Mabosi wa mashirika mawili ya Serikali nchini, wanaodaiwa kulipwa mshahara wa Sh milioni 36, wamekanusha madai hayo, huku wakielezea kushangazwa na taarifa hizo wakati hata nusu ya fedha hizo, hawapati.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu alisema halipwi mshahara huo.
Akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo kuhusu taarifa ya utekelezaji na utendaji wa shirika hilo kwa mwaka 2014/15, Mchechu alisema shirika hilo pamoja na kutekeleza majukumu yake, bado lina changamoto za uhaba wa fedha.
“Katika ujenzi wa nyumba zetu, Serikali haigharamii masuala ya miundombinu kama vile maji, umeme, barabara hilo ni jukumu letu na linatugharimu fedha nyingi.
“Sasa nashangaa wako watu wanasema mimi nalipwa mshahara mkubwa, sielewi wametoa wapi huo mshahara kwa sababu silipwi mshahara huo, mimi nalipwa chini ya huo walioutaja,” alisema Mchechu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura),Felix Ngamlagosi aliiambia kamati hiyo kwamba mamlaka hiyo ina changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa watumishi na maslahi duni.
Alisema wakati maslahi ya wafanyakazi ni duni, ameshangaa kusikia vyombo vya habari vikisema yeye ni miongoni mwa wakurugenzi wanaolipwa Sh milioni 36 kwa mwezi.
“Jamani hapa tunazungumzia maslahi duni ya watumishi wetu, nashangaa kusikia naambiwa nalipwa milioni 36, mshahara wangu haufiki hata nusu ya hizo fedha,” alisema Ngamlagosi.
Nyumba nafuu
Awali wajumbe wa kamati hiyo baada ya kupitia taarifa hiyo ya NHC, waliiomba Serikali kuharakisha kuwepo kwa sera ya nyumba ili kurahisishia mashirika yanayohusika na masuala ya ujenzi wa nyumba kujenga nyumba za bei nafuu kwa wananchi.
“Yapo malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba NHC mnauza nyumba kwa bei kubwa, huku mkitoa matangazo kuwa nyumba hizo ni bei nafuu,” alihoji mjumbe wa Kamati hiyo, Mbunge wa Ushetu, Elias Kwandikwa.
Akijibu hoja hiyo, Mchechu alisema nyumba zinazojengwa na NHC zinauzwa kuanzia Sh milioni 30 hadi 250 kwa fedha taslimu na kwamba mnunuzi atatakiwa kulipa kodi.
Aliongeza kuwa kama mnunuzi hatakuwa na fedha taslimu, benki washirika wanatoa mikopo kwa ajili ya ununuzi wa nyumba hizo, ila wanunuzi watatakiwa kulipa riba za benki husika.
Baada ya majibu hayo, wajumbe hao walitaka Serikali iangalie jinsi ya kupunguza mzigo kwa shirika hili na ikiwezekana waondolewe kodi ya uingizaji vifaa vya ujenzi ili kusaidia nyumba hizo kuuzwa kwa bei nafuu, kwa lengo la kuwanufaisha wananchi hasa wale wa kima cha chini.
Akizungumzia hoja hizo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula alisema shirika hilo, linapaswa kuwasiliana na watendaji katika maeneo husika ya ujenzi wa nyumba hizo, ili wawasaidie kubeba gharama ndogondogo.
“Serikali na wizara zinafanya kazi kwa ushirikiano na NHC, na hili la gharama za miundombinu, kila halmashauri nchini ambayo ujenzi wa nyumba hizo unafanywa, inaweza kuangalia jinsi ya kusaidia gharama za miundombinu, ili nyumba hizo ziuzwe kwa bei nafuu zaidi kwa wananchi,” alisema Mabula.