Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha Tanzania Labour Party ( TLP), Augustino Mrema amelaani hatua ya Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif kutangaza kumwondoa Rais wa Zanzibar, Dr Shein madarakani kabla ya 2020 huku akiwataka wazanzibar kutoyumbishwa na kauli za mwanasiasa huyo.
Mrema amezungumza hayo leo jijini Dar es salaam mbele ya waandishi wa habari na kusema kwamba amani ya Zanzibar ni muhimu kuliko maslahi binafsi hivyo ni vyema kuzitafakari kauli ambazo zinaweza kuleta machafuko.
Amesema hakuna mtu aliye juu ya sheria hivyo kuwepo kwa watu wanaochochea vurugu ni kama waahini pia ni vyema hatua zichukuliwe dhidi yao katika kuhakikisha wananchi wanakuwa salama
Aidha Mrema amesema kwamba amani ya Zanzibar ikiharibika hata bara haiwezi kuwa salama hivyo ni vyema kauli za kuvuruga amani zizingatiwe ili kulinda maslahi ya wananchi wa pande zote mbili.
Amesema Zanzibar ina historia ya kuuawa watu mwaka 2001 kutokana na vurugu za kisiasa hivyo lazma kwa sasa suala la ki uchochezi liangaliwe kwa macho mawili dhidi ya watu wanaotaka kuvuruga amani katika mazingira hayo.
Mrema amesisitiza hakuna chama cha siasa ambacho kinajengwa kwa kususia uchaguzi bali kwa kufanya hivyo ni kuwanyima wapiga kura haki pia ni hatari na kunaweza kusababisha chama kusambaratika kama kulivyotokea kwa baadhi ya vyama mfano, UPC cha Uganda na vinginevyo.
Pamoja na hayo mrema amefafanua kwamba mahakama ya ICC haingalii tu viongozi wa serikali bali hata viongozi wa kisiasa ambao wamesababisha mauaji kutokana na kauli wanazozitoa.
Pia mwenyekiti huyo wa TLP amewataka wahisani kutoingilia mambo ya ndani ya nchi kwani kusitisha misaada kwa hoja ya kufutwa uchaguzi wa Zanzibar na sheria ya mitandao ni kuingilia uhuru wa watanzania.