Safari ya kuelekea kwenye mafanikio inahitaji ujasiri, sio ujasiri tu bali ujasiri wa hali ya juu sana, kama ilivyo ujasiri alionao simba awapo mwituni, katika kusaka riziki yake ili kuhakikisha ya kwamba halali au hafi kwa sababu ya njaa.
Ujasiri huo huo alikuwa nao simba ndio ambao unauhitaji wewe ndugu yangu, katika safari ya kujifunza, chukua muda wa kujivika taswira ya kiujasiri ili ufanikiwe zaidi.
Nafahamu ya kwamba ipo haja ya wewe kuendelea kujua mbinu ambazo zitakufanya upate ujasiri huo. Hata hivyo niweze kushukuru Mungu kwa kunipa kalama hiyo ya kuweza kutumia fikra chanya ambazo zinanifanya nikupe baadhi ya mambo yatakayokusaidia kwa namna moja ama nyingine katika kusaka mafanikio hayo.
Kama alivyo simba kuishi katika misingi ya kujiamini ,basi ndivyo ambavyo nilivyo na hasira juu ya neno mafanikio.
Laiti ungelifanya uchunguzi siku moja kumchunguza simba ungaligundua ya kwamba simba anaishi kwa kujiamini ili aendelee kuishi miaka mingi zaidi, pia simba huyo huyo anaishi kwa hofu ambayo itafanya asilale au afe njaa.
Kupitia hilo ifike mahali na wewe pia uishi kwa kujiamini ya kwamba unajua ambacho unakihitaji, pia uishi kwa hofu ya kushindwa katika mafanikio pia uishi kwa kuwa na hofu ya Mungu kwa kila hambo ambalo unalifanya siku zote.
Watu wengi ambao wamefanikiwa na ambao hawajafanikiwa wanafanana katika masuala ya kuishi bila hofu ya Mungu. Wapo wale ambao licha ya kwamba maisha yao ni kitajiri, lakini bado wanaishi katika misingi ya kutenda mambo yao bila kumshirikisha Mungu, maisha ambayo kiukweli yanafanya waishi kwa wasiwasi licha ya maisha yao kuwa mazuri.
Nikija upande wa pili wa shilingi ambapo watu wengi wanaishi maisha ya duni, ambapo wengi wetu tupo pia tumekuwa ni watu wa kukata tamaa siku zote na imefiki mahali tumejikuta tunamsahau Mungu, sio kumsahau Mungu tu bali imefika kipindi mpaka tunakufuru, unaweza kusema leo nahubiri la hasha ila ukweli ubaki palepale kwa jambo lolote ambalo unalifanya ili uweze kufanikiwa unatakiwa uishi kwa kuwa na HOFU YA MUNGU.
Zifuatazo ndizo kanuni ambazo unatakiwa kuzitumia kufanikiwa;
1. Kuwa tayari kujifunza.
Moja ya njia ya kukusaidia kufanikiwa zaidi ni lazima uweze kujifunza, huenda ukawa hajanipata vizuri ila ukweli wenyewe ndio huu hapa, watu wengi wanataka kupanda ngazi ya kimafanikio, bila kujua namna ya kuitumia ngazi hiyo ya kupata mafanikio.
Kwa mfano leo hii utamkuta mtu anataka kuwa mfanyabiashara mkubwa lakini ukimwambia kuwa jambo hilo linahitaji ulazima wa kujifunza, utakuta mtu huyo hayupo tayari kujifunza juu ya biashara hiyo.
Lakini mimi huwa naamini jambo lolote ukitaka kulifanya kwa weledi ni lazima uwe tayari kujifunza, fikiria kwa umakini kisha uone ni kitu gani ambacho hauitaji kujifunza ambacho kinahusiana na mafanikio?
Ukitafakari kwa umakini utagundua ya kwamba hakuna jambo hata moja. Mambo ambayo hutakiwi kujifunza labda matendo ya hiari na yasiyo ya hiari yanayotokana na msukumo wa mwili tu yatokanayo na mawazo ya binadamu hasa hisia.
Kujifunza huku hakuhitaji wewe kukaa darasani miaka mingi, mpaka ufanikiwe ila inahitaji kujua unataka nini? Baada ya hapo ndio utagundua unatakiwa kujifunza nini.
Nikuibie siri ambayo hajawahi mtu yeyote kukuambia kwamba siri ya utajiri ipo kwenye "maandishi" siri hii usimwambie mtu bali chukua hatua pindi utakapopata ukweli juu ya jambo hilo, wengine wakikuuliza juu ya mafanikio yako ndipo uwambia siri ya mafanikio ilipo.
2. Kuwa tayari kulipa gharama.
Mara kadhaa niwehi kuandika ya kwamba "chochote bila chochote huwezi kupata chochote" wengi walikuwa hawajanielewa ila leo ndio uwanja wako wa kuweza kunielewa juu ya jambo hilo.
Iko hivi kwa chochote kile ambacho unakitaka leo kina gharama zake, kama maelezo ya hapa juu yanavyojieleza kwamba unahitaji kuwa tayari kujifunza, basi jambo hili huenda sambamba na kulipa gharama, gharama hizi ni kama vile za kujifunza kwenye makongamono, kununua vitabu, majarida, magazeti ,vipeperushi kulipa ada za mafunzo mbalimbali ikiwemo semina au shule.
Ukiyafanya hayo utakuwa kwa ubora na weledi wa hali ya juu, utakuwa ni miongoni mwa watu ambao wanafanya mambo ya kimaendeleo kila siku, pia jamii ambayo inakuzunguka watatamani kwa kiwango kikubwa kitu ambacho unafanya wewe.