Kulwa Alfre alivyobabuka mgongo.
MWANZA: Kweli hujafa hujaumbika! Mwanamama Kulwa Alfred (37), mkazi wa Pasiansi jijini hapa amelala kitandani kwa takribani siku 547 ambazo ni sawa na mwaka mmoja na nusu akisumbuliwa na matatizo ya miguu kiasi cha kumsababishia eneo kubwa la mwili wake kubabuka.
Akisimulia kwa majonzi, jirani wa Kulwa ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, aliliambia Amani kwamba, Kulwa alianza kusumbuliwa na miguu kuvimba, wakati mwingine kukosa nguvu ambapo haikujulikana tatizo linalomsumbua.
“Miguu ilikosa nguvu, walijitokeza ndugu zake na kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza kwa matibabu lakini kutokana na matibabu kuchukua muda mrefu, wale ndugu wakamwacha pale.
“Ikabidi watu wa hospitali watafute njia nyingine ya kumrudisha kwake ambapo walipomfikisha waliwaomba watu waliokuwepo hapo wamsaidie kufanya mazoezi,” alisema jirani huyo.
Aliongeza, Kulwa anaishi na watoto wake watatu na wa kwanza mwenye miaka 12 anasumbuliwa na matatizo ya kutosikia kutokana na kupata ajali ya pikipiki, wa pili ana miaka nane, wa mwisho miaka mitano.
Akipatiwa huduma
“Hakukuwa na mtu aliyejitokeza kumsaidia Kulwa, mumewe alishaondoka tangu kuanza kwa matatizo hivyo aliporudishwa nyumbani akitokea hospitali, alikuwa ni mtu wa kujiburuza kwa kufanya mazoezi.
“Ilifika kipindi hakuweza tena kujiburuza, akawa ni mtu wa kukaa kitandani huku huduma zote akizipatia kitandani ikiwa ni pamoja na kujisaidia haja zote. Kwa kuwa, watoto wake walikuwa wadogo alikosa huduma na hivyo kusaidiwa na mwenyekiti wake wa mtaa (hakumtaja jina).”
Kwa sasa wasamaria wema wamejitokeza na kumfikisha kwa mara nyingine Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza kupatiwa matibabu ambapo bado hali yake hairidhishi na anahitaji misaada zaidi.
Kama umeguswa na yaliyompata Kulwa, unaweza kumchangia kwa namba; 0759 665 555.
Kwa maelezo zaidi angalia Kipindi cha Nitetee Sauti ya Mnyonge kesho saa 3 usiku kwenye Runinga ya Channel Ten.