WAZIRI wa Fedha, Dk Phillip Mpango, amemtaka Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almas Maige (CCM) kumpa ushahidi ikiwemo majina ya wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), aliowatuhumu kufanya biashara na mwajiri wao.
Dk Mpango alisema hayo Jumatano usiku alipokuwa akijibu hoja za wabunge kuhusu Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango na kuongeza kuwa akipewa ushahidi huo, ataufanyia kazi.
Awali katika mchango wake, Maige alisema anao ushahidi wa maandishi (huku akiwa ameushika), unaoonesha kuwa kati ya mashirika ya umma yanayovunja Sheria ya Manunuzi, BoT ipo.
Alidai kuwa Sheria ya Manunuzi imetoa fursa ya kuanzishwa kwa vitengo na idara za manunuzi (PMU), lakini fursa hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya na vijana wa vitengo, hivyo kuiibia Serikali.
Kwa mujibu wa madai ya Maige, katika benki hiyo kuna vijana wamefungua makampuni ambao wamekuwa wakiyatumia kuomba zabuni za benki hiyo na kuyalipa.
Mbali na tuhuma hiyo, Maige ambaye alitangaza maslahi kuwa yeye ni mkandarasi wa daraja la kwanza, alidai pia kuna vijana wengine wamekuwa wakitoa zabuni kwa kampuni za nje ya nchi, ili watumie zabuni hiyo kupata safari za nje.
Alidai kuwa vijana hao baada ya kutoa zabuni kwa kampuni za nje, hutengeneza safari za kwenda kufanya uhakiki (due diligence) katika nchi zinakotoka kampuni hizo, ambako huko hupokea rushwa.
Katika kuthibitisha hilo, Maige alidai kuwa vijana hao wamediriki kutoa zabuni kwa kampuni iliyofungiwa na Mamlaka ya Manunuzi ya Umma Tanzania (PPRA).
Akijibu hoja hiyo, Dk Mpango alisema tuhuma hizo ndio kazisikia bungeni, hivyo hana uhakika ila akipewa ushahidi ataufanyia kazi kwa kuwa, utumbuaji majipu umesaidia kuongeza mapato na kutoka mfano wa makusanyo ya Sh trilioni moja kila mwezi.
Hivi karibuni, Serikali ilisitisha utoaji wa Sh bilioni 925 zilizokuwa zimeidhishwa na BoT kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya madeni ya Serikali.
Mbali na hilo, Serikali iliagiza Kitengo cha Madeni ya Nje ambacho awali kilikuwa chini ya BoT na baadaye kupelekwa wizarani, kirejeshwe mara moja ili kuimarisha udhibiti wa ukopaji na ulipaji wa madeni.
Kabla ya agizo hilo, ilielezwa kuwa malipo hayo yalikuwa yameidhinishwa na BoT kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya madeni mbalimbali lakini Serikali ikaagiza fedha hizo zirejeshwe Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki upya.