Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watu wengine wawili, akiwamo mpenzi wa mfanyakazi wa ndani wa Anathe Msuya, aliyeuawa kwa kuchinjwa nyumbani kwake.
Anathe, ambaye ni dada wa Bilionea Erasto Msuya, aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana Mei 26 nyumbani kwake Kibada, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Wauaji hao hawakuchukua chochote kwenye nyumba hiyo. Bilionea Msuya aliuawa Agosti mwaka jana kwa kupigwa risasi na tayari watu 12 wamekatwa, wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo.
Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema hadi sasa wamekamata watuhumiwa wanne wakihusishwa na mauaji ya dada wa bilionea huyo.
Kati ya watuhumiwa waliokamatwa, yumo mume wa Aneth, msaidizi wa ndani wa Anathe na mtuhumiwa mwingine ambaye Kamanda Sirro hakumtaja jina.
“Mwanzo tulimkamata mume wa marehemu na msaidizi wa ndani wa marehemu, lakini sasa wameongezeka wengine wawili, akiwamo hawara wa msaidizi wa ndani. Tunaendelea kuwahoji na upelelezi ukikamilika tutawafikisha mahakamani,” alisema Sirro.
Kwa mujibu wa mama mdogo wa marehemu, Lilian Benjamin, msaidizi wa ndani wa dada wa bilionea huyo aliondoka saa sita mchana na kuacha funguo nyumba ya jirani.
Lilian alisema msaidizi huyo alimpigia simu ghafla bosi wake mchana na kumwambia anaondoka na hataendelea na kazi.
Mauaji ya Aneth ni mwendelezo wa mauaji yanayoikumba familia hiyo ya Msuya baada ya kaka yake, Erasto ambaye alikuwa ni mfanyabiashara tajiri wa madini, kuuawa Agosti 7, 2013 kwa kupigwa risasi zaidi ya 12 kwa kutumia bunduki ya SMG katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.
Februari 10, mawakili wanaosimamia kesi ya Erasto, Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emanuel Safari na John Lundu, waliiambia mahakama kuwa Serikali inakusudia kuita mashahidi 50 kuthibitisha shtaka hilo na kuwasilisha vielelezo 40, ikiwamo bunduki hiyo.
Mawakili hao walidai mipango ya kumuua bilionea Msuya ilianza Julai 26,2013 jijini Arusha, ikiwahusisha washtakiwa na waliotekeleza mauaji hayo wangelipwa Sh5 milioni kila mmoja.
Wakitoa maelezo ya tukio hilo, mawakili hao waliiambia mahakama kuwa washiriki ambao wasingeenda moja kwa moja kwenye mauaji, wao wangelipwa Sh3 milioni kila mmoja.
Mshtakiwa wa kwanza, Shariff Mohamed anadaiwa kuwa ndiye alikuwa mpangaji mkuu na alitoa fedha za maandalizi yote ya mauaji.
Washtakiwa wengine ni Shaibu Jumanne, ambaye anafahamika kwa jina la utani la Mredii, Mussa Mangu, Jalila Zuberi (Said), Karim Kihundwa, Sadick Jabir (Msudani) na Ally Mussa (Mjeshi).