JUMUIYA ya Wanataaluma ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA) imesema kilichotokea si walimu kugoma kufundisha programu ya Stashahada Maalumu ya Elimu, Sayansi, Hisabati na Tehama, bali tatizo ni kutoelewana na Menejimenti ya chuo kutokana na mazingira mabovu ya uendeshaji wa programu hiyo chuoni hapo.
Aidha, imelaani kitendo cha wanafunzi 7,802 wa Programu Maalumu ya Ualimu wa Msingi na Sekondari, waliorudishwa nyumbani bila kupewa muda wa kutosha kujiandaa kwa kuzingatia umri wao na mazingira waliyokuwa wanaishi, hali inayofanya wazagae mitaani huku wakiwa hawana pa kwenda.
Hayo yako kwenye tamko lililotolewa jana na Katibu wa jumuiya hiyo, Lameck Thomas, ambalo lilieleza kuwa lawama zimekuwa zikitupwa kwa walimu kutokana na taarifa hizo kutolewa na upande mmoja, ambao ni Menejimenti ya chuo kwenda serikalini bila kuwepo na taarifa yoyote kutoka kwa walimu kupitia jumuiya yao.
Thomas alisema si kweli kama walimu waligoma kufundisha lakini tatizo kubwa ni kutoelewana kati ya walimu na Menejimenti ya chuo kutokana na mazingira mabovu ya uendeshaji wa programu hiyo chuoni hapo.
"Hatuzungumzii fedha zaidi tunazungumzia suala la kuboresha elimu ili taifa lipate walimu wa baadaye katika kufundisha Sayansi, Hisabati na Tehama, vifaa vya kufundishia navyo ni changamoto kubwa,” alisema.
Katibu huyo alisema kama Jumuiya ya Wanataaluma wanapata hisia kwamba Wizara ya Elimu, imeamua kwa makusudi kushirikiana na uongozi wa chuo kupotosha uhalisia wa jambo hilo kwani hakuna hata wakati moja ambao wamefanya mawasiliano na walimu wenyewe kupata ukweli kutoka upande wao.
“Alichosema waziri bungeni juzi ni taarifa ya upande mmoja ambayo haitatupeleka kwenye utatuzi wa kudumu wa suala hili kutokana na ukweli kwamba walimu nao wana mengi ya kuzungumza,” alisema katibu huyo.
Alisema serikali imejenga desturi ya kuonana na menejimenti za vyuo pindi yanapotokea matatizo bila kupata taarifa kutoka vyanzo vingine hali ambayo imekuwa inasababisha vyanzo sahihi vya matatizo kutojulikana kwa uwazi.
Alisema changamoto za ufundishaji kutokana na uhaba na walimu kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo. Akitoa mfano alisema kwa sasa Chuo cha Sayansi Asilia na Hesabu, kina upungufu wa walimu 128 waliokuwa wanahitajika kufundisha programu hiyo kwa ufanisi; na kwa muhula uliopita walimu 72 tu ndio walibeba mzigo wa upungufu huo na muhula huu hali ilikuwa inaelekea kuwa mbaya zaidi.
“Wingi wa wanafunzi na uhaba huu wa walimu ulisababisha upangaji wa ratiba na kufundisha kutokana na ukweli kwamba kozi ziligawanywa katika mikondo mingi ambayo walimu walilazimishwa kuifundisha huku wakiwa na majukumu ya kufundisha kozi za shahada na majukumu mengine,” alifafanua.
Alisema chuo kimekuwa na desturi ya kupokea wanafunzi wengi bila kuzingatia idadi ya walimu waliopo na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia na hiyo si mara ya kwanza kwa chuo kufanya hivyo, kwani mwaka 2008 walileta wanafunzi wengi ambao matokeo yake walimu kufundisha masomo mengi kuliko uwezo wao wa kazi.
Alisema taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma ilipotoshwa, kwani haijaeleza ukweli wa madai uliowasilishwa na chuo husika.
Alisema katika Chuo cha Sayansi Asilia na Hesabu taarifa inasema yaliyowasilishwa ni madai ya Sh milioni 367.8 na kupungua mpaka Sh milioni 90 wakati uhalisia ni kwamba madai hayo hata yangebanwa namna gani yasingepungua mpaka chini ya Sh milioni 223.7.
