Aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akitoa salamu za Sikukuu ya Pasaka kwenye Ibada Maalumu ya Kitaifa iliyofanyika kwenye Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano, Upanga jijini Dar es Salaam.
Makonda alipewa nafasi ya kutoa salamu mara baada ya Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam wa Kanisa hilo, Dk Valentino Mokiwa kumaliza kutoa mawaidha ya masomo ya Pasaka.
Akiwaomba Watanzania kuongeza kasi ya kumuombea Rais Magufuli, Makonda alisema Rais anachukua hatua zinazowaathiri watu wengi waliokuwa wamejitengenezea mtandao wa kuiba mali za umma kwa maslahi yao binafsi.
“Rais anapomuondoa Mkuu wa Mkoa anayeiba mali ya umma, machungu hayabaki kwa Mkuu huyo wa Mkoa peke yake bali yanawakumba watu wake ambao katika mtandao ule wote walikuwa wananufaika na wizi huo.
“Au mathalan aliyefukuzwa ni mkandarasi, basi utakuta katika mtandao wake wapo watu kati ya 80 hadi 100, hawa wote wananufaika na wizi au ufisadi wa mkandarasi huyo. Ukichunguza utakuta wapo watu wa Manunuzi, Wahasibu na wengineo,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Alisema hata hivyo kwa vile Rais anayo dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania ili kuhakikisha kuwa wanyonge ambao ni wengi wananufaika na rasilimali za nchi yao, ni lazima Watanzania wazidi kumuombea ili atimize lengo lake na kuifikisha Tanzania mahali pazuri.
“Uzuri ni kwamba wezi na mafisadi ni wachache sana, lakini wema na wazalendo ni wengi. Kinachotakiwa ni wale wengi kumuomba Mungu kwa nguvu zao ili kusafisha maovu, wizi na ufisadi vinavyofanywa na watu wachache kwa maslahi yao na familia zao,” alisema Makonda.
Akizungumzia hali ya ulinzi na usalama, alisema si nzuri na kwamba kazi kubwa inapaswa kufanywa ili kukabiliana na janga la ujambazi na uhalifu katika Mkoa wa Dar es Salaam, huku akionya kuwa kuanzia Julai mosi ataongoza operesheni kabambe ya kuwabaini watu ambao hawatajitokeza kuhakiki umiliki wa silaha zao.
“Juzi tu hapa, majambazi wamevamia mahali saa 4:00 asubuhi wakiwa na bunduki na mabomu. Hili si jambo la mchezo. Lakini pia kuna mahala kwenye mpaka wetu na Mkoa wa Pwani, kuna msitu ambako kuna wahalifu wana kambi ambako wanatoa mafunzo ya kutumia silaha hadi kwa watoto wa shule wanaopita hapo,” alisema.
Alisema ili kupambana na umiliki usio halali wa silaha ni lazima watu wote wanaomiliki silaha wajitokeze ili kuzihakiki upya katika muda uliowekwa na serikali, watakaokaidi watakumbana na mkono mrefu wa sheria.
“Wengine silaha ilikuwa inamilikiwa na mzazi wake, sasa kwa vile ameshatangulia mbele za haki, yeye anaichukua na kuendelea kuitumia. Hapana hii si mali yake ni mali ya serikali ni lazima airejeshe na kuomba upya ili kama ana sifa aweze kupewa kuimiliki kihalali,” alisema Makonda.