Jana asubuhi, mwandishi wetu alishuhudia magari yakipita katika daraja hilo, kama ilivyo katika barabara zilizozoeleka za Mandela na Morogoro, huku baadhi ya madereva wakiendesha na kujipiga picha kwa simu za mkononi.
Watembea kwa miguu nao hawakuwa nyuma na idadi yao ilizidi kuongezeka mchana baada ya mvua zilizokuwa zikinyesha kuisha na sehemu kubwa walionekana kama watalii waliokuwa wakipiga picha na kuzunguzunguka katika eneo hilo.
“Sasa hivi mtu anakuwa na chaguo apite wapi anapoona atafanikisha safari yake kulingana na mahitaji,” alisema mmoja wa madereva waliotumia daraja hilo, Emmanuel Nzera.
Alisema kufunguliwa kwa daraja hilo ni neema kwa kuwa litaondoa usumbufu wa foleni katika vivuko upande wa Kigamboni na Feri na kwamba, kinachosubiriwa sasa ni gharama ya kulipia itajwe.
Mkazi wa Kigamboni, Ashura Ally alisema matumizi ya daraja hilo yatarahisisha usafiri kwa kuruhusu daladala kupita, jambo ambalo litawapunguzia gharama za bodaboda.
“Sasa kutakuwapo na wingi wa watu, hivyo na magari yatakuwa na safari za huku ambazo zitatusaidia kufika Feri na mjini kwa urahisi,” alisema.
Awali, mitumbwi ambayo ilikuwa ikitumika kuvusha abiria kabla kutoka Kigamboni kwenda Kurasini ilionekana ikiwa imeegeshwa kwenye ufukwe chini ya daraja hilo.
Hata wakati magari mengi na watu wakikimbilia katika daraja hilo la kisasa, hali ilikuwa tofauti katika eneo la Kivukoni kulikoshuhudiwa magari machache yakiingia kwenye vivuko vya Mv Kigamboni na Mv Magogoni.
Idadi kubwa ya watu iliyozoeleka kuwapo katika eneo la kusubiria vivuko mwishoni mwa wiki ilionekana kupungua na hakukuwa na pilika za abiria kuwahi kuingia kwenye vivuko.
Mmoja wa madereva waliokuwapo Kivukoni, Mussa Nzilo alisema ataendelea kutumia vivuko kwa kuwa kuna watu wanakaa maeneo ya karibu na Feri, hivyo kutumia daraja itakuwa safari ndefu kwao.
“Mimi nakaa hapo Feri kwenye kota za Bandari nikisema nipite kule Kurasini nitapoteza muda, ikizingatiwa kwamba huku hakuna foleni kama unavyoona sehemu kubwa ya watu wamekimbilia darajani,” alisema Nzilo.
Pamoja na watu wengi kuhamasika kutumia daraja hilo, kulikuwa na mkanganyiko wa baadhi ya watumiaji kushindwa kufahamu njia sahihi wanazotakiwa kupita.
Wafanyabiashara katika eneo hilo walisema huenda daraja likawa neema kwao kutokana na kuongezeka kwa watu, hivyo mzunguko wa fedha unaweza ukaongezeka.
“Japokuwa sijaona kituo, lakini hata kitendo cha watembea kwa miguu kupita hapa kwa wingi inaashiria baada ya kuzinduliwa rasmi pengine idadi ya watu itaongezeka na kusababisha kupanuka kwa biashara,” alisema Neema Nditi.
Daraja hilo linatarajiwa kuzinduliwa rasmi Jumanne ijayo na Rais John Magufuli.