Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakitotekeleza mpango wa kuhamia Dodoma kwani ni wa kukurupuka.
Msimamo huo umetolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alipozungumza na gazeti hili wakati wa kutoa heshima za mwisho za aliyekuwa mpigapicha mwandamizi wa gazeti la Tanzania Daima, Joseph Senga ambaye anatarajiwa kuzikwa leo huko Kwimba, Mwanza.
“Serikali inaendeshwa kwa kukurupuka. Ni mpango usiotekelezeka,” alisema Mbowe.
Alisema uhamaji unaotekelezwa sasa haukuwa na maandalizi wala mkakati kwenye ilani ya chama tawala wala Bajeti ya Serikali hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kukwama huko mbele.
Miongoni mwa vitu vinavyoufanya mpango huo usitekelezeke kwa ufanisi, kwa maoni yake, alisema miundombinu ya kutosheleza watendaji wote na wadau wengine muhimu ambao watalazimika kufuata huduma muhimu za wizara na idara za Serikali.
“Huku ni kuwaumiza wananchi. Watumishi wa Serikali, wanahabari na wadau wengine wakihama wote watapata wapi malazi katika mji ule?”
Muda mfupi baada ya kukabidhiwa majukumu ya kuiongoza CCM, Julai 23, Rais John Magufuli alieleza nia yake ya kutekeleza uhamisho wa makao ya Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na kwamba atahakikisha, ndani ya miaka minne anatimiza ndoto hiyo ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya tangu mwaka 1973.
Siku moja baadaye, akihutubia kwenye hafla ya Siku ya Mashujaa mjini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza kuhamia mjini humo Septemba na kusema kuwa wizara nyingine zitamfuata.
Tangu kutolewa kwa matamko hayo ya viongozi waandamizi wa Serikali; wizara, taasisi, mashirika ya umma, idara na baadhi ya ofisi binafsi, mabalozi na wanadiplomasia zimeanza kuandaa mazingira ya utekelezaji huo.
Lakini, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni alionyesha wasiwasi wake juu ya umakini wa Serikali kutekeleza azma hiyo akisema kutakuwa na usumbufu mkubwa kwa watumishi na familia zao suala linaloweza kupunguza morali yao ya kazi. “Watu wana familia zao. Watoto wanasoma... Dodoma hakuna shule za kutosha watoto watakaohama na wazazi wao.”
Alisema wakati wazo hilo linatolewa na kuungwa mkono enzi za Mwalimu Nyerere kulikuwa na sababu za msingi lakini hivi sasa kuna mabadiliko makubwa yaliyochagizwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Alisema wakati huo mindombinu ya mawasiliano haikuwa rafiki tofauti na iliyopo sasa inayowezesha watu walioko New York, Marekani kufanya mkutano na wenzao waliopo popote duniani kwa kutumia miutano kwa njia ya masafa. “Sababu zimepitwa na wakati,” alisisitiza.
Alishauri, mpango huo ungetekelezwa kwa utaratibu maalumu, akitoa mfano kwa wizara moja au mbili kuhama kwa kila mwaka mpaka zitakapokamilika ili kupunguza gharama zisizo na ulazima.
Alisema kuhamisha wizara siyo waziri au katibu mkuu pekee, bali ni watumishi wote na miundombinu yote iliyopo ambayo ni muhimu kwa utekelezaji wa majukumu yake: “Kwa mfano, Wizara ya Kilimo ina watumishi 2,000 na maelfu ya mafaili yenye taarifa za kiutendaji… unawahamishaje watu wote hawa na mindombinu iliyopo unaifanyaje? Namshangaa IGP anaposema anahama wakati mifumo yote ya uchunguzi na taarifa imejengwa hapa kwa kutumia mabilioni ya fedha za wananchi.”
Wiki iliyopita, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Polisi, Nsato Marijani alisema jeshi hilo litahamia Dodoma mwezi huu na watakaohusika ni Inspekta Jenerali na baadhi ya makamishna.