Siku chache baada ya Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza kufanya mikutano nchi nzima kwa lengo la kuishtaki kwa wananchi Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, CCM wamejibu mapigo kwa kuapa kuwafuata kila kona watakayopita.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka alisema kuwa chama hicho hakiwezi kuvumilia kuona Chadema wanazunguka kuharibu taswira ya Rais Magufuli na Serikali yake ambayo alieleza kuwa imefanya kazi kubwa kuwatumikia wananchi katika kipindi kifupi.
Alisema kuwa wamepata taarifa zisizo na shaka kuwa Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana Mei 16 mwaka huu ilibaini kuwa kwa muda mfupi, Magufuli ametekeleza ajenda zote ilizokuwa ikinadi wakati wa Uchaaguzi Mkuu.
Ole Sendeka alisema kuwa utendaji wa Rais Magufuli unatuma ujumbe wa dhahiri kuwa Chadema watashindwa tena katika uchaguzi wa mwaka 2020.
Aliongeza kuwa malalamiko ya udikteta wanayoyasambaza yanaonesha kuwa hawana mjadala wowote wa kumkosoa Rais Magufuli.
“Tunawaonya viongozi wa Chadema. Wanapaswa kutumia majukwaa hayo kunadi sera za Chadema. Nataka kuwahakikishia kuwa, kama Chadema wataenda sehemu fulani Jumatatu, sisi tutakuwa pale Jumanne kusafisha hali ya hewa kwa kuwaeleza ukweli wananchi,” alisema Ole Sendeka.
Chadema wamepanga kufanya mikutano nchi nzima kwa kile walichoeleza kuwa ni kuishtaki Serikali kwa wananchi kuhusu mwenendo wa Serikali ikiwa ni pamoja na kubanwa kwa Demokrasia na Bunge kwa ujumla na utumbuaji majipu usiofuata sheria na taratibu.