Imeelezwa kwamba serikali imeshaanza kushirikisha wadau mbalimbali kupata maoni ya jinsi ya kuendesha mpango huo kwa ufanisi na tija.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) alisema serikali itaanza kutoa fedha hizo kuanzia mwaka wa fedha ujao. Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki baada ya mkutano wa wadau waliokuwa wanajadili rasimu ya mpango huo wa utoaji fedha kwa ajili ya maendeleo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wawakilishi wa halmashauri za wilaya, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), mabenki, mifuko ya hifadhi ya jamii na vikundi mbalimbali. “Kwa kuanzia, fedha hizo zitatolewa kwa awamu tatu katika kipindi cha miaka mitano,” alisema.
Alisema fedha hizo zitatolewa kupitia benki kabla ya kutolewa kwa vikundi mbalimbali kama Vicoba, Saccos na vikundi vingine kulingana na taratibu zitakazowekwa. Alisema mpango utaanza na mikoa 10 iliyo nyuma katika kutumia huduma za kifedha kwa kuzingatia taarifa ya utafiti ya Finscope ya mwaka 2013.
Mikoa hiyo ni Singida, Lindi, Mtwara, Mbeya, Shinyanga, Geita, Kagera, Dodoma, Rukwa na Ruvuma. Akifungua mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uhusiano ya Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama, alisema mkutano huo ulilenga kupata maoni ya wataalamu ya namna bora ya kuutekeleza.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri, Kaimu Mkurugenzi, Maendeleo ya Sekta Binafsi, Uwekezaji na Uwezeshaji, Ofisi ya Waziri Mkuu, Victor Mwainyekule alisema mawazo yaliyopatikana yatazingatiwa kuboresha mpango huo unaolenga kupambana na umaskini.
Mkuu wa Uendeshaji, Benki ya Wanawake (TwB), Zablon Yebete alisema mpango huo ni uwekezaji mkubwa kwa Watanzania unaopaswa kuungwa mkono na vyombo vya fedha na wadau wengine nchini.
“Tunatakiwa kuunga mkono mpango huu unaohusisha vyombo vya fedha katika utekelezaji wake kwa faida ya taifa,” alisema. Kwa mujibu wa mpango huo, walengwa watapatiwa mafunzo ya ujasiriamali kabla ya kupatiwa fedha hizo.