Serikali itakosa mchango wa dawa zenye thamani ya Dola 375 milioni za Marekani (Sh787 bilioni), ambazo zimekuwa zikichangwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID).
USAID ilitoa mchango huo chini ya mradi wa kutunza na kugawanya dawa hasa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV) kwa kipindi cha miaka 10 nchini.
Mradi huo ambao pia umeisaidia Serikali kujenga maghala ya kuhifadhia dawa umefikia mwisho.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya alisema licha ya mradi huo kufikia ukomo na kuwa na msaada, wizara imejipanga kuhakikisha kuna uhakika wa upatikanaji wa dawa nchini.
Dk Ulisubisya alisema hata bajeti ya mwaka 2016/17 ya Wizara ya Afya imetoa kipaumbele kwenye dawa.
“Tunataka kuhakikisha Watanzania wanafikiwa na huduma ya dawa kote nchini,” alisema.
Dk Ulisubisya alisema kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, USAID ilitekeleza mradi huo na wananchi zaidi ya 8,000 wamefikiwa na kupata huduma ya dawa.
Alisema wakati mradi huo unaanza watu waliokuwa wanatapa dawa hasa za ARV walikuwa wachache.
Dk Ulisubisya alisema shirika hilo pia lilisaidia kuweka mfumo wa kisasa wa kielektroniki wa kufuatilia matumizi na mahali dawa zinapopatikana.
Kaimu Mkurugenzi Afya wa USAID nchini, Janeane Dauis alisema mradi huo umekuwa na mafanikio nchini.
Dauis alisema shirika hilo litaendeleza ushirikiano wake na Serikali ya Tanzania ili kuweka msukumo zaidi wa kuboresha sekta ya afya nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu alisema mbali na kupata msaada wa kujengewa maghala na USAID, wako kwenye mkakati wa kujenga maghala yao ya kuhifadhi dawa.
Bwanakunu alisema shirika hilo lilitoa Dola 14.2 milioni za Marekani (Sh29.8 bilioni) kwa ajili ya ujenzi wa maghala.
Mkurugenzi huyo alisema MSD inatarajia kujenga maghala yake.Alitaja maeneo wanayotarajia kujenga maghala hayo kuwa ni Dar es Salaam eneo la Buguruni, Mtwara na Moshi.
Pia, alisema MSD inaendelea kupanua wigo wake katika mikoa mbalimbali ukiwamo Iringa.