Kama vile mmea unavyoweza kupandwa kwenye mbolea ukaota, kukua na baadaye kuzongwa na magugu ambayo huudumaza na hatimaye kama hayatang’olewa kuua, ndivyo ndoto za mwanadamu na mafanikio yanayoweza kujengewa tabia njema ya kukua lakini baadaye tabia mbaya ambazo huja na mafanikio zikaua kila kitu.
Ili mwanadamu afanikiwe maishani mwake ni lazima awe na tabia pamoja na mwenendo unaovuta au kuchochea mafanikio, zipo tabia za namna hiyo maishani ambazo mwanadamu akizifanya na kuzifanya ziwe sehemu ya maisha yake, mafanikio humfuata hata kama hayataki! Lakini ziko tabia ambazo mwanadamu anaweza kuzianzisha maishani mwake, zikaota mizizi na kuwa sehemu yake, ambazo hukwamisha kabisa mafanikio na hata kama kuna kipaji zinaweza kukiua kisimletee manufaa yoyote maishani.
Wapo watu wengi waliozaliwa na vipaji vya kuimba, kuandika, kucheza mpira na kadhalika lakini kwa sababu ya tabia fulani walizozianzisha maishani mwao, vipaji hivyo vilikufa kama ambavyo mmea hufa ukizongwa na magugu.
Tabia mbaya zinatesa watu, zimerudisha watu nyuma, zimefanya watu waliotakiwa kuwa mabilionea wafe wakiwa maskini, waliotakiwa kuandika vitabu au kugundua dawa za kutibu magonjwa, walikufa bila kufahamu kwamba hiyo ndiyo ilitakiwa kuwa hatima yao kwa sababu ya tabia mbaya ya hofu.
Tabia zote mbaya na nzuri hujengwa, hakuna mwanadamu aliyezaliwa na tabia mbaya au nzuri, zote tumezitengeneza sisi wenyewe wakati tunakua, nazo baadaye hugeuka kuwa vichocheo au vigingi vya sisi kuelekea kwenye mafanikio! Kila mwanamke anapozaa mtoto, watu husema tu “mama fulani amezaa mtoto wa kike au wa kiume!” Hakuna mwanamke hata mmoja ambaye huzaa halafu watu wakasema “leo mama fulani amezaa jambazi” au “mama fulani amezaa mteja wa unga!” au “mama fulani amezaa mzinzi!” wanawake wote huzaa watoto wazuri wanaovutia, lakini watoto hawa ukiwafuatilia baadaye maishani mwao huishia kuwa na tabia fulani ambazo hawakuzaliwa nazo, bali walijifunza wakati wanakua.
Ziko tabia zinazochochea maendeleo au kuvuta mafanikio kumfuata mtu, ukiwaangalia watu wengi waliofanikiwa maishani huwa na tabia za kufanana na miongoni mwa tabia hizo ni; UADILIFU, UAMINIFU, USEMA KWELI, DHAMIRA NA UCHAPAKAZI NA HOFU YA MUNGU.Mtu mwadilifu na mwaminifu huwavuta watu wengi sana kufanya naye kazi, watu wengi wanataka kuhusiana na watu waaminifu na waadilifu badala ya matapeli na watu waongo wasiosema ukweli! Vilevile watu wavivu wasio na dhamira ya kufanikiwa na hata wasio na hofu ya Mungu, huvuta watu wachache sana kushirikiana nao.
Watu wengi wenye tabia mbaya hujitenga wao wenyewe au kutengwa na jamii bila kufahamu, kwa sababu hiyo bahati ambazo siku zote maishani mwetu huletwa na watu huwa haziwafikii kirahisi kwa sababu sifa zao mbaya huwa zimesambaa! Hivyo basi mwanadamu anaweza kuwa hana fedha, lakini sifa yake ya uadilifu na uaminifu ikamfanya aungane na mtu mwenye fedha anayetafuta watu wa kushirikiana nao, ndiyo maana kuna msemo usemao uaminifu ni mtaji.
Kama tunataka kufanikiwa maishani ni vizuri sana kujiepusha na tabia mbaya ambazo tumezitengeneza wenyewe maishani mwetu na zimegeuka kuwa vikwazo au vigingi kwenye maendeleo, tabia hizi zipo, lazima ziondolewe kama kweli mtu amedhamiria kubadilisha maisha yake.
Hakuna mwanadamu aliyekamilika kila mmoja wetu analo eneo fulani maishani mwake ambalo anapambana ili awe bora, hivyo basi kama unafahamu tatizo lako ni matumizi mabaya ya fedha au ulevi au uzinzi au matumizi ya dawa za kulevya, tabia ambazo zimekukwamisha kusonga mbele ni lazima uziue tabia hizo mara moja ili upate kufanikiwa.
Ni kweli ni kazi ngumu sana kuua tabia ambayo umeijenga kwa muda mrefu, lakini inawezekana kabisa kufanya hivyo, utaumia lakini baadaye utasikia furaha! Si lazima uikate tabia hiyo mara moja, unaweza kupunguza kila siku hatimaye ukakata mizizi yake kabisa.
Mfano kama unakunywa bia ishirini kila siku na hizo ndizo zinazomaliza fedha zako ambazo ungezitumia kujenga nyumba au kuwekeza, unaweza kupunguza bia mbilimbili kila siku hatimaye siku moja utajikuta hujanywa bia kabisa na kuendelea na maisha hayo.
Wakati unapunguza bia unakuwa na jambo jema unalolianzisha kwa ajili ya kuchukua nafasi ya bia huku ukiwaepuka marafiki ambao siku zote walikuchochea kuendelea na tabia hiyo. Haya yakifanyika unaweza kung’oa tabia zote mbaya katika maisha yako na kuanzisha tabia njema zitakazokuwezesha kusonga mbele.