Mnamo mwezi Machi, 2016, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilitoa notisi ya siku 60 ikiwataka wanufaika wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kujitokeza na kuanza kurejesha mikopo yao.
Aidha, taarifa hiyo pia iliwataka waajiri kuwasilisha taarifa za waajiriwa wao na makato ya marejesho. Baada ya kipindi hicho kumalizika, kipindi cha notisi hiyo kiliongezwa ambacho pia kimekwisha.
Kufuatia hatua hiyo, Bodi inapenda kuwataarifu wanufaika wote wa mikopo kwamba kuanzia wiki ijayo itaanza kutangaza majina ya wale wote ambao hawajaweza kujitokeza na kuanza kurejesha mikopo yao.
Zoezi hili litajumuisha pia waajiri ambao hawajawasilisha taarifa za waajiriwa wao. Hatua hiyo itafuatiwa na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote watakaoshindwa kutimiza matakwa hayo kwa mujibu wa kifungu cha 19A (1) cha sheria Na. 9 ya mwaka 2004.
Hivyo basi, wanufaika wa mikopo wanahimizwa kuanza kulipa madeni yao na waajiri kuwasilisha taarifa za waajiriwa au kufika kwenye ofisi za Bodi ya Mikopo ili kupata Ankara za madeni yao kabla ya zoezi la kutangaza majina halijafanyika. Marejesho yanaweza kufanyika kupitia Akaunti:
A/C No. 2011100205 – NMB
A/C No. 01J1028467503 – CRDB
A/C No. CCA0240000032 – TPB
Ni muhimu kuzingatia taarifa hii ili kuepuka usumbufu utakaojitokeza kutokana na hatua zitakazochukuliwa.
Imetolewa na:
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu