Chama cha Wananchi (CUF), kimesema kinajiandaa kutoa tamko zito kuhusu hatima yake kisiasa visiwani Zanzibar.
Kufuatia
hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zaniabar (ZEC), Jecha Salum
Jecha kufuta Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, ambao chama hicho
kinaamini kuwa kilishinda, CUF iligomea uchaguzi wa marudio wa Jumapili
iliyopita.
Tangu hapo, Rais Dk. Ali Mohammed Shein alishaapishwa Alhamisi iliyopita kuongoza visiwa hivyo mpaka mwaka 2020.
CUF inaamini matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana yangeonyesha kuwa mgombea wao, Maalim Seif Hamad, ameshinda kwa kishindo.
Aidha,
Chama hicho kimesema hakitababaishwa na hatua ya serikali kumwondolea
walinzi Maalim Seif kwasababu chama hicho kina walinzi wa kutosha
kufanya kazi hiyo .
Akizungumza
na Nipashe jana, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Magdalane
Sakaya, alisema CUF inafanya maandalizi ya vikao vya ngazi za juu
ambavyo ndivyo vitakavyotoa maamuzi kuhusu mustakabali wa kisiasa
visiwani humo, baada ya uchaguzi wa marudio.
Sakaya
ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kaliua mkoani Tabora kwa tiketi ya CUF,
alisema ingawa shughuli za chama zinaendelea kama kawaida, vikao hivyo
ambavyo ni Kamati Tendaji na Baraza Kuu vitakaa ndani ya muda mfupi ujao
na vitajadili na kutoa msimamo wa chama kuhusu hatma ya Zanzibar.
“Tunaendelea
na maandalizi ya vikao hivyo na wiki ijayo vitakaa na kutoa mwelekeo wa
nini kinaendelea na nini msimamo wa chama kuhusu siasa za Zanzibar,
lakini tunaendelea kuamini kuwa mgombea wetu ndiye chaguo sahihi la
Wazanzibari katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana,” alisema Sakaya.
Aidha,
Sakaya alisema CCM ilishapanga siku nyingi za kuhakikisha wanashinda
kwa hila kwenye uchaguzi huo ili wabadili Katiba ya Zanzibar
inayozungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa na hatimaye waunde serikali
peke yao ambayo haitakuwa na vyama vya upinzani.
Kuhusu
taarifa za Maalim Seif kupunguziwa walinzi, Sakaya alisema CUF haiwezi
kubababishwa na hilo kwasababu chama chao kina walinzi wa kutosha ambao
watamlinda wakati wote na aliongeza kuwa hatua ya CCM kulazimisha
kumwapisha Dk. Shein ni udikteta wa kupindukia.
Alielezea
kushangazwa na idadi kubwa ya askari polisi na wa JWTZ wakati wa
uchaguzi wa marudio, hali ambayo iliwatisha wananchi na wengine kuogopa
kwenda kwenye shughuli zao za kila siku.
“Baadhi
ya wanachama wa CUF bado wako mahabusu hadi leo na wanasheria wetu
wanaendelea na mchakato wa kuwatoa maana hawana kesi," alisema Sakaya.
"Wengi
walipigwa na kuteswa na kubambikiwa kesi kwasababu za kisiasa na kwa
kuwa wameshatimiza kile walichokuwa wanakitaka tunaamini watawaachia.”
Mwenyekiti
wa ZEC Jecha alimtangaza Dk. Ali Mohammed Shein kuwa Rais wa Zanzibar
Jumatatu kwa kupata asilimia 91.4 ya kura halali.
Kwa
mujibu wa Jecha, Shein alipata kura 299,982 kati ya jumla ya wapiga
kura waliojitokeza 341, 865. Jumla ya Wazanzibari wlaiojiandikisha
walikuwa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana ambao
ulifuntwa na Jecha walikuwa 503,580.
Nafasi
ya pili ilichukuliwa na mgombea urais wa ADC, Hamad Rashid aliyepata
kura 6,734 na Maalim Seif Sharif Hamad (CUF) alishika nafasi ya tatu kwa
kupata kura 6,076.
Ushindi
wa Dk. Shein wa asilimia 91.4 una maana vyama vingine saba
vilivyoshiriki vilikosa asimilia 10, ambazo kisheria zingeliweza
kukifanya kuingia kwenye serikali ya umoja wa kitaifa.
Jecha
aliufuta uchaguzi wa Oktoba 25 kwa madai ya kuwepo kasoro kubwa, hatua
ambayo ilipingwa vikali na CUF, ambacho aliyekuwa mgombea wake wa urais,
Maalim Seif Sharif Hamad, alisema alikuwa ameshinda kwa zaidi ya 52%.
Bado
haijafahamika ikiwa Dk. Shein ataunda serikali nyengine yenye muundo wa
umoja wa kitaifa, kwasababu mbali na chama chake, hakuna chama kingine
kilichotangazwa na ZEC kufikia asilimia 10 ya kura za jumla wala kupata
wajumbe kwenye baraza la wawakilishi, masharti muhimu kwa chama
kujumuishwa kwenye uundaji wa serikali kwa mujibu wa katiba ya visiwa
hivyo.