KIAMA cha watoa na wapokea rushwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewadia baada ya Mwenyekiti mpya wa chama hicho, Rais John Magufuli, kuahidi kuwa atakomesha rushwa ndani ya chama hicho kwa nguvu zote.
Magufuli ambaye anasifika kwa kusema kweli, aliahidi kukomesha rushwa ndani ya chama hicho juzi mjini hapa. Alisema aligombea urais mwaka jana kwa tiketi ya CCM na kwenye mchujo huo alishuhudia jinsi rushwa ilivyo kero.
Aidha, alisema kuwa alikwenda mkoani Iringa wakati wa mchujo kutafuta wadhamini, lakini alikuta wilaya moja yote imeshanunuliwa, hivyo ilibidi aende kwenye kata moja vijijini wilayani humo, ambako alipata wadhamini.
Magufuli alisema hayo wakati akitoa hotuba ya shukrani kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, uliofanyika mjini hapa. Katika mkutano huo, Magufuli alichaguliwa kwa kishindo kuwa Mwenyekiti wa chama hicho.
Mwenyekiti huyo mpya wa CCM alisema mara nyingi fedha imekuwa kigezo cha kupata uongozi katika chama hicho kikongwe, mfano kwenye urais, ubunge na udiwani.
Alisema hali hiyo imesababisha haki kupotea, wasio na fedha kushindwa kupata uongozi na pia imekuwa chanzo cha chama kupoteza maeneo kwa wapinzani.
Magufuli alisema serikali haiwezi ikafanikiwa kuondoa rushwa, kama chama chenyewe tawala kinakumbatia rushwa.
“Katika uongozi wangu nimedhamiria kukomesha rushwa. Mtu yeyote atakayetoa rushwa, hatachaguliwa,” alitangaza Rais Magufuli na wajumbe kumshangilia kwa nguvu.
Alisema kamati za maadili za chama za ngazi zote, zitatumika kufuatilia watoa rushwa na kuandaa taarifa zao, zitakazopelekwa katika vikao vya juu kwa uamuzi.
Aliwakumbusha watoa rushwa kuwa kanuni za uongozi za chama, zinasema mtu atakayethibitika kuwa ametoa rushwa ili kupata uongozi, atanyang’anywa cheo chake.
Alisema yeye aligombea urais na kuupata bila rushwa, hivyo chama chini ya uongozi wake, hakitawaonea aibu watoa rushwa.
Aliwaonya waliozoea kupata uongozi kwa rushwa, kuacha mara moja; na mfano wa watu hao ni wanaonunua kadi nyingi za CCM kisha kuzigawa kwa wanachama ili washinde mikutano ya kuchuja wagombea na watoa takrima.
Wengine ni wanaofanya kampeni kabla ya muda uliopangwa. Mbali na rushwa, Magufuli alitaja jambo lingine linalomkera katika chama kuwa ni usaliti.
Alisema ni heri kuishi na mchawi kuliko na msaliti kwa sababu msaliti ni mtu hatari mno. Alisema katika kipindi chake cha uongozi, atahakikisha suala la usaliti linafikia mwisho katika chama.
“Kuna watu hivi sasa utamkuta asubuhi yupo CCM lakini usiku Chadema. Tutakomesha hali hii. Wasaliti wa namna hii hawatakuwepo”, alisema.
Aliwaagiza wasaliti waliopo, watubu kuanzia sasa au waondoke wenyewe kwenye chama kwa sababu wasipopisha, wataondolewa tu. Mwenyekiti huyo wa CCM alisema CCM ya sasa, haihitaji watu aliowaita “CCM Maslahi” au “CCM Pandikizi”.
Alieleza wanachama wa CCM wanaohitajika zama hizi ni wale ambao mchana na usiku ni CCM, wakati wa jua na mvua wapo CCM na wakati wa shibe na njaa pia wapo CCM. Mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, imekuwa ajenda kubwa ya Magufuli tangu akiwa mbunge na waziri kwa miaka 20.
Juhudi zake za kupiga vita rushwa ni moja ya sifa zilizombeba kwenye mchujo wa kuwania urais ndani ya CCM mwaka jana, ambapo kulikuwa na wagombea 38. Kwenye mchujo huo aliibuka kidedea na wenzake 37 kura zao hazikutosha.
Hivi karibuni Bunge lilipitisha Muswada wa Sheria ya Kuanzisha Mahakama Maalumu ya Rushwa na Ufisadi. Rais Magufuli amesaini muswada huo kuwa sheria. Mahakama hiyo ilitarajiwa kuanza kazi Julai Mosi mwaka huu. Tayari serikali imeteua majaji 14 wa mahakama hiyo maalumu chini ya Mahakama Kuu ya Tanzania