KIFO ni fumbo kubwa katika maisha ya mwanadamu kwani huwa hakijulikana siku wala saa kitakapotokea. Wapo mastaa ambao enzi za uhai wao walijikuta wakiimba au kufanya mambo yenye maneno yaliyoashiria kuwa walikiona kifo chao kwamba kiko karibu. Katika makala haya tunakuletea orodha ya mastaa mbalimbali wa hapa nchini na nje ya nchi ambao wamefariki dunia muda mfupi au siku chache baada ya kufanya kazi zilizozungumzia kifo au maisha baada ya kifo.
STEVEN KANUMBA
Huyu alikuwa ndiye kinara wa filamu Bongo lakini kabla ya mauti kumfika mwaka 2012, alipata kutoa kazi yake iliyoitwa Ndoa Yangu ambayo simulizi yake ni kama alijitabiria kifo chake.
Licha ya filamu hiyo, Steven Kanumba ambaye alifariki baada ya kudondoka chumbani kwake, aliimba wimbo uitwao Nitayainua Macho Yangu ambao ulichezwa na redio nyingi baada ya kifo chake, ulikuwa ukizungumzia maisha baada ya kuondoka duniani.
ANGELA CHIBALONZA
Mwanamama huyu ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), aliyeishi yeye na familia yake jijini Nairobi nchini Kenya, alifariki kwa ajali ya gari katika Barabara ya Naivasha. Kabla ya kufikwa na umauti, mwimbaji huyu alikuwa ameshatoa nyimbo nyingi ikiwemo ile inayozungumzia maisha ya peponi ambayo inakwenda kwa jina la ‘Kutoka Chini’.
FANUEL SEDEKIA
Mwimbaji huyu wa nyimbo za Injili alifariki dunia mwaka 2009 katika Hospitali ya Poriya Tiberia iliyopo nchini Israel baada ya kuugua kwa muda mfupi ugonjwa wa kisukari. Alikuwa amekwenda huko kwa ajili ya maombi. Siku chache kabla ya kifo mwanamuziki huyu alitoa wimbo uliokwenda kwa jina la Safari ya Imani ambayo ndani yake kuna maneno yanayoelezea safari ya kuelekea peponi.
JOHN KOMANYA
Mchungaji huyu wa Kanisa la Cathedral of Joy International Tanzania, ambaye alikuwa pia ni mwimbaji wa nyimbo za Injili alifariki dunia mwaka 2015 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu kutokana na kusumbuliwa na tatizo la mishipa inayopeleka oksijeni kwenye ubongo kufeli. Kabla ya kupatwa na umauti, Komanya aliimba Wimbo wa Bwana Niinue ambao pia unazungumzia maisha baada ya kifo hali ambayo ilichukuliwa kama alikiona kifo chake.
GATARE EPHRAIM, AMOS PHARASI, PHILBERT MANZI
Hawa ni wanamuziki watatu wa kundi maarufu la Kwaya nchini Rwanda la Ambassador Of Christ ambao walifariki baada ya kupata ajali ya gari. Kabla ya hapo, kundi hilo liliimba wimbo maarufu, wa Kwetu Pazuri ambao unazungumzia maisha ya mbinguni.
Zipo simulizi zinazosema, wakiwa njiani, Gatare aliyekuwa kiongozi, aliwaambia wenzake, “Nyote mlio katika gari hili, lazima mjue kila mtu ana jukumu la kuongoza kundi hili hata kama kesho mimi sitakuwepo” wakati Amos naye alisema “Kazi niliyotumwa kufanya katika kundi hili nimemaliza, imebaki kwenu kuiendeleza.”
Naye Philbert alisema “dada nakuomba msamaha, hata kama wewe ndo umenikosea, nami jinsi nilivyopokea, naweza kuwa nimekukosea pia.” Dakika kumi baada ya kauli hizo, gari lililowabeba wanakwaya hao liligongana na lori katika Kijiji cha Tinde, Kahama mkoani Shinyanga na watatu hao walifariki dunia hapohapo.
ORIDA NJOLE
Ni mwimbaji wa nyimbo za Injili ambaye alifariki dunia mwaka 2014 katika Hospitali ya Temeke kutokana na tatizo la kuishiwa damu. Orida kabla ya kufariki dunia alitoa albamu iliyokwenda kwa jina la Duniani Tu Wapitaji ambapo alizungumzia kuhusu kifo na maisha baada ya haya ya duniani.