Dar es Salaam. Mama mzazi wa binti mmoja mkazi wa Dakawa wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro hivi karibuni alipokea ujumbe wa picha ya video katika simu yake ya mkononi na haraka aliifungua akiwa na shauku ya kuitazama.
Lahaula! Shauku yake ya kuitazama video hiyo aliyodhani ni sawa na nyingine za matukio ambazo amekuwa akiziona zikisambazwa mitandaoni, iligeuka huzuni na fedheha kubwa alipoona ikimwonyesha bintiye akidhalilishwa na wanaume huku akilalamika asirekodiwe bila mafanikio.
Mama huyo alijizoazoa haraka na simu yake akatimua mbio hadi Polisi kuripoti tukio hilo lililolenga kumdhalilisha binti yake na kuifedhehesha familia nzima. Hicho ndiyo kiini cha vijana 11 wa Dakawa kukamatwa ili waisaidie Polisi kuhusu walioshiriki tukio hilo na walioisambaza video hiyo kwa mama huyo na kwenye mitandao ya kijamii hasa WhatsApp.
Katika video hiyo, wakati mwanamme mmoja akimdhalilisha huyo binti, mwingine alikuwa akirekodi na baada ya kukamilisha tendo hilo lisilo na utu tena bila huruma waliwatumia watu wengine katika eneo la Dakawa.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Betty Mkwasa aliliambia gazeti hili jana kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuona video ile alikuwa mama wa msichana. “Alikimbia polisi kwenda kutoa taarifa,”alisema Betty.
Baada ya kufika Polisi, Betty alisema polisi walimwambia mama huyo hawawezi kuandika maelezo hadi mhusika ambaye ni binti yake afike kituoni. Walisema hivyo kwa sababu ni mtu mzima hivyo anatakiwa kutoa maelezo mwenyewe. Saa chache baada ya kuandikisha maelezo yake, polisi waliwakamata vijana wawili kwa tuhuma za kuhusika na unyama huo. Betty alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi na leo watafikishwa mahakamani.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi na kwamba hadi jana watuhumiwa 11 walikamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Kamanda Matei alisema tisa kati yao wanaoshikiliwa ni kwa kosa la kusambaza picha za utupu huku vijana wawili ambao ni Zuberi Thabiti (30) na Iddy Adamu (32) ni kwa kosa la kufanya mapenzi na msichana huyo kwa nguvu huku wakirekodi.
Ilivyokuwa
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Matei alisema kuwa watuhumiwa hao walifanya kitendo hicho Aprili 28 mwaka huu majira ya saa 1.00 usiku katika nyumba ya kulala wageni yenye jina la ‘Titii’ iliyopo Dakawa.
Kamanda Matei alisema kuwa binti huyo aliitwa kwenye nyumba hiyo ya wageni na Thabiti ambaye ni mkazi wa Mbarali wilaya ya Mbeya ambaye alikuwa na uhusiano naye kimapenzi. Baada ya kuingia chumbani alimkuta pia Adamu mkazi wa Makambako, Njombe ambao walimlazimisha kufanya mapenzi huku mmoja akimrekodi picha za video na baadaye kuzisambaza kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Wanaoshikiliwa kwa kosa la kusambaza picha za utupu ni Rajabu Salehe (26), Said Athman (26), Musi Ngai (36), Said Muhammed (24), John Peter (24), Hassan Ramadhan (27), Ramadhan Ally (26), Lulu Peter (38) na Magreth Njonjone (30).
Wote ni wakazi wa Dakawa, Morogoro na wamevunja Sheria ya Makosa ya Mitandao, kifungu namba 14, kifungu kidogo (1) (a)
Kamanda Matei alisema wakati wa tukio hilo watuhumiwa hao walimtisha binti huyo kwa kisu ili asipige kelele wakati akidhalilishwa na walimtaka asitoe siri hiyo vinginevyo watamuua.
Kamanda alisema wawili hao ni marafiki wa msichana huyo na kwamba Thabiti ambaye ni mpenzi wa sasa wa msichana huyo alipanga na Adamu ambaye ni mpenzi wake wa zamani kumkomesha.
Alisema Thabiti alimwambia mpenzi wake wakutane hotelini. Msichana alipofika aliwakuta chumbani huku Adamu akiwa ameshika kisu na kamera. “Wakamlazimisha afanye vile na kumtishia kumuua kama angekataa,”alisema Matei.
Hata hivyo, Betty alisimulia kisa hicho na kusema watuhumiwa hao walifanya unyama huo kwa sababu ya usaliti wa mapenzi. Alisema msichana alidaiwa kujihusisha kimapenzi na dereva wa mpenzi wake.
Kwa mujibu wa Betty, baada ya mpenzi wake kugundua alipanga njama ili kuwakomoa wote wawili. Alisema mpenzi wake alimwambia wakutane hotelini na alipofika alimkuta Zuberi pamoja na dereva wa mchumba wake hotelini.
“Akawambia wafanye kile kitendo huku akirekodi video,”alisema Betty. “Nia yake ilikuwa kuwakomoa…kwa nini atembee na dereva wake,”alisema Betty na kwamba baada ya hapo picha hizo zilianza kusambaa.
Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema hali hiyo inaonyesha jinsi maadili yanavyozidi kuporomoka katika jamii.
“Hilo siyo kosa la kisheria peke yake ni udhalilishaji mkubwa,”alisema.
Dk Hellen alisema licha ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kukemea suala hilo ni vyema jamii ikazingatia suala la maadili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Edda Sanga alisema vyama vya kutetea haki za wanawake vinafanya mkutano wa pamoja kujadili suala hilo.
“Leo (jana) tumekutana ili tujadili na kuja na tamko la pamoja,”alisema Sanga na kuongeza kwamba jambo hilo halivumiliki kwa sababu vitendo kama hivyo vinaendelea kujitokeza mara kwa mara.
Tuesday, May 17, 2016
Mama atumiwa picha bintiye akidhalilishwa
Published Under
MATUKIO
About Author
BLOG NAMBA MMOJA KWA MATANGAZO YA AJIRA NA NAFASI ZA KAZI TANZANIA. Soma zaidi