Alisema mfano mwingine ni Chuo cha Elimu Masafa na Sayansi za Kompyuta ambao taarifa inasema waliwasilisha madai yanayozidi Sh milioni 100 wakati taarifa ya chuo inasema ni madai ya Sh milioni 53.7 tu.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Edson Baradyana alisikitishwa na yaliyotokea na kuitaka serikali kufanya jitihada za makusudi ili kumaliza mgogoro huo na hilo litawezekana kama walimu, wanafunzi na Menejimenti kukaa pamoja.
Baradyana alisema wanafunzi hawakutendewa haki kwani ilitolewa notisi ya ghafla ya kuondoka chuoni huku wengine wakiwa hawana nauli na hawakujua pa kwenda hali inayofanya waendelee kuzurura mitaani.
Alisema wanaamini kama Menejimenti ya chuo ingeonesha ushirikiano wa karibu kwa walimu wanaofundisha programu hiyo na kushirikiana, hayo yasingetokea au yasingekuwa makubwa kiasi hicho.
“Lazima kuangaliwa na kutatuliwa kwa changamoto nyingine zilizoibuliwa na wanataaluma na wanafunzi katika uendeshaji wa programu hiyo badala ya kujikita kwenye suala la malipo tu, serikali iwe na utaratibu wa kuwasiliana na walimu na wanafunzi mara kunapotokea matatizo vyuoni ili kupata taarifa toshelezi kutoka pande zote,” alisema Mwenyekiti wa Udomasa.
Aidha, wakati wa kurejeshwa nyumbani kwa wanafunzi hao wa Udom kukibebwa kisiasa na vyama vya upinzani, taarifa ya serikali imeeleza kuwa wahadhiri waliogoma, walitaka kulipwa posho ya zaidi ya Sh milioni 900.
Akitoa taarifa ya pili bungeni juzi usiku, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema wanafunzi hao si sehemu ya kazi zilizoko katika mikataba ya ajira ya wahadhiri hao, ila ni sehemu ya kazi ya ziada.
Kwa kuwa kazi hiyo ni ya ziada, Profesa Ndalichako alisema walikubaliana walipwe posho ya kazi ya nyongeza ambayo uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ulikuwa tayari kutoa zaidi ya Sh milioni 200.
Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, wahadhiri hao walisisitiza kuwa wanataka posho hiyo iwe zaidi ya Sh milioni 900, jambo lililokataliwa na Mkaguzi wa Ndani wa Mahesabu wa Udom aliyesema kuwa kiwango hicho ni kikubwa kuliko uhalisia wa kazi yenyewe.
Kutokana na kutokubaliana kati ya wahadhiri hao na uongozi wa Udom, wahadhiri hao ndio wakaitisha mgomo wa kufundisha wanafunzi hao huku wakiendelea na kazi za kufundisha walio katika programu za shahada ya kwanza na kuendelea.
Profesa Ndalichako alisema kwa uamuzi huo wa wahadhiri, serikali isingeweza kuwachukulia hatua kwa kuwa wamegomea kazi ya ziada na si kazi waliyoajiriwa na kuingia mkataba na chuo.
Kwa hali hiyo, Profesa Ndalichako alisema serikali ililazimika kuingilia kati ambapo Mei 10, mwaka huu Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya alikwenda chuoni hapo kutafuta suluhu.
Mbali na Naibu Waziri, alisema hata makatibu wakuu wa wizara hiyo nao walikwenda kuzungumza na wahadhiri hao bila mafanikio, huku wanafunzi hao wakikaa chuoni bila kuingia darasani kwa wiki ya tatu.
Profesa Ndalichako alisema mbali na madai ya wahadhiri hao, pia wakati wa kutafuta suluhu ya jambo hilo, walitazama suala la tija kwa wanafunzi hao wa diploma maalumu ambao ni zaidi ya 7,800 na pia kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza ambao pia wanapaswa kufundishwa na wahadhiri hao.
Kutokana na kukosa masomo kwa wiki tatu mfululizo na kuwepo kwa uwezekano wa kukosekana tija katika ufundishaji, Profesa Ndalichako alisema ndio uamuzi wa kuwarudisha nyumbani wanafunzi hao ukafanyika ili serikali iangalie upya utaratibu wenye tija zaidi wa kuwaendeleza wanafunzi hao.
Aidha, Profesa Ndalichako alisema wakati wanafunzi hao wakitakiwa kurudi nyumbani, walizingatia hali yao ya kipato, kwa kuwa tayari walikuwa wameshapewa fedha za kujikimu za siku 60 tangu Aprili 21, mwaka huu.
Profesa Ndalichako aliwataka wanafunzi hao kuvuta subira wakati serikali inatafuta namna bora ya kuwapatia elimu hiyo kwa kuzingatia tija kwao.