Imesema miongoni mwa madhara hayo ni ya kiafya pamoja na kupotea kwa mapato mengi kutokana na uingizwaji wa simu hizo nchini.
Aidha, imetahadharisha kuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza katika uzimaji simu na kuwataka wananchi na wafanyabiashara wazingatie maagizo yaliyotolewa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alisema hayo wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha habari hapa nchini juzi.
‘Tunategemea kuzima simu zote feki kutokana na madhara yake kiafya hasa kwa watumiaji, kukosekana kwa viwango vya ubora wa simu hizi na hivyo wananchi kupoteza fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa simu hizi kwani hufa mara kwa mara,” alisema.
Prof. Mbarawa alisema kwa sasa jopo la wataalamu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) lipo mkoani Singida kwa ajili ya kutoa elimu ya utambuzi wa simu hizo ili kuwasaidia wananchi kuzibaini kwa urahisi.
Alisema wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari kabla ya kununua simu, ikiwamo kumuuliza muuzaji, kudai risiti na kuitunza ili kudhibiti uingizwaji na usambazaji wa bidhaa hizo nchini.
Katika hatua nyengine, Prof. Mbarawa alisema suala la Mkongo wa Taifa linaendelea vizuri na serikali kwa kushirikiana na watoa huduma wa mawasiliano wanaendelea na usimikaji wa minara ya mawasiliano katika sehemu mbalimbali za nchi hususan vijijini ili kuweka huduma bora za mawasiliano nchini.