo wa watumishi hewa, ajira zipo kwa wingi.
“Nataka vijana ili twende kwa kasi, ndiyo njia pekee ya kufikia maendeleo tunayoyatarajia,” alisemna.
Rais pia alizungumzia uamuzi wake wa juzi wa kuvunja Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kutengua uteuzi wa aliyekuwa mwenyekiti wake, Profesa Awadhi Mawenya.
Rais Magufuli alisema zaidi ya Sh. bilioni 87 zililipa mikopo hewa kwa wanafunzi 480 wenye daraja la nne kidato cha nne, huku ikiaminika mikopo ni kwa ajili ya watoto wa masikini.
“Unashangaa anayesimamia kitengo ni Profesa. Hapa ndiko nchi ilikofikia,”alisema.
Rais Magufuli alitoa mfano mwingine wa Meli kubwa 65 za makontena zilizotia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam bila kuandikwa, ambazo alisema “hazijulikani zilielekea wapi na hazikulipwa.”
Baada ya Rais Magufuli kumaliza hotuba yake, alimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (34) kuwasalimia wajumbe wa mkutano huo.
Makonda alisema alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, aliunda kamati ndogo ya kufuatilia barabara na kubaini zaidi ya Sh. bilioni 2.2 zilitumika kujenga barabara ambazo mvua ikinyesha hazipitiki.
Alisema pia walibaini barabara zilizokuwa zikarabatiwe kwa Sh. milioni 200, zilitengewa Sh. bilioni moja kwa kila barabara na baadaye ziliombwa zaidi ya Sh. bilioni 5.9 na zilikuwa katika mchakato wa kulipwa lakini alizizuia.
“Manispaa ya Kinondoni ni tatizo kubwa...unakuta wananchi wanalia shida, wao wanalia kwa uongo kwa kuwa wanajua kuna fedha wanapata kama hizo.
“Nashukuru Mfuko wa Barabara umewanyima fedha na wameambiwa watengeneze barabara za awali hadi zikamilike kwa kutumia mapato yao ya ndani,” alisema.
Mbali na nafasi kadhaa za Wakuu wa Wilaya ambako habari za uhakika zinasema wengi watabadilishwa, Rais Magufuli pia ana nafasi ya uteuzi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, baada ya kuteungua uteuzi wa Charles Kitwanga kwa sababu ya ulevi, Ijumaa iliyopita.
Aidha, Rais Magufuli hajateua Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga tangu atengue uteuzi wa Anne Kilango Malecela kwa kutoa taarifa ya uongo kuwa mkoa wake haukuwa na watumishi hewa Aprili, mwaka huu.
Rais Magufuli pia hajafikisha jumla ya Wabunge 10 anaoruhusiwa kuwateua kwa mujibu wa katiba, hivyo kuweka uwezekano wa kuwapo kwa vijana wengi zaidi serikalini kwa mara ya kwanza katika miaka 55 ya Uhuru.