HATIMAYE Prof. Ibrahim Lipumba, aliyekuwa Mwenyekti wa Chama cha Wananchi (CUF) ametangaza kurejea kwenye nafasi yake ya uenyekiti-taifa wa chama hicho.
Amesema, anarejea kwenye nafasi hiyo baada ya muda wa kutosha alioutumia kutafakari siasa za nchini na namna demokrasia inavyokanyagwa na watawala wa nchi hii.
“Nimemwandikia Katibu Mkuu (Maalim Seif Sharif Hamad) kutengua barua yangu niliyoandika 5 Agosti mwaka jana,” amesema Prof. Lipumba.
Prof. Lipumba alijiuzulu nafasi yake mwaka jana kwa madai ya kutoridhishwa na uamuzi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumridhia Edward Lowassa kupeperusha bendera ya umoja huo kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 kupitia Chadema.
Hata hivyo amesema, analazimika kurejea kwenye nafasi ya uenyekiti wa chama hicho taifa kutokana na kuguswa na matatizo ya demokrasia nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam amesema kuwa, amemuandikia barua Maalim Seif ili atengue uamuzi wake wa awali wa kuachia nafasi hiyo.
Katiba ya mwaka 1992 Toleo 2013 Ibara ya 117 inaeleza kwamba, barua ya kujiuzulu inapaswa kujadiliwa na Mkutano Mkuu kujadili jambo ambalo mpaka sasa halijafanyika.
Prof. Lipumba aliteuliwa kutwaa nafasi hiyo na Mkutano Mkuu mwaka 1999. Ibara hiyo inaipa mamlaka mkutano huo kukubali ama kukataa kujiuzulu kwake na kwamba, kauli yake ya leo kuwa Maalim Seif atengue barua yake inatokana na kutokwenda kwenye ngazi hiyo (Mkutano Mkuu) nyingine ya uamuzi.
Prof. Lipumba amesema kuwa, dhuluma iliyofanyika katika visiwa vya Zanzibar ya kuporwa kwa haki ya wananchi, imemsukuma kurejea kwenye mapambano ya haki nchini.
Amesema, demokrasia ya Tanzania ina matatizo akitaja miongoni mwayo ni Bunge kuendesha kwa itikadi ya chama.
Pia amesema kuwa, uongozi wa Rais John Magufuli unaonekana kuwa wa kasi isiyojali Demokrasia.
Akizungumzia Zanzibar amesema, chama chao na watanzania wapenda haki hawatambui utawala wa Dk. Ali Mohammed Shein visiwani humo kwa kuwa hakupatikana kwa njia halali ya kidemokrasia.
Amesema kuwa, Rais Magufuli asipozingatia misingi ya demokrasia nchi haitakuwa na uwajibikaji.