Akiwa ameshika upaja wa nyama ya mbwa.
TANGA: Kitendo cha kijana aliyefahamika kwa jina la Zakaria Swaki, mkazi wa Kijiji cha Mlalo, wilayani Lushoto mkoani Tanga kukutwa na hatia ya kuwalisha watu nyama ya mbwa kimezua taharuki huku wengi wakidai kuwa, kwa hali ilivyo watakuwa hawawaamini wauza nyama.
Wakizungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, wananchi hao wa Mlalo na viunga vyake walisema walikuwa wanatilia shaka nyama aliyokuwa akiuza kijana huyo hivyo kutiwa kwake hatiani kunaonesha alianza kufanya hivyo muda mrefu.
“Kwa kweli nimeshitushwa sana na taarifa hii, sina hata hamu ya kula tena nyama maana inavyoonekana amewauzia watu nyama hiyo kwa muda mrefu,” alisema Jamali Shemshahuo, mkazi wa Kijiji cha Ngazi. Naye Mama Jenny anayefanya biashara ya kuuza pombe za kienyeji maeneo ya Misheni alisema:
“Niliwahi kununua nyama kwa yule kijana lakini niliitilia shaka licha ya kwamba niliipika na kuwauzia wateja wangu. “Halafu sasa, wapo walioisifia supu yake kuwa ni tamu, kumbe maskini nilikuwa nawalisha nyama ya mbwa. Yule kijana akafungwe tu maana ametutia kwenye dhambi kubwa ila tumepata fundisho la kutojinunulia nyama mtaani.”
Kijana huyo alitiwa mbaroni hivi karibuni kufuatia tuhuma za kwamba amekuwa akiwauzia wananchi nyama ya mbwa ambapo alifikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Mlalo na akakiri kufanya kosa hilo. Kufuatia kukiri huko, kijana huyo alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela ambapo ameshaanza kukitumikia katika Gereza la Lushoto